TGNP YAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI, YAHIMIZA USAWA WA KIJINSIA KUFIKIA DIRA 2050
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umeadhimisha Siku ya Wanawake Duniani 2026 kwa kufanya kongamano maalum lililofanyika tarehe 11 Machi 2026 katika Viwanja vya TGNP, Mabibo jijini Dar es Salaam, likilenga kuhamasisha haki na usawa kwa wanawake na wasichana kama msingi wa maendeleo jumuishi ya taifa.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP, Gemma Akilimali, amesema maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ni fursa muhimu ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana katika harakati za kupigania haki za wanawake pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha usawa wa kijinsia nchini.
Alisema maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu ya kitaifa isemayo “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi Kufikia Dira 2050,” ambayo inahamasisha jamii kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa katika nyanja zote za maendeleo.
Akilimali alisema kauli mbiu hiyo inakuja wakati muafaka ambapo Tanzania imeanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iliyozinduliwa Julai 2025, akisisitiza kuwa mafanikio ya dira hiyo yanategemea ushiriki sawa wa wanawake na wanaume katika maendeleo ya taifa.
“Mwaka huu Siku ya Wanawake Duniani si maadhimisho tu, bali ni wito wa kuchukua hatua madhubuti za kuondoa vikwazo vya kimfumo vinavyozuia upatikanaji wa haki sawa kwa wanawake na wasichana,” alisema Akilimali.
Alibainisha kuwa kumekuwa na hatua mbalimbali chanya nchini katika kuimarisha usawa wa kijinsia, ikiwemo kuimarishwa kwa Bajeti yenye Mtazamo wa Kijinsia (Gender Responsive Budgeting – GRB) pamoja na utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA II).
Kwa upande wa uwakilishi wa wanawake katika vyombo vya maamuzi, alisema kumekuwa na maendeleo ambapo kwa sasa wanawake wanashikilia takribani asilimia 39.5 ya viti vya Bunge, ikilinganishwa na asilimia 37.4 baada ya uchaguzi wa mwaka 2020.
Aidha, alisema wanawake ni zaidi ya asilimia 51.3 ya Watanzania kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, jambo linaloonesha umuhimu wa kuwapa nafasi sawa katika maendeleo ya taifa.
Akilimali pia alikumbusha kuwa Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda inayolenga kulinda haki za wanawake, ikiwemo Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu (UDHR), Mkataba wa Kutokomeza Aina Zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW), Mpango Kazi wa Beijing, pamoja na Itifaki ya Jinsia na Maendeleo ya SADC.
Alisisitiza kuwa kuwekeza kwa wanawake ni uwekezaji wa kimkakati unaochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Niwakumbushe kanuni moja muhimu: Mwanamke akiendelea, jamii nzima inapiga hatua. Kuwekeza kwa mwanamke ni msingi wa kujenga jamii jumuishi na yenye maendeleo,” alisema.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Clara Kalanga, alisema dunia mwaka huu inaadhimisha miaka 115 tangu kuanza kwa Siku ya Wanawake Duniani mwaka 1911, huku Tanzania ikiwa katika kipindi muhimu cha kuanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Alisema maadhimisho ya mwaka huu yanaambatana pia na kampeni ya kimataifa ya “ToaIliUpate (Give to Gain)”, inayohamasisha watu binafsi, mashirika na jamii kushiriki kikamilifu katika kuendeleza usawa wa kijinsia kupitia utoaji wa rasilimali, maarifa, ushauri na mafunzo.
Kalanga aliongeza kuwa TGNP kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa shughuli kadhaa katika mwezi mzima wa Machi, ikiwemo maadhimisho katika ngazi ya jamii kupitia Vituo vya Taarifa na Maarifa katika zaidi ya kata 90 kutoka mikoa 13 nchini kuanzia tarehe 1 hadi 31 Machi 2026.
Aidha, alisema tarehe 17 Machi 2026 kutafanyika Kongamano la Vijana, huku kuanzia tarehe 25 hadi 27 Machi 2026 kukifanyika maadhimisho ya kimataifa yatakayowakutanisha wadau kutoka nchi za India, Haiti, Ethiopia, Bangladesh, Canada na Tanzania.
Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP, Gemma Akilimali akizungumza wakati wa kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani 2026 kwa kufanya kongamano maalum lililofanyika tarehe 11 Machi 2026 katika Viwanja vya TGNP, Mabibo jijini Dar es Salaam.