Costech yaja na ‘Tanzania Ventures Lab’ kuwezesha bunifu, biashara changa

Dar es Salaam. Katika mwendelezo wa kuhakikisha bunifu na biashara changa za vijana zinaendelezwa, Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) kwa kushirikiana na Sahara Ventures imekuja na programu ya kitaifa inayolenga kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini Tanzania.

Pia kuharakisha ukuaji wa biashara changa haswa zinazofanywa na vijana ili waweze kukua zaidi.

Programu hiyo iliyopewa jina la ‘Tanzania Ventures Lab (TVL) itatekelezwa kupitia Kituo cha Teknolojia cha Dar Teknohama Business Incubators (DTBi) na Buni Innovation Hub, majukwaa ya kitaifa yaliyo chini ya Costech yanayohusika na kukuza ubunifu, teknolojia na ujasiriamali.

Akizungumza katika hafla fupi ya uzinduzi iliyofanyika leo Alhamisi, Machi 12, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Costech, Dk Amos Nungu amesema programu hiyo ya miaka minne inatarajiwa kunufaisha bunifu pamoja na biashara changa 1,000 za vijana katika sekta sita za kimkakati.

Nungu amesema kwa kila mwaka wanatarajia kuzishika mkono na kuziwezesha bunifu takribani 250 kutoka kwa vijana wanufaika.

Amesisitiza kuwa lengo la programu hiyo ni kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini kwa kuunganisha wabunifu, watafiti, wawekezaji, sekta binafsi na taasisi za serikali katika mfumo mmoja wa kukuza na kuendeleza biashara changa.

“Tanzania Ventures Lab ni hatua muhimu katika kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini. Kwa kusaidia biashara changa zenye uwezo mkubwa na kuimarisha ushirikiano kati ya utafiti, sekta binafsi na uwekezaji, programu hii itasaidia kugeuza mawazo ya ubunifu kuwa biashara zinazochangia maendeleo ya uchumi wa Tanzania,” amesema Nungu.

Mkurugezi Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk Amos Nungu akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa ‘Tanzania Ventures Lab’ programu ya kitaifa inayolenga kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini Tanzania.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa Sahara Ventures, Jumanne Mtambalike amesema utekelezaji wa programu hiyo utajielekeza katika kuwezesha bunifu na biashara changa zilizopo ndani ya sekta sita za kimkakati.

Sekta hizo ni pamoja na nishati, utalii, madini, viwanda, teknolojia pamoja na kilimo na ufugaji.

Amesema kuwa sekta hizo zimechaguliwa kutokana na mchango wake katika ukuaji wa uchumi, ajira, maendeleo ya viwanda na ubunifu wa teknolojia.

Ameeleza kuwa programu hiyo itakapotekelezwa kikamilifu itasaidia kuongezeka kwa biashara zinazotokana na ubunifu na teknolojia.

“Pia itasaidia kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika shughuli za ujasiriamali pamoja na kuimarika kwa uwekezaji wa bunifu nchini,”amesema Mtambalike.

Naye Mtendaji Mkuu kutoka Kituo cha Teknolojia cha Dar Teknohama Business Incubators (DTBi), Patience Karua amewahimiza vijana wabunifu kuchangamkia fursa hiyo ambayo itawasaidia kupata mitaji pamoja na ujuzi zaidi utakaowawezesha kubiasharisha bunifu zao pamoja na kukuza biashara changa.