RAIS SAMIA NA AFISA MTENDAJI MKUU ABF SUGAR KUENDELEZA UWEKEZAJI SEKTA YA SUKARI

:::::::::

Na Mwandishi wa OMH

Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania, jana Machi 11, 2026, alimkaribisha Paul Kenward, Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya ABF Sugar, aliyefika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma kwa ziara ya heshima.

Katika ziara hiyo, Bw. Kenward aliambatana na viongozi wengine waandamizi wa kampuni hiyo akiwemo Balozi. Ami Mpungwe, Mwenyekiti wa Bodi ya Kilombero Sugar Company Limited; Guy Williams, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo; pamoja na Derick Stanley, Mkurugenzi wa Mahusiano ya Kampuni. 

Ikumbukwe kuwa Kilombero Sugar Company Limited inamilikiwa kwa ubia kati ya ABF Sugar ambayo inashikilia asilimia 75 ya hisa, na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH), inayomiliki asilimia 25 zilizobaki.

Mazungumzo kati ya Rais na ujumbe huo yalijikita katika kukuza zaidi sekta ya sukari nchini, uwekezaji unaoendelea na fursa za kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuendeleza ajenda za maendeleo ya taifa. 

Katika tukio hilo pia alikuwepo Bw. Nehemiah Mchechu, Msajili wa Hazina, pamoja na baadhi ya wataalamu kutoka OMH.

Kundi la ABF Sugar ni sehemu ya Associated British Foods (ABF), iliyoorodheshwa katika Soko la Hisa la London, Uingereza.

Kundi hilo lina mauzo ya takribani pauni bilioni 3 kwa mwaka na linaendesha viwanda 21 katika nchi tisa duniani, likiajiri takribani wafanyakazi 35,000.

Katika mazungumzo hayo, Bw. Kenward alimweleza Rais Samia kuwa kampuni hiyo tayari imewekeza zaidi ya sh900 bilioni katika sekta ya sukari nchini Tanzania na inaendelea kupanua uwekezaji wake, ikiwemo katika miundombinu ya umwagiliaji, uzalishaji wa nishati na utengenezaji wa ethanoli.

Alieleza kuwa mradi wa kiwanda kipya cha sukari umekamilika kwa kiasi kikubwa na unatarajiwa kuanza uzalishaji wa kibiashara mwezi Juni mwaka huu baada ya majaribio ya uzalishaji kukamilika. 

Mradi huo unatarajiwa kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa uzalishaji wa sukari nchini na kusaidia Tanzania kufikia lengo la kujitosheleza kwa sukari.

Kupitia upanuzi huo, uzalishaji wa sukari unatarajiwa kuongezeka kutoka takribani tani 126,000 hadi kufikia takribani tani 271,000 kwa mwaka. 

Aidha, idadi ya wakulima wadogo wanaoshiriki katika mnyororo wa thamani wa zao la miwa inatarajiwa kuongezeka kutoka wakulima 8,000 hadi kufikia takribani 16,000, hatua itakayoongeza kipato cha wakulima na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika jamii za vijijini.

Mbali na hilo, mradi huo pia utachangia upatikanaji wa nishati nchini kwa kuzalisha megawati 10 za umeme zitakazoingizwa katika gridi ya taifa, huku upanuzi wa uzalishaji wa ethanoli ukitarajiwa kupunguza uagizaji kutoka nje na kuimarisha mnyororo wa thamani wa viwanda nchini.

Kwa upande wake, Rais Samia alikaribisha uwekezaji unaoendelea wa ABF Sugar na kusisitiza dhamira ya Serikali kuendelea kuunga mkono uzalishaji wa ndani pamoja na kuimarisha sekta ya sukari nchini. 

Alibainisha kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha uwepo wa mazingira thabiti na rafiki ya uwekezaji yatakayowezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa taifa.

“Ushirikiano kati ya Serikali na wawekezaji ni muhimu katika kufanikisha vipaumbele vya maendeleo ya taifa, ikiwemo kukuza viwanda, kuongeza ajira, kuongeza thamani ya rasilimali za ndani na kuboresha maisha ya wananchi, hususan katika maeneo ya vijijini,” alisisitiza Mhe. Rais.