Suala la ukosefu wa ajira rasmi limekuwa likiumiza kichwa wengi, kuanzia kwa watu binafsi hata Serikali, lakini sasa Kwanzahub imekuja na suluhu ambalo hata kama sio la kumaliza tatizo lakini walau kupunguza na kuonyeshwa njia ya kutatua tatizo hilo.
Suluhu hiyo inahusisha kutoa jukwaa la vijana kuonyesha mawazo yao ya kibunifu, kuyelea, kuyauza lakini ni sehemu ya kijana hususani muhitimu kuweza kujifunza na kupata kipato cha ziadi wakati akisubiri ajira rasmi.
Mwanzilishi Kwanzahub Mihayo Wilmore anasema kuanzishwa kwa jukwaa hilo kunatokana na uzoefu wa maisha yake halisi ambao unaonyesha kuwa mtu hawezi kujitengeneza ila ni lazima ashikwe mkono kufikia hatua Fulani.
“Hakuna mtu anaweza kujiinua na kufikia mafanikio fulani bila kushikwa mkono na watu, binafsi nimesaidiwa na watu wengi hadi kufikia hapa ndiyo maana najua umuhimu wa kumshika mkono kijana hususani mwenye mawazo ya kibunifu,” amesema Wilmore ambaye ni mtaalamu wa mifumo ya kompyuta.
Anasema maono yake ni Kwanzahub ambayo inamilikiwa na kampuni ya Twigaalpha kuwa chimbuko la ubunifu nchini kwa kuweka mazingira yanayovutia hilo lakini zaidi kuibua mijadala ya kisayansi na kibunifu kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
“Nchini kwetu tumezoea kuwa na mijadala ya kisiasa zaidi lakini inawezekana kuwa na mijadala ya kisayansi, kihandisi na ubunifu wa kidijitali nchini. Tunataka kutengeneza chipukizi wa fikra muhimu,” anasema Wilmore.
Anasema Kwanzahub inakaribishwa kila mwenye wazo la tofauti kutumia jukwaa lao kulikuza akisema kuna vijana wengi wana mawazo lakini hawajui namna ya kuyaendeleza na wapi watapata usaidizi wa kutimiza ndoto zao.
Anasema miongoni mwa mambo ambayo yatafanywa kwa kituo hicho ni kufundisha juu ya usimamizi na uongozi, kuliweka wazo katika viwango vya juu vinavyovutia uwekezaji lakini pia kuuwekea ulinzi ubunifu husika.
Kuhusu upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya kukuza ubunifu na kutimiza ndoto za wabunifu Wilmore anasema wanategemea kuwa na ushirika na taasisi za ndani na nje ya nchi ili kusaidia ukuaji wa mwazao yanayotolewa na wabunifu wanaotumia jukwaa hilo.
“Sisi wenyewe tuna biashara zetu kupitia Twigalpha na nyingine, tutatumia faida kutoka kwenye biashara zetu kuwekeza kwenye mawazo hayo, uzuri ofisi ni mali yetu hivyo tuna anwani ya kudumu, tunatarajia kuwa na washirika na wahisani kwa ajili ya kupata fedha za kuendesha jukwaa hili,” anasema Wilmore.
Anasema mbali na vyanzo hivyo pia kuna watu wana mawazo yao na mitaji wanayo ila hawajui namna ya kuyafanikisha hao wakija watalipia gharama za utaalamu na ofisi ambazo zitarudi kufadhili wale wasionacho.
“Kuna wengine watalipia ada ya uanachama kwa ajili ya jukwaa kuwa huduma fulani ikiwemo kutoa mafunzo au ujuzi kwa wafanyakazi wao kwa ajili kuboresha eneo Fulani la kiutendaji,” anasema Wilmore.
Mbali na jukwaa la kukuza ubunifu Wilmore anasema KwanzaHub inatoa fursa ya watu kufanya kazi na kulipwa katika masuala ambayo wanahitaji utaalamu wake akisema si lazima kufuta ratiba ya kazi iliyozoeleka badala yake mtu anaweza kufanya kazi kwa muda wake wa ziada.
“Huu ni utaratibu wa kawaida katika mataifa yaliyoendelea watu wanafanya kazi zaidi ya mbili na wengine wanafanya kazi huku wakiwa wanasoma lakini hapa kwetu si jambo la kawaida sana. Sisi tumefanya ofisi yetu kuwa wazi saa 24 ikiwa na mazingira yote muhimu kwa mtu kufanya kazi kwa muda anaona unafaa kwake,” anasema.
Anasema anafanya hivyo kwakuwa watu wanakuwa na muda tofauti lakini pia kila mtu ana muda wake wa utulivu, wapo wa mchana, asubuhi na wengine usiku na muhimu ni kufanya kazi zenye tija muda wa kukaa ofisini si muhimu sana.
Jambo lingine wanalolifanya na kujenga uwezo kwa vijana ambapo sasa kupitia mradi wao wa Twigalpha Thinkathon wanachukua vijana kati ya 25-30 na kuwapa mafunzo kwa kipindi cha miezi sita lakini baada ya miezi mitatu mtu anaweza kuchagua kuendelea au kuacha.
“Sasa tunayo awamu ya kwanza ina vijana 12 na haina muda maalumu wa kudahili, tunatamani tungekuwa nao wengi zaidi lakini tunatarajia tutaendelea kupanua fursa hii kwa wengi zaidi,” anasema Wilmore.
Anasema Thinkathon ni fursa kwa wahitimu ambao wamehitimu miaka ya hivi karibu na wanatuta kujijenga kitaaluma, kupata kipato lakini pia kutengeneza wasifu kabla ya kuingia katika soko rasmi la ajira.