TGNP YASISITIZA USAWA WA KIJINSIA KUFIKIA DIRA YA MAENDELEO 2050

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Clara Kalanga Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 115 ya Siku ya Wanawake Duniani.

*****

Na Mwandishi Wetu Dar es salaam.

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umesisitiza umuhimu wa kuhakikisha wanawake wanapata haki na usawa ili kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050, ukieleza kuwa maendeleo ya taifa hayawezi kufikiwa ikiwa nusu ya nguvu kazi ya nchi itaachwa nyuma.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 115 ya Siku ya Wanawake Duniani, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Clara Kalanga, alisema taifa linaanza safari mpya ya maendeleo baada ya uzinduzi wa Dira ya 2050 Julai 2025, hivyo ni lazima kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi na uongozi.

Kalanga alisema kauli mbiu ya kitaifa ya mwaka huu “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi Kufikia Dira 2050” inasisitiza umuhimu wa ushiriki sawa wa wanawake katika kujenga taifa lenye uchumi shindani na jumuishi.

Aliongeza kuwa kimataifa maadhimisho hayo yanaambatana na kampeni ya “ToaIliUpate (Give to Gain)”, inayohamasisha jamii kutoa rasilimali, maarifa, muda na fursa kwa wanawake ili kuimarisha usawa wa kijinsia na maendeleo ya pamoja.

Alisema TGNP kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa shughuli kadhaa katika mwezi wa Machi, zikiwemo maadhimisho katika kata zaidi ya 90 kutoka mikoa 13, kongamano la vijana Machi 17 pamoja na maadhimisho ya kimataifa yatakayofanyika Machi 25 hadi 27 yakishirikisha washiriki kutoka India, Haiti, Ethiopia, Bangladesh, Canada na Tanzania.

Kalanga alieleza kuwa pamoja na jitihada hizo, bado kuna changamoto kubwa za pengo la kijinsia duniani, akitaja takwimu za UN Women zinazoonesha wanawake wanalipwa ujira mdogo kwa takribani asilimia 23 ikilinganishwa na wanaume, huku zaidi ya wanawake bilioni 2.7 wakikosa uhuru wa kuchagua kazi sawa na wanaume katika baadhi ya maeneo.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Clara Kalanga Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 115 ya Siku ya Wanawake Duniani.

Alisema takwimu pia zinaonyesha wanawake wengi bado wanabeba mzigo mkubwa wa kazi za nyumbani zisizolipwa, hali inayowapunguzia fursa za kiuchumi na ushiriki katika nafasi za uongozi.

Kwa upande wa uwakilishi wa kisiasa, Kalanga alisema duniani wanawake wanashikilia takribani asilimia 27 ya viti vya bunge, huku Tanzania ikiwa imefikia asilimia 39.5 kutoka asilimia 37.4 mwaka 2020, hatua aliyosema ni chanya lakini bado kunahitajika juhudi zaidi kufikia uwiano wa 50 kwa 50.

Awali akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP, Dada Gemma Akilimali, alisema maadhimisho ya mwaka huu ni zaidi ya sherehe bali ni wito wa kuchukua hatua za kuvunja mifumo kandamizi na sheria za kibaguzi zinazozuia wanawake na wasichana kupata haki sawa katika jamii.

Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP, Dada Gemma Akilimali.

Cajentan Tumaini mwansheria kutoka Dawati la Familia, kutoka kituo Cha Sheria na Haki za binadamu ( LHRC).