Chunya yaweka mikakati kuongeza uzalishaji wa ufuta

Chunya. Halmashauri ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, imeweka mikakati madhubuti ya kuongeza uzalishaji wa zao la ufuta kutoka kilo milioni 2.4 zilizozalishwa msimu uliopita hadi kufikia kilo milioni 6, katika msimu wa kilimo wa 2026/2027.

Hatua hiyo imechochewa na uamuzi wa halmashauri kugawa tani 6,000 za mbegu bora za ufuta kwa wakulima kupitia Chama cha Msingi cha Wakulima wa Ufuta cha Kilimo Kwanza (Kilimo Kwanza Amcos).

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Machi 11, 2026, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Gideon Mapunda amesema ongezeko hilo la uzalishaji linaenda sambamba na uhakika wa masoko ya ndani pamoja na juhudi za kudhibiti utoroshwaji wa zao hilo unaofanywa na baadhi ya watu wasio waaminifu.

Amesema katika msimu uliopita, ufuta uliuzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani chini ya usimamizi wa vyama vya msingi vya wakulima (Amcos), ambapo zaidi ya Sh5.179 bilioni zilipatikana kutokana na mauzo ya zao hilo.

Kwa mujibu wa Mapunda, mafanikio hayo yamehamasisha wakulima kuongeza juhudi katika uzalishaji ili kufikia lengo la kuzalisha kilo milioni 6 katika msimu ujao, hatua itakayosaidia kuongeza kipato cha wakulima na mapato ya halmashauri.

“Ili kufikia malengo tuliyojiwekea tayari tumetoa tani 6,000 za mbegu bora za ufuta. Aidha, Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (Copra) imetoa kilo 700 za mbegu hizo kwa lengo la kuwasaidia wakulima kuacha matumizi ya mbegu za marudio na kuongeza tija katika msimu wa 2026/2027,” amesema Mapunda.

Ameongeza kuwa halmashauri imejipanga kuhakikisha ufuta wote unauzwa ndani ya wilaya kupitia mfumo rasmi wa soko, huku hatua madhubuti zikichukuliwa kudhibiti utoroshwaji wa zao hilo. Pia amebainisha kuwa bei elekezi ya Serikali kwa sasa ni Sh2,390 kwa kilo moja.

Mapunda amesema hadi sasa wakulima 728 wamejiunga na vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) na wameanza kunufaika na mfumo wa stakabadhi ghalani kupitia usimamizi wa vyama vyao.

Amesema halmashauri imeamua kulifanya zao la ufuta kuwa la kimkakati ili kuongeza uzalishaji na kukuza mapato ya ndani yanayosaidia kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Awali, tulitegemea zaidi zao la tumbaku, lakini sasa tumeelekeza nguvu pia katika uzalishaji wa ufuta na tunaendelea kuhamasisha wakulima kujiunga na vyama vya msingi ili waweze kunufaika na kilimo chenye tija,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Tamim Kambona amesema wameweka mikakati ya kuhakikisha kunakuwa na maghala ya kutosha kwa ajili ya kuhifadhi na kununulia ufuta kutokana na umuhimu wa zao hilo kiuchumi.

“Kama halmashauri tutaendelea kuweka mazingira wezeshi katika sekta ya kilimo, hususan kwa mazao ya tumbaku na ufuta, ili kuongeza mapato ya halmashauri yanayowezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Wakulima wa Ufuta cha Kilimo Kwanza (Kilimo Kwanza Amcos), Peter Mayala ameishukuru halmashauri kwa kushirikiana na wakulima katika kuboresha miundombinu ya soko na maghala, jambo lililorahisisha upatikanaji wa soko la uhakika kwa zao hilo.

Mkulima Christian Ntaly amesema pamoja na jitihada zinazofanywa, bado kuna changamoto ya upatikanaji wa elimu ya kilimo bora cha ufuta pamoja na maeneo yanayofaa kwa uzalishaji wa zao hilo.

“Kimsingi hii ni fursa kubwa kwetu wakulima, lakini tunaomba Serikali iendelee kutoa elimu zaidi kuhusu kilimo cha ufuta na kubainisha maeneo yanayofaa kwa uzalishaji ili kuongeza tija na kuunga mkono mikakati ya halmashauri,” amesema.