AKILI ZA KIJIWENI: Pedro utafakari ushauri wetu

SISI hapa kijiweni kazi yetu ni kutoa ushauri tu halafu mwisho wa siku tunamuachia muhusika mwenyewe achague kuufanyia kazi au kuachana nayo.

Kwa sababu tuna uzoefu kidogo na soka la Tanzania, kuna dalili fulani zikianza kujitokeza tunaanza kupata picha ya kile kinachoweza kutokea mbele ya safari kama kitakuwa na neema au nuksi.

Hilo ndilo linatufanya leo tumcheki jamaa yetu Pedro Goncalves ambaye ni kocha mkuu wa Yanga na kumpa tahadhari kuwa anapaswa kuongeza umakini katika majukumu yake ili yasije kumkuta siku za usoni.

Maoni ya baadhi ya wanachama na mashabiki wa Yanga kwa kile anachokifanya ndani ya timu hiyo, yameanza kumkataa na anapaswa kurekebisha kwa haraka hali ya mambo vinginevyo AFCON 2027 inaweza kumkuta akiwa sio Kocha Mkuu wa Yanga.

Kuna Wanayanga ambao hawafurahishwi na namna kocha huyo anavyopenda kujilinda sana katika mechi kubwa badala ya kuifungua timu na kushambulia kama ambavyo walizoeshwa na makocha wengi waliopita miaka ya hivi karibuni.

Wenyewe wanaiamini timu na wachezaji wao. Wanaona hawastahili kushika roho kwa muda mrefu kwa sababu wanashambuliwa wakati walishazoea kuwa wao ndio wanafanya wapinzani waishi kwa hofu kwa muda mrefu wa mchezo. Kingine ni kwamba yule Okello wao wenyewe wanaamini anastahili kuchezeshwa pale nyuma ya mshambuliaji kwa maana ya namba 10. Eti kule pembeni unakompanga wanaona unamnyima fursa ya kuonyesha uwezo wake.

Sasa bwana Pedro urekebishe mambo haraka kabla hao jamaa hawajakugeuzia kibao. Unaweza kujiona uko salama kwa sababu timu inapata matokeo mazuri lakini hao Yanga hawatabiriki na wanaweza kukuchomoa pamoja na hayo matokeo yako. Mwenzako Zlatko Krmpotic aliwahi kutimuliwa huku akiwa ameshinda mechi tatu mfululizo bila kuruhusu bao.