Dodoma. Tume iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kutathmini shughuli ya uhamaji wa hiari wa wananchi kutoka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, imetaja sababu tano za kukwama kwa shughuli hiyo.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mussa Iyombe amebainisha hayo leo Alhamisi Machi 12, 2026 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya Tume yake mbele ya Rais Samia.
Iyombe ametaja sababu hizo kuwa ni kutoshirikishwa kwa wananchi, upungufu wa sheria na kanuni, ujenzi wa nyumba moja kwa familia zenye wake zaidi ya mmoja, motisha kwa waliohama kupungua na mpango huo kuendeshwa kwa ushawishi badala ya utashi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa kwenye hafla ya kupokea Taarifa za Tume ya Rais ya Kutathmini Mgogoro wa Ardhi katika Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na Tume ya Rais ya Kutathmini Zoezi la Uhamaji wa Hiari wa Wakazi wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma leo Machi 12, 2026.
“Mheshimiwa Rais, shughuli hii halikufanikiwa, zimehama kaya 1,678 kati ya kaya 23,000 zinazoishi Ngorongoro, na sasa kuna zaidi ya Sh212.35 bilioni ambazo ziko tayari kujenga nyumba kwa watakaohama kwa hiari,” amesema Iyombe.
Mwenyekiti huyo amesema hadi sasa kuna nyumba 1,559 zilizojengwa Msomela mkoani Tanga ambazo hazijapata wakaaji, sababu ikielezwa kuwa wenye wake zaidi ya mmoja wanapata ugumu kuhusu nyumba moja ataweza kumpa mke yupi.
Tume hiyo iliyoundwa Desemba 2024, imekabidhi taarifa yao yenye kurasa zaidi ya 300, na imeomba pia Serikali kusitisha mara moja kuwajengea nyumba wakazi hao, badala yake iwape fedha ili wajenge nyumba kwa kufuata mila na tamaduni zao.
Viongozi mbalimbali na Mabalozi wa Nchi mbalimbali wakiwa kwenye hafla ya kupokea Taarifa za Tume ya Rais ya Kutathmini Mgogoro wa Ardhi katika Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na Tume ya Rais ya Kutathmini Zoezi la Uhamaji wa Hiari wa Wakazi wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, leo Machi 12, 2026.
Pendekezo lingine lililotolewa na Tume hiyo ni kutaka kiundwe chombo maalumu cha kuratibu uhamaji wa hiari badala ya mfumo unaotumika sasa.
Kuhusu sheria, amesema imekuwa na upungufu kwani inatambua kabila moja la Wamasai wakati kuna makabila mengine, hivyo kuna ubaguzi.
Vilevile, Tume imetaja malalamiko kwa waliobaki ikiwemo kukosa huduma za msingi wakati waliohama kilio chao ni mazingira waliyoyakuta na malalamiko mengine ya wenyeji ni kuporwa ardhi yao na kupewa wageni.
Hata hivyo, ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika uhamaji huo ikiwemo wananchi kuwa na makazi bora na huduma za kijamii ambazo zimeboreshwa huku wananchi wakiendelea na shughuli za kilimo.