SERIKALI imesema itakiunga mkono kituo cha Olympafrica Zanzibar kilichopo visiwani hapa kwa kukifanyia maboresho ya miundombinu kwani kinakuza vipaja vya michezo kwa watoto.
Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Rais Ikulu, Ufuatiliaji na Usimamizi wa Utendaji wa Serikali, Profesa Mohammed Hafidh Khalfan alipotembelea kituo hicho kilichopo Dole, Wilaya ya Magharibi A, Unguja.
Profesa Khalfan alisema kituo hicho kinasaidia kukuza vipaji vya michezo mbalimbali ndio sababu ya Serikali kutoa msaada wake. “Serikali inafanya uwekezaji mkubwa katika kujenga na kuboresha miundombinu mbinu, kwa hiyo ni muhimu kuvisapoti vituo kama hivi,” alisema.
Alisema moja ya majukumu ya ofisi yake ni kusimamia masuala ya miundombinu pamoja na huduma za jamii, zikiwemo sekta za michezo, afya na elimu, ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na kutoa manufaa yaliyokusudiwa.
Aliongeza kuwa, amevutiwa na huduma zinazotolewa katika kituo hicho ikiwemo kutoa fursa pana kwa vijana kukua katika maadili ya kimichezo.Â
“Serikali tayari imetumia fedha nyingi katika ujenzi na uimarishaji wa viwanja na miundombinu ya michezo, hivyo kuna wajibu wa kuhakikisha vituo hivyo vinaimarishwa na kuendelezwa ili kuleta tija iliyokusudiwa,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kituo hicho, Hussein Ali Ahmada, alisema ujio wa viongozi hao unawapa matumaini kwa sababu wamepata fursa ya kueleza changamoto na mafanikio yao.