WAKATI Mbeya City ikitimkia Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara kwa ajili ya mechi yake dhidi ya Singida Black Stars, kocha mkuu wa timu hiyo, Mecky Maxime ameonesha kuridhishwa na ubora wa kikosi chake haswa straika, akiahidi furaha kwa mashabiki.
Hata hivyo, timu hiyo haikusita kueleza kilio chake kwa kutumia uwanja wa ugenini kwa mechi za nyumbani ikiwa ni kuwaathiri kiuchumi na kupoteza nguvu ya nje ya uwanja kwa kukosa mashabiki wake.
Mbeya City imeamua kutumia uwanja huo baada ya Sokoine uliopo jijini Mbeya kufungiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kukosa sifa za kikanuni ikiwa ni muda mchache baada ya timu hiyo kushinda mabao 3-0 dhidi ya Bandari Tanzania kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho la CRDB hatua ya 32 Bora.
Timu hiyo inatarajia kuwa uwanjani Machi 15, 2026 kuikaribisha Singida Black Stars, ikiwa ni mechi ya Ligi Kuu Bara, huku ikiwa na rekodi nzuri ya kupata matokeo mazuri uwanja wa ugenini.
Tangu kuanza Ligi Kuu msimu huu, Mbeya City haijapata ushindi Uwanja wa Sokoine, huku ushindi wa mechi tatu ikiupata ugenini dhidi ya Fountain Gate (0-1), KMC (0-3) na TRA United (0-2). Inashika nafasi ya 14 katika msimamo ikiwa na pointi 13.
Maxime ameliambia Mwanaspoti kuwa, kwa muda ambao ligi imesimama wamekuwa na maandalizi mazuri ambapo matokeo ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Bandari Tanzania yameongeza nguvu mpya kikosini.
Amesema kutokana na kasi waliyoonesha nyota wake haswa sehemu ya ushambuliaji, inatoa mwanga kwa timu hiyo kufanya vizuri, akieleza kuwa anafahamu ugumu wa mechi dhidi ya Singida BS lakini wanahitaji ushindi.
“Kwa muda mrefu Sokoine imekuwa ngumu kwetu kupata ushindi, lakini juzi uliona tunacheza vizuri vijana wanatengeneza nafasi nyingi na kuweza kushinda mabao 3-0, kiwango kile kilionesha ari na nguvu mpya.
“Kwa sasa akili na nguvu zipo kwenye mchezo dhidi ya Singida Black Stars kuhakikisha tunaendeleza ushindi ili kujiweka nafasi nzuri ukizingatia hatuko pazuri tunahitaji pointi tatu,” amesema Maxime.
Kwa upande wa Ofisa Habari wa Mbeya City, Gwamaka Mwankota, amesema kufungiwa Uwanja wa Sokoine ni kuingia gharama kubwa, kupoteza nguvu ya mashabiki wake na wajasiriamali kukosa fursa za kiuchumi.
“Ka ujumla tumekubali na kutii kanuni, sheria na taratibu za soka nchini kwa kuhamia Tanzanite Kwaraa Babati, tunaomba mashabiki mkoani Manyara watupokee na kutupa ushirikiano,” amesema Mwankota.