Makubaliano Musongati yafungua ukurasa mpya uchimbaji Nikeli Afrika Mashariki

Dar es Salaam. Kampuni ya Lifezone Metals inayomiliki Tembo Nickel, imesaini makubaliano ya miezi 14 na Serikali ya Burundi kuhusu maendeleo ya mgodi wa Nikeli wa Musongati.

Hatua hiyo inatajwa kuwa inaenda kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika sekta ya madini na miundombinu.

Akizungumza kuhusu makubaliano hayo yaliyosainiwa Machi 10, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Tembo Nickel, Benedict Busunzu amesema muda wa utekelezaji unaweza kuongezwa kulingana na maendeleo ya mradi.

Amesema makubaliano hayo yanaweka msingi wa maendeleo ya mgodi wa Musongati, yakizingatia pia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, inayolenga kukuza uchumi wa viwanda na kuongeza thamani ya rasilimali za madini.

Kwa mujibu wa Busunzu, mgodi wa Musongati una wastani wa asilimia 1.31 ya nikeli, asilimia 0.21 ya shaba na asilimia 0.09 ya kobalti, huku ukikadiriwa kuwa na zaidi ya tani milioni 150 za rasilimali hizo.

Makubaliano hayo yalitiwa saini na Mtendaji Mkuu wa Lifezone Metals, Chris Showalter na Waziri wa Madini, Nishati, Viwanda, Biashara na Utalii wa Burundi, Dk Hassan Kibeya.

Hafla ya utiaji saini ilifanyika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani mjini Washington, D.C. mbele ya Naibu Katibu Msaidizi wa Marekani anayeshughulikia Afrika ya Kati na Ushirikiano wa Biashara, Sarah Troutman.

Busunzu amesema hatua hiyo pia inaonyesha umuhimu wa mradi wa reli ya kisasa ya SGR ya Tanzania pamoja na sera za nchi za kuhamasisha uchakataji wa madini ndani ya nchi.

Ujenzi wa reli ya SGR kuelekea magharibi, nao unatajwa kuwa kiungo muhimu cha kuunganisha miradi ya madini na masoko ya kimataifa.

Awamu ya pili ya reli ya pamoja ya Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), inayofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa zaidi ya dola 696 milioni (Sh1.7 trilioni), inalenga kufungua uwezo wa uzalishaji wa nikeli katika mgodi wa Musongati.

Ujenzi wa kipande cha reli kinachounganisha Tanzania na Burundi ulianza Agosti 16, 2025.

Reli hiyo pia itahudumia mradi wa Tembo Nickel uliopo Kabanga kwa kusafirisha bidhaa zilizokamilika kutoka Kabanga na Kahama hadi Bandari ya Dar es Salaam.

 “Tembo Nickel inachangia kufanikisha uchumi wa dola 1 trilioni kupitia uchimbaji endelevu, uchakataji wa madini ndani ya nchi na maendeleo ya miundombinu ya usafirishaji,” amesema Busunzu.