Ilichokisema CCM mbele ya mwakilishi wa UN

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitaendeleza dhamira yake ya  muda mrefu wa kuheshimu utawala wa sheria, kidemokrasia na ushiriki wa kisiasa kwa njia za amani.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro wakati akikiwakilisha chama hicho katika mazungumzo na Balozi Parfait Onanga-Anyanga, Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa kwa Umoja wa Afrika (UNOAU).

Balozi Onanga-Anyanga yupo nchini Tanzania kama Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, akikutana na makundi mbalimbali kama sehemu ya juhudi za taasisi hiyo ya kidiplomasia ulimwenguni kutafuta mwafaka wa mzozo wa kisiasa wa matukio ya Oktoba 29, 2025.

Taarifa ya Kenani Kihongosi, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM aliyoitoa leo Jumatano, Machi 11, 2026 imeeleza, chama hicho kimewakilishwa na Katibu Mkuu wake, Dk Asha Rose-Migiro.

“Dk Migiro amesisitiza dhamira ya muda mrefu ya Tanzania katika kuendeleza utawala wa kidemokrasia, ushiriki wa kisiasa kwa njia za amani na kuheshimu utawala wa sheria. Alibainisha kuwa Tanzania inaongozwa na misingi ya Mkataba wa Umoja wa Afrika kuhusu Demokrasia, Uchaguzi na Utawala, pamoja na viwango vya kimataifa vilivyowekwa katika Azimio la Ulimwengu la Haki za Binadamu na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa,” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha, Katibu Mkuu ameeleza mageuzi ya kisheria yaliyofanyika katika Tume ya Uchaguzi na taasisi nyingine, ikiwemo kutungwa kwa sheria mpya za uchaguzi mwaka 2024, hatua zilizolenga kuongeza uwazi, uwajibikaji na kuimarisha imani ya wananchi katika mchakato wa uchaguzi.

Taarifa hiyo inasema Dk Migiro amegusia pia matukio ya vurugu yaliyotokea katika baadhi ya maeneo wakati na baada ya uchaguzi mkuu, yaliyosababisha vifo na uharibifu wa mali, ikiwemo mashambulizi dhidi ya ofisi za CCM.

Aidha, amesema hatua stahiki zilichukuliwa kurejesha utulivu na amani nchini.

Kwa pamoja, CCM na Umoja wa Mataifa wamesisitiza umuhimu wa kuendeleza mazungumzo na maridhiano miongoni mwa wadau wa kitaifa.

Dk Migiro amemthibitishia Balozi Onanga-Anyanga kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika kuimarisha amani, usalama na maendeleo jumuishi.

“CCM imepongeza ushirikiano madhubuti uliopo kati ya Tanzania na Umoja wa Mataifa, na kuthibitisha dhamira yake ya kustawisha mshikamano wa kitaifa, utulivu na demokrasia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” imeeleza taarifa hiyo.