Arusha. Mahakama ya Rufani imebatilisha hukumu ya kifungo cha miaka 20 jela aliyokuwa amehukumiwa raia wa kigeni, Lonie Rayford na kuamuru aachiwe huru baada ya kubaini kuwa hapakuwepo ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), ya kusikilizwa kwa kesi yake.
Raia huyo alidaiwa Julai 4, 2018 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam alisafirisha dawa za kulevya aina ya heroini yenye uzito wa kilo 2.188.
Awali, Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mei 26, 2023 ilimuhukumu kifungo cha miaka 20 jela baada ya kumkuta na hatia.
Raia huyo alishtakiwa na kutiwa hatiani kwa kosa hilo kinyume na kifungu cha 15(1)(a) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019 na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).
Kifungu hicho kilisomwa pamoja na aya ya 23 ya Jedwali la Kwanza la sheria na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Kudhibiti Uhalifu wa Kiuchumi na Kuratibu (EOCCA).
Uamuzi wa kubatilisha hukumu hiyo na kuifuta ulitolewa jana Machi 10, 2026 na jopo la majaji wa Mahakama ya Rufani ambao ni Augustine Mwarija, Panterine Kente na Zainab Muruke.
Ilielezwa kuwa mahakama iliyosikiliza kesi hiyo haikuwa na mamlaka ya kusikiliza na kuamua shauri hilo kwa sababu idhini ya DPP iliyotumika kuanzisha mashtaka haikutaja kifungu sahihi cha sheria kilichodaiwa kukiukwa.
Kutokana na kasoro hiyo ya kisheria, Mahakama ya Rufani iliamua kubatilisha mwenendo wote wa kesi katika Mahakama Kuu, kufuta hatia ya mrufani na kuweka kando adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela aliyokuwa amepewa.
Jaji Kente alisema Mahakama imebaini kuwa mashtaka dhidi ya mrufani yaliwasilishwa kama kosa la uhujumu uchumi chini ya sheria tajwa hapo juu, ambapo kwa mujibu wa kifungu cha 26(1) cha sheria hiyo, mashtaka hayo hayawezi kuanzishwa bila idhini ya DPP.
Mahakama ilibaini kuwa idhini iliyotolewa na DPP haikurejea kifungu mahsusi cha sheria kinachounda kosa lililokuwa linamshtaki mrufani, yaani kifungu cha 15(1)(a) cha Sheria ya DCEA, na badala yake idhini hiyo ilirejelea kwa ujumla tu aya ya 23 ya Jedwali la Kwanza la EOCCA bila kutaja wazi kifungu hicho.
Jaji alisema kwa mujibu wa msimamo wa kisheria uliowekwa katika maamuzi ya awali ya Mahakama hiyo, idhini ya DPP lazima irejelee moja kwa moja kifungu cha sheria kinachounda kosa linaloshtakiwa, vinginevyo idhini hiyo huwa batili na haiwezi kuipa mahakama mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Kwa kuzingatia kanuni hiyo, Mahakama ilihitimisha kuwa Mahakama Kuu iliendesha kesi bila kuwa na mamlaka ya kisheria kwa sababu mashtaka yaliyoanzishwa dhidi ya mrufani hayakuwa na idhini halali ya DPP kama inavyotakiwa na sheria.
Jaji alisema kuwa kutokana na kasoro hiyo ya msingi ya kisheria, mwenendo wote wa kesi pamoja na hukumu iliyotolewa dhidi ya mrufani unaonekana kuwa batili tangu mwanzo.
Mahakama hiyo iliagiza mrufani aachiliwe huru mara moja kutoka gerezani isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali za kisheria.
Katika kesi ya msingi mahakamani hapo, ilidaiwa mahakamani kuwa siku hiyo maofisa wa Jeshi la Polisi pamoja na wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) walipokea taarifa za kiintelijensia kwamba Rayford alikuwa akijihusisha na biashara ya dawa za kulevya na alikuwa anatarajiwa kusafiri kutoka Tanzania kwenda Marekani.
Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, maofisa hao walifika katika eneo la abiria wanaoondoka katika uwanja huo na kumkamata mrufani pamoja na mizigo yake miwili. Baada ya upekuzi kufanywa katika moja ya mizigo hiyo, ilidaiwa kubainika kuwepo kwa vifurushi vilivyokuwa na dawa za kulevya aina ya heroini.
Baada ya kukamatwa, upande wa mashtaka ulidai kuwa mrufani alihojiwa na maofisa wa uchunguzi na kukiri kuwa dawa hizo zilikuwa zake na kwamba alikuwa akizisafirisha kutoka Dar es Salaam kwenda Bologna, Italia.
Kwa upande wake, Rayford alikanusha tuhuma zote dhidi yake na kudai kuwa dawa hizo hazikuwa zake na kwamba hakukamatwa akiwa na dawa zozote za kulevya katika mizigo yake au mwilini mwake.
Alidai pia kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka haukuwa wa kweli na haukuweza kuthibitisha bila shaka kuwa yeye ndiye aliyekuwa akisafirisha dawa hizo.
Hata hivyo, baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, Jaji wa Mahakama Kuu aliyesikiliza kesi hiyo aliamua kuwa upande wa mashtaka ulikuwa umethibitisha shtaka dhidi ya mrufani kwa kiwango kinachotakiwa kisheria.
Jaji huyo aliamini ushahidi wa mashahidi wa mashtaka kwamba dawa hizo zilipatikana katika mizigo ya mrufani. Mahakama pia ilizingatia kuwa mrufani alisaini hati ya kukiri ukamataji wa vitu hivyo, akitambua kuwa vilikuwa vyake.
Rayford alikata rufaa katika Mahakama ya Rufani akipinga uamuzi huo kwa kuwasilisha sababu kadhaa. Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, Mahakama ilibaini suala muhimu kuhusu idhini ya DPP iliyotumika kuanzisha mashtaka dhidi ya mrufani.
Majaji walieleza kuwa kwa mujibu wa sheria za makosa ya kiuchumi, idhini ya DPP ni sharti muhimu kabla ya kesi kama hiyo kuanza kusikilizwa mahakamani.
Hata hivyo, katika kesi hiyo idhini iliyotolewa ilitaja tu kifungu cha sheria kinachohusiana na makosa ya kiuchumi bila kutaja kifungu mahsusi cha sheria ya dawa za kulevya kinachounda kosa aliloshtakiwa nalo mrufani.
Kwa mujibu wa majaji, kasoro hiyo ilimaanisha kuwa Mahakama Kuu haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo tangu mwanzo.
Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, upande wa Jamhuri ulikiri kuwa kulikuwa na kasoro katika idhini hiyo ya DPP na kukubali kuwa kutotajwa kwa kifungu mahsusi cha sheria kulimaanisha kuwa mashtaka hayakuanzishwa kwa mujibu wa sheria, hivyo Mahakama Kuu haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Hata hivyo, uliomba Mahakama ya Rufani iamuru kesi hiyo isikilizwe upya ili haki itendeke. Hoja hiyo ilipingwa na wakili wa utetezi akisema kufanya hivyo kungemletea mrufani madhara makubwa kwa sababu tayari alikuwa amekaa gerezani kwa muda mrefu tangu kukamatwa kwake mwaka 2018.
Alieleza pia kuwa kuamuru kesi mpya kungeipa nafasi upande wa mashtaka kurekebisha mapungufu yaliyokuwapo katika kesi yao ya awali, hivyo kuiomba Mahakama ibatilishe kesi yote, kufuta hatia na kumwachia huru mrufani bila masharti.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Mahakama ya Rufani ilikubaliana na hoja kwamba idhini ya DPP ilikuwa na kasoro kubwa ya kisheria.
Majaji walieleza kuwa kwa mujibu wa sheria, idhini hiyo lazima itaje vifungu mahsusi vya sheria vinavyodaiwa kukiukwa ili kuipa mahakama mamlaka ya kusikiliza kesi.
Walibainisha kuwa kutokuwepo kwa rejea ya kifungu cha 15(1)(a) cha Sheria ya Dawa za Kulevya kulifanya idhini hiyo kuwa batili. Mahakama pia ilirejea maamuzi yake ya awali katika kesi nyingine zilizowahi kujadili suala kama hilo, ikisisitiza kuwa idhini isiyo sahihi ya DPP haiwezi kumpa mahakama mamlaka ya kusikiliza kesi ya aina hiyo.
Kutokana na hali hiyo, majaji waliamua kuwa mwenendo wote wa kesi katika Mahakama Kuu haukuwa halali. Baada ya kubatilisha kesi hiyo, Mahakama ilikataa kutoa amri ya kusikilizwa upya kwa kesi.
Majaji walieleza kuwa uamuzi wa kama mrufani atashtakiwa tena au la unabaki mikononi mwa DPP, hivyo kuagiza Rayford aachiliwe huru mara moja kutoka gerezani isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali za kisheria.