Geita. Jeshi la Magereza wilayani Chato mkoani Geita limeanza utekelezaji wa mkakati wa kisayansi wa kuwajengea wafungwa na mahabusu umahiri wa kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK).
Lengo la mkakati huo ni kuwasaidia kuondokana na ujinga na kuwawezesha kujitegemea wanaporejea katika jamii baada ya kumaliza vifungo vyao.
Programu hiyo hadi sasa ina zaidi ya miezi miwili tangu kuanzishwa kwake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Machi 11, 2026 na Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Magereza Wilaya ya Chato, Antony Mashauri, wafungwa na mahabusu 32 wananufaika na mpango huo kwa kupata muda wa kujifunza kila asubuhi kabla ya kuanza shughuli zao za kila siku.
Mashauri amesema kwa sasa Jeshi la Magereza halijikiti tu katika kukamata, kuhifadhi na kulinda wafungwa, bali pia katika utoaji wa huduma za urekebishaji kwa kuwajengea stadi mbalimbali za maisha, zikiwemo kilimo, uvuvi na ufugaji.
Amesema katika kufanikisha mpango huo, Gereza la Chato liliwasiliana na Halmashauri ya Wilaya ya Chato kuomba kupatiwa mwalimu wa kusaidia ufundishaji.
Mkuu wa Gereza la Wilaya ya Chato, Antony Mashauri, akizungumza katika hafla ya kupokea zawadi kutoka mtandao wa Polisi wanawake kwaajili ya wafungwa na mahabusu walio katika Gereza hilo.
Kupitia ushirikiano huo, mwalimu huyo hushirikiana na askari wa gereza hilo katika kufundisha, licha ya kuwa na majukumu ya kufundisha katika shule nyingine.
“Bada ya kuanzisha program hiyo, tuliwasiliana na uongozi wa halmashauri, tukamwandikia barua ya mkurugenzi kumwomba mwalimu, ametupatia mwalimu mmoja wa kiume ambaye anashirikiana na mwinmgine ambaye ni askari magereza.
“Darasa hilo linaendelea vizuri na mpaka sasa wafungwa hao wana madaftari, wana kalamu, wanafundishwa uumbaji wa herufi, kuhesabu, tunaamini kwamba baada ya miezi mitatu mpaka sita, tutakuwa na wafungwa ambao wamekuja hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu, wanatoka baada ya kifungo au wakishinda kesi yake wanatoka wakijua kusoma, kuandika na kuhesabu,” amesema.
Mashauri ameeleza hayo wakati wa tukio la kupokea bidhaa mbalimbali zilizotolewa na mtandao wa Polisi wanawake Mkoa wa Geita kwa wafungwa na mahabusu, walipokuwa wakihitimisha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Kamishina Msaidizi wa Polisi mkoani Geita, Adam Maro amesema mtandao wa Polisi Wanawake umeamua kuwapelekea zawadi hizo wafungwa na mahabusu, kama sehemu ya kudhihirisha upendo wao na kuwahimiza katika masomo, kwani gereza ni pia eneo la kujifunza na kukuza stadi za maisha.
“Wameletwa hapa ili kurekebishwa, sio kwamba tumewatupa, hawa ni watoto wetu na ni ndugu zetu, tumeona kama Jeshi la Polisi, suala hili linaweza kuweka alama katika mpango mzima wa kuzuia, kubaini na kutanzua kero za uhalifu,” amesema.
Ameongeza kuwa zawadi hizo zitaifanya mioyo ya wafungwa na mahabusu kubadilika kitabia kwa kuthamini jinsi askari hao walivyojitolea kwa upendo.
“Naamini kabisa mioyo yao itabadilika na watakuwa na mchango wa baadaye, na yale mafunzo waliyoyapokea kutoka hapa, watayapeleka kwenye familia zao na hatutakuwa na uhalifu katika taifa hili, hata Jeshi la Polisi litakuwa la uzalishaji badala ya jeshi la kukamata kamata wahalifu,” amesema.
