Mikoani. Mvua zinazoendelea kunyesha katika baadhi ya mikoa nchini, zimesababisha vifo vya watu watano, uharibifu wa miundombinu ya majengo, barabara pamoja na kuathiri mazao.
Pia, zimesababisha upotevu wa muda kwa wananchi, wanafunzi kukosa masomo na kupanda kwa gharama za usafiri katika maeneo mbalimbali yanayoendelea kukumbwa na mvua hizo.
Mkoani Dodoma, mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia juzi imesababisha vifo vya watu watano katika wilaya za Kondoa, Chemba na Bahi.
Watu wawili kati ya waliopoteza maisha waliangukiwa na ukuta wa nyumba huku watatu wakisombwa na maji ya mvua.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera akizungumza leo Jumatano Machi 11, 2026 na Mwananchi amesema waliopoteza maisha ni Rukia Juma (26) aliyesombwa na maji katika Daraja la Magambi wilayani Chemba alipokuwa akijaribu kuokoa kiatu chake kilichochukuliwa na maji.
Baadhi ya nyumba zilizozingirwa na maji Mtaa wa Mageuzi Kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga baada ya mvua kubwa kunyesha.
Wengine ni Zakia Omari (60) na mjukuu wake Nasfati Mshana (8) waliokuwa wakivuka Mto Kalambachini wilayani Kondoa kabla ya kusombwa na maji, pamoja na Yareld Msomhola (72) na mjukuu wake Joseph Msomhola (9) walioangukiwa na ukuta wa nyumba katika Kijiji cha Lamaiti wilayani Bahi.
“Wito wangu kwa wananchi, katika kipindi hiki cha mvua wawe makini wanapotumia njia zenye maji. Wazazi wawe waangalifu kwa watoto na kuwafuatilia wanapokwenda na kurudi shule, ni muhimu kuchukua tahadhari,” amesema Hyera.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mahomanyika jijini Dodoma, Abraham Mputu amesema mvua hizo zimetenganisha mtaa huo katika pande mbili baada ya daraja kubomoka, hali iliyowafanya baadhi ya wakazi kushindwa kufika barabarani.
Mjini Moshi, mawasiliano katika baadhi ya maeneo yamekatika kutokana na ubovu wa barabara uliosababishwa na mvua.
Hali hiyo imewalazimu baadhi ya wakazi kushindwa kuingiza magari nyumbani kwao, hasa katika maeneo ya barabara za Bishop na Airport, Kata ya Korongo.
Mkazi wa Korongo, Leonard Msami amesema hali hiyo inawaletea usumbufu wananchi.
“Tunahitaji hatua za haraka kutoka serikalini. Barabara zetu zimegeuka kama mito, hakuna mahali pa kupita kwa vyombo vya usafiri wala watembea kwa miguu,” amesema.
Diwani wa Korongo, Issah Bulilo amesema baadhi ya barabara katika eneo hilo hazipitiki kutokana na kuharibiwa na maji ya mvua.
Wakazi wa mtaa wa Mgulu wa Ndege kata ya Mkundi wakipita katika korongo la Watumishi wakati wa ziara ya kamati ya maafa ya serikali ya mtaa huo kukagua athari za mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Morogoro. Picha na Juma Mtanda
Amesema barabara hizo zimekuwa mbovu kwa muda mrefu bila kufanyiwa matengenezo licha ya taarifa kuwasilishwa katika mamlaka husika.
Hata hivyo, Mwananchi imezungumza na Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) Wilaya ya Moshi, Cathbert Kwayu amesema tayari tathmini imefanyika na katika mwaka wa fedha 2026/27, wamepanga kufanya matengenezo ya kilomita mbili za barabara hizo kwa kiwango cha changarawe.
Huko Unguja, shughuli za biashara katika masoko ya Jumbi na Chuini zimesimama baada ya maji ya mvua kuingia maeneo hayo, hali inayodaiwa kusababishwa na kuziba kwa mitaro na njia za asili za maji.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma amesema licha ya maji kuingia katika masoko hayo, bado hakuna madhara makubwa yaliyoripotiwa isipokuwa usumbufu kwa wafanyabiashara na wateja.
Katika Manispaa ya Morogoro, wakazi wa Korongo la Watumishi wamesema mvua hizo zimeleta changamoto kubwa ya mawasiliano baada ya barabara kufungwa na maji.
Mkazi wa eneo hilo, Pendo Kisengi amesema hali hiyo imewafanya wakazi kujikuta kama wako kisiwani kwa sababu hawawezi kuvuka kwenda maeneo mengine.
Amesema iwapo mvua itaendelea kunyesha, mmomonyoko wa udongo unaoelekea kwenye korongo unaweza kuhatarisha barabara na hata nyumba zao.
“Kila mwaka udongo unaendelea kumeguka na nyumba zilizo karibu na korongo ziko hatarini. Tunaiomba Serikali iingilie kati kwa sababu uwezo wa mtu mmoja mmoja hautoshi na nyumba hizi zinaweza kusombwa na maji,” amesema.
Henry Sandy amesema Machi 6, 2026 nusura apoteze maisha baada ya sehemu aliyokuwa amesimama kuporomoka na kumfukia kwa udongo hadi kiunoni katika eneo hilo.
Mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Mkundi Mlimani, Jackline Samuel (16) amesema hulazimika kuchelewa shule au kutofika kabisa mvua zinaponyesha asubuhi kutokana na kushindwa kuvuka makorongo hayo.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mgulu wa Ndege, Beno Mbamba amesema mvua za hivi karibuni zimebomoa nyumba nne huku zaidi ya nyumba 50 zikiwa hatarini kubomoka kwa kuwa zimejengwa karibu na mkondo wa Korongo la Watumishi.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Shabaani Marugujo amewataka wananchi kuepuka kuvuka maji yanayotiririka kwa nguvu ili kuepuka ajali.
Katika Wilaya ya Kilosa, Mwenyekiti wa Kijiji cha Changarawe Kata ya Masanze, Nicholaus Mkoma amesema mafuriko yamesababisha hasara kubwa kwa wananchi baada ya kuharibu mazao na nyumba.
Amesema tathmini ya uharibifu inaendelea, bado hawajapata takwimu kamili za walioathirika.
“Zipo nyumba zimeanguka, nyingine zimejaa maji kiasi cha wananchi kushindwa kuishi ndani yake, huku mashamba mengi pia yakiwa yamejaa maji,” amesema.
Mkazi wa kijiji hicho, Josephat Maguno amesema mvua zinazoendelea kunyesha zinahatarisha maisha yao baada ya Mto Miyombo kujaa na kumwaga maji katika makazi ya watu na mashamba.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka amesema tayari Mkuu wa Mkoa wa Morogoro amefika katika maeneo yaliyoathirika kwa ajili ya kufanya tathmini ya uharibifu wa miundombinu na makazi ya wananchi.
Katika Jiji la Mwanza, wakazi pamoja na watumiaji wa Barabara ya Mwanza–Shinyanga inayokatiza katika Daraja la Mkuyuni jana Jumanne walikwama baada ya daraja hilo kufurika maji.
Baadhi ya wananchi walilazimika kupata msaada kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kuvuka eneo hilo baada ya magari kushindwa kupita kutokana na maji mengi yaliyofunika daraja.
Daraja la Mkuyuni ambalo mara kwa mara limekuwa likisababisha adha kwa watumiaji wa barabara hiyo, limefurika maji ikiwa ni siku chache tu tangu lianze kutumika baada ya kukamilika kwa maboresho yaliyofanywa na Serikali kwa gharama ya Sh14 bilioni.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya abiria wamelazimika kubadili njia au kutembea kwa miguu.
Mmoja wa abiria, Frolence Mbaraka amesema amelazimika kutembea kutoka Mswahili hadi Nyegezi baada ya daladala kushindwa kuendelea na safari kutokana na daraja hilo kufurika maji, hali inayoongeza gharama za maisha kwa wananchi hasa wanapolazimika kukodi pikipiki.
“Baada ya magari kukwama kwenye maji, daladala nyingi zilianza kurudia njia ya Igogo, hivyo abiria tulilazimika kushuka na kutembea kwa miguu na wengine walilazimika kulipa fedha ili kuvushwa,” amesema Mbaraka.
Mkazi wa Butimba, Deus Kabisha amesema hali hiyo imeongeza ugumu wa maisha kwa wananchi kwa sababu hata wafanyabiashara wadogo wanapata shida kusafirisha bidhaa zao, huku akieleza kuwa, baadhi ya madereva hulazimika kuegesha magari katika maeneo yasiyo salama.
Hali ilivyo mkoani Iringa
Mkoani Iringa, Wilaya ya Kilolo kumetajwa kuathirika na mafuriko yaliyosababisha uharibifu wa miundombinu katika baadhi ya maeneo, hususan katika kata za Nyanzwa na Mtandika ambako daraja limesombwa na maji na kukata mawasiliano kati ya maeneo hayo.
Mkazi wa Nyanzwa, Kasian Mbidule amesema daraja hilo lilikuwa kiunganishi muhimu kwa wananchi katika kupata huduma mbalimbali za kijamii.
Amesema mvua hizo pia zimesababisha uharibifu wa barabara ya Iringa–Pawaga eneo la Hoho na kufanya usafiri kuwa mgumu kwa wananchi wanaotumia njia hiyo.
Mkazi wa Kata ya Mkimbizi amesema mvua hizo zimeongeza changamoto kwa wananchi wanaotegemea barabara hiyo, huku akihofia wanafunzi kukosa vipindi kutokana na ugumu wa usafiri.
Katika Mkoa wa Manyara, zaidi ya ekari 10,000 za mazao zimeharibiwa na mafuriko wilayani Simanjiro, hususan katika Kata ya Naisinyai baada ya mashamba kusombwa na maji.
Tukio hilo lilitokea Machi 9, 2026 huku diwani wa kata hiyo, Taiko Laizer akisema mahindi na maharagwe yamesombwa na maji na kusababisha hasara kubwa kwa wakulima.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Fakii Lulandala alipotembelea eneo hilo amewataka wananchi wanaoishi mabondeni katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko kuhama ili kuepuka madhara zaidi.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Changarawe kata ya Masanze wilaya ya Kilosa wakiyahama makazi yao baada ya mto Miyombo kujaa na kumwaga maji kusababisha mafuriko kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha wilayani humo. Picha Hamida Shariff
Amesema Serikali haina bajeti ya kutoa mbegu kama walivyoomba baadhi ya wakulima waliopoteza mazao yao kutokana na mafuriko hayo.
Imeandikwa na Habel Chidawali (Dom), Janeth Joseph (Moshi), Christina Thobias (Iringa), Jesse Mikofu (Zanzibar) na Joseph Lyimo (Manyara),Saada Amir (Mwanza), Hamida Shariff na Juma Mtanda Morogoro.