MAKAMU WA RAIS DKT.NCHIMBI AWASIHI VIONGOZI WA DINI. NA WATANZANIA KUIOMBEA NCHI,VIONGOZI WA SERIKALI NA VYAMA VYA SIASA

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amewasihi Viongozi wa dini na Watanzania kwa ujumla kutumia mwezi wa toba wa Ramadhani na Kwaresma kuiombea Nchi, Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa ili kujenga nchi moja yenye upendo na mshikamano.

Makamu wa Rais, amesema hayo mara baada ya kushiriki Iftari aliyoiandaa kwaajili ya wananchi mbalimbali wa Mkoa wa Dodoma pamoja na Viongozi wa Serikali, Taasisi za Dini na Chama Cha Mapinduzi, iliyofanyika Mkoani Dodoma.

Amesema jambo kubwa ni kuhakikisha hamasa ya mapenzi ya nchi inakuwepo kwa kila mmoja na chemchem ya mapenzi kwa nchi iwepo katika roho ya kila mtanzania ili kuishi kwa kupendana na kushirikiana chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 Pia, Makamu wa Rais amesema katika mambo ya maana yanayoweza kufanyakika katika mwezi wa toba ni pamoja na kumuahidi Mwenyezi Mungu kwamba kila mtanzania atafanya jitihada ya kuunganisha watanzania kujenga nchi kuwa nchi moja yenye upendo.

Iftar hiyo imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandishi Hamad Masauni, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro, Waziri wa Madini Anthony Mavunde, Kamati ya Maridhiano, Viongozi mbalimbali wa Dini, Wabunge wa Mkoa wa Dodoma, Wakuu wa Wilaya pamoja na wananchi.