Dar es Salaam. Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) imekuja na kanuni maalumu ambazo zinalenga kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kudhibiti baadhi ya vitendo vinavyoumiza wafanyabiashara ikiwemo kuandaa maonyesho yasiyoweza kuleta tija.
Hayo yameelezwa katika kikao cha pamoja na wadau kilichoandaliwa na Tantrade kwa ajili ya kujadili kanuni hizo kilichofanyika leo Machi 11, 2026 jijini Dar es Salaam.
Amesema lengo la kufanya hivyo ni kutengeneza taratibu za kuwezesha biashara ambazo ni shirikishi zitakazokuza ufanyaji wa shughuli hizo kwa kinamama, vijana na wanawake.
Kaimu Meneja kitengo cha uwezeshaji biashara Tantrade, Deo Shayo amesema kumekuwa na matukio mengi ya ukuzaji biashara hivyo ni muhimu kuboresha taratibu, yaweze kuwa na manufaa, yapunguze utapeli na kuleta tija kwa nchi na kuitangaza katika maeneo mbalimbali ya kiuwekezaji.
Tunashirikisha watu katika hizi kanuni ili kuhakikisha wanafanikisha biashara zao na kujenga uchumi wa nchi.
Amesema wanatarajia kanuni hizo zikiwa rasmi zitakuza biashara na si kukwaza biashara zinapofanyika.
Akielezea moja ya eneo ambalo linaguswa ni uandaaji wa maonyesho ya biashara lakini hayana hadhi kuanzia programu zinavyokwenda huku wengine wakitaja uwepo wa viongozi wa kitaifa jambo ambalo si kweli.
Amesema Tantrade wana utaratibu wa kuratibu itifaki kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje kiasi cha kuwafanya kuwa na uwezo wa kujua mgeni gani akienda atapokewa vipi.
“Lakini sasa tasnia inakuwa kama imevamiwa kuna ambao wanaibuka na wanashindwa kufanya tunapokea malalamiko. Unaweza kukuta mtu ameanzisha tukio la kibiashara lakini watu wanaimba mapambio pale au ni tukio ambalo watu wamechangishwa fedha za gharama kwenye mabanda hakuna watembeleaji wala tija,” amesema.
Amesema kanuni hizo hazilengi kukwaza biashara na endapo itafikia hatua mwandaaji amechukuliwa hatua basi anakuwa amevunja sheria kwa kiwango kikubwa.
Kwa mujibu wa kanuni pendekezwa mtu anayetaka kuandaa maonyesho ni lazima apewe kibali kulingana na ukubwa wa shughuli anayotaka kufanya.
Kwa anayeandaa maonyesho yenye gharama za zaidi ya Sh31 milioni atapaswa kulipa ada Tantrade ya Sh2.36 milioni kwa ajili ya kupata kibali na wale ambao gharama ni chini ya Sh30 milioni watalipia Sh1 milioni.
Kwa wanaoandaa mikutano ya wanunuzi na wauzaji gharama ni Sh2.36 milioni, jukwaa la biashara Sh2.36 milioni na mikutano mingine ya kibiashara atapaswa kulipia Sh1 milioni.
Ofisa Sheria wa TanTrade, Francis Lemelo amesema rasimu ya kanuni hizo imeandaliwa ili kusaidia wadau mbalimbali katika sekta ya biashara ukigusa maeneo matano muhimu.
Maeneo yaliyoguswa ni kanuni za kufifilisha makosa za Tantrade 2026, kanuni za kuratibu ushirikiano na majukumu ya taasisi mbalimbali za Serikali, sekta binafsi zinazohusiana na biashara za mwaka 2026.
Pia kuna kanuni za mamlaka za maendeleo ya biashara (tozo) za mwaka 2026 na kanuni za matumizi ya alama za rajami ya raifa (huduma za bidhaa) za mwaka 2026.
“Mageuzi haya ni sehemu ya juhudi pana za kurahisisha sera na mifumo ya udhibiti ili kuendana na mabadiliko yanayoendelea katika sekta ya biashara.
Walengwa wakuu wa mabadiliko haya yanayopendekezwa ni pamoja na biashara ndogo, za kati na kubwa, wauzaji wa bidhaa nje ya nchi na wale wanaotarajiwa kuanza kuuza nje, pamoja na vyama vya wafanyabiashara na taasisi za sekta binafsi,” amesema.
Akitoa maoni yake, kiongozi wa kampuni ya Woiso, Michael Mramba amesema kanuni hizo zitawaweka pamoja wafanyabiashara kwani awali hazikuwa kimkakati na kushindwa kutatua changamoto zilizokuwapo.
“Lakini kwa namna hii tunakwenda kukuza uchumi wa biashara na kuleta Pamoja wafanyabiashara wa ndani na nje, tulikuwa tukitoa maoni mbalimbali wakati wa maonyesho tulikuwa tunaona kimya kumbe kulikuwa na mkakati mkubwa unaandaliwa ambao unajibu changamoto hizo,” amesema.