Unguja. Wananchi 422,908 wamenufaika na kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, inayojulikana kama Samila Legal Aids, wakiwemo wanawake 209,185 na wanaume 213,723.
Pia, kupitia kampeni hiyo, migogoro 749 imepokelewa ikiwemo ya ardhi, mirathi, ndoa, ajira, udhalilishaji, ukatili wa kijinsia na matunzo ya watoto, huku migogoro 259 ikitatuliwa papo kwa hapo.
Kauli hiyo imetolewa leo, Alhamisi, Machi 12, 2026, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Haroun Ali Suleiman, wakati akizungumza na Mwananchi.
“Kampeni hii imenufaisha wananchi wa Zanzibar kwa kufikiwa karibu na huduma za msaada wa kisheria ambapo mikoa mitano na Wilaya 11 za Unguja na Pemba zilifikiwa,” amesema.
Vilevile, amesema Wizara hiyo, kwa kushirikiana na wahusika wengine, imetoa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi 680,184, wakiwemo wanaume 312,954 na wanawake 367,230.
Aidha, Haroun Ali Suleiman amesema Serikali imetoa msaada katika taasisi 12 zinazoshughulika na utoaji wa huduma, ikiwemo bajaji saba, kompyuta, printa na vishikwambi, ili kuwasaidia watoa huduma kuwa karibu na wananchi.
“Tunaendelea kuongeza juhudi kwa kujenga nguzo ndani ya misingi tuliyoiweka kwani tumeanza kufanya tathmini ya mafanikio na changamoto za taasisi zinazoshirikiana na wizara katika utoaji msaada wa kisheria,” amesema.
Amesema, tathmini hiyo itatoa mwelekeo bora zaidi katika juhudi na mikakati ya utoaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi kwa kipindi cha miaka mitano inayofuata.
Wizara hiyo, kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu imefanya mapitio mafupi ya Sheria 158 ili kubaini mlingano na migongano ya sheria za Zanzibar na kutoa mapendekezo ya kurekebisha, kufuta au kuanzisha mpya.
Wizara hiyo, imezindua mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa mashauri ili kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wakati pamoja na kutoa mafunzo ya mfumo huo kwa majaji, mahakimu, makadhi, makarani na wadau wa sekta ya haki.
Amesema, kwa upande wa uendeshaji kesi, katika kipindi cha miaka mitano waliendesha kesi 7,352 katika Mahakama mbalimbali za Unguja na Pemba.
Amefafanua kuwa, takwimu zinaonesha kesi zinapungua kwani mwaka 2021/22 zimepungua kwa asilimia 1.7, mwaka 2022/23 kesi zimepungua kwa asilimia 30.7 kutoka 2,255 hadi 1,563 na kwa mwaka 2023/24 kesi zimepungua kwa asilimia 20.7. kutoka 1,563 hadi 1,239).
Ameeleza, hali hiyo inaonyesha kuwa uhalifu wa kijinai unapungua ikilinganishwa na miaka ya nyuma na hiyo inatokana na mikakati ya Serikali kwa taasisi zinazosimamia masuala ya kijinai kuimarika kiutendaji, miundombinu, vitendea kazi na kuongezeka kwa weledi wa watendaji.
Naye, Salma Awadh amesema awali walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya ardhi inayosababishwa na utalii katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, lakini hilo limetatuliwa kupitia kampeni hiyo.
Amesema, kampeni hiyo imekuwa ni jawabu kwa wengi waliokuwa na changamoto hizo na wanashukuru kupata haki zao.
Kombo Pandu amesema kampeni hiyo imekuwa mwarobaini kwa wote wenye matatizo ya kisheria.
