Chadema yaiambia UN mabadiliko ya kikatiba muhimu Tanzania

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemweleza Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa(UN) kuwa msimamo wa chama hicho ni uchunguzi huru ufanyike ili wale wote waliobainika kuhusika na vurugu za Oktoba 29,2025  zilizosababisha vifo na majeruhi wawajibishwe.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa jana Jumanne  Machi 10,2026 Chadema, wametoa  msisitizo huo  mbele ya mwakilishi maalumu wa UN, Parfait Onanga-Anyanga aliyekutana na ujumbe viongozi hao wakiongozwa na John Mnyika ( katibu Mkuu) na Dk Rugemeleza Nshala (mwanasheria mkuu wa chama hicho).

Mazungumzo hayo yamefanyika ofisi ya UN zilizopo jijini Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine wamejadili kwa kina hali  ya siasa nchini kufuatia matukio ya Oktoba 29, 2025 na athari zake.

Katika taarifa hiyo, Mnyika alimpatia mwawakilishi huyo uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho  ambao ni msimamo wa chama uliotolewa kwa umma Desemba 11, 2025.

“Chadema inaendelea kusisiza kutaka kufanyike uchunguzi utakaofanywa na chombo huru ili kubaini wote waliohusika kuua, kujeruhi na kupoteza watu Oktoba 29 na kuwawajibisha wote watakaobainika kuhusika.”

“Tunasisitiza kufanyike mabadiliko ya kikatiba yatakayowezesha kuwepo kwa chaguzi huru na haki nchini,” amesema Mnyika.

Tayari mwakilishi huyo maalumu ameshakutana na uongozi wa ACT Wazalendo, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya  Siasa  ambapo pia  atakutana na makundi mengi  wakiwemo viongozi wa CCM.