WOTE katika kijiwe chetu leo tumekubaliana kuwa Rushine De Reuck ni usajili mzuri sana ambao Simba wameufanya msimu huu kutokana na mchango mkubwa anaoutoa katika safu ya ulinzi ya timu hiyo.
Ni kiongozi mzuri wa safu ya ulinzi, ana hesabu sahihi anapokabiliana na washambuliaji wa timu pinzani, anamudu kuokoa mashambulizi ya chini na juu na na uwezo wa kuichezesha timu kuanzia nyuma.
Wakati aliposajiliwa wapo waliodhani Simba imepigwa kwamba Mamelodi Sundowns haiwezi kumuacha mchezaji mzuri lakini jamaa amejibu kwa vitendo uwanjani na sasa wengi tunampigia saluti.
Kiwango bora ambacho amekuwa akikionyesha, kilituaminisha baadhi yetu hapa kijiweni kwamba Rushine anaweza kurudishwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ katika kipindi hiki ambacho inajiandaa kushiriki Fainali za Kombe la Dunia. Hatukuwa na imani kwamba angeenda Kombe la Dunia lakini basi hata kuwemo tu katika kikosi cha awali kwa ajili ya mechi mbili za kimataifa dhidi ya Panama tulidhani anaweza kuitwa.
Hata hivyo haijawa kama tulivyotegemea. Kocha Hugo Broos wa Bafana Bafana ameamua kutomuita De Reuck katika kikosi chake cha awali alichokitangaza juzi, jambo linalotoa ishara ya wazi kwamba beki huyo ni ngumu kuwemo katika kikosi cha Kombe la Dunia.
Inawezekana De Reuck anaangushwa na kiwango cha ushindani kilichopo katika ligi kulinganisha na zile za wachezaji wa nafasi yake walioitwa katika kikosi cha Afrika Kusini. Ni jambo lililo wazi kwamba hapa nchini kuna mechi chache sana za mashindano ya ndani ambazo De Reuck anakutana nazo hivyo pengine Broos na benchi lake la ufundi wanakuwa hawajajiridhisha vya kutosha kama anaweza kuwabeba katika Kombe la Dunia.
Mwisho wa siku tunaitimisha tu kwamba wenzetu wana machaguo mengi ya wachezaji katika timu zao za taifa. Ingekuwa ni hapa Tanzania, De Reuck asingekosa nafasi Taifa Stars.