Ziara ujumbe wa Congo yafungua matumaini ya soko la mahindi

Dar es Salaam. Wakulima wa Tanzania, sasa kupata uhakika wa soko la mahindi baada ya ujumbe wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi kukagua na kuridhishwa na ubora wa bidhaa hiyo.

Ujumbe huo wa watu tisa umetua nchini leo Alhamisi Machi 12, 2026 na kwenda moja kwa moja kwenye ghala la kuhifadhi mahindi la Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA), lililopo Keko wilayani Temeke kuangalia namna bidhaa hizo zinavyohifadhiwa.

Ujio wa ujumbe ni matokeo ya ziara iliyofanywa na Serikali ya Tanzania nchini Congo, ikiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweri ambapo walikwenda kuzungumza na Taifa hilo kuhusu ununuzi wa nafaka zilizopo nchini.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa NFRA, Dk Andrew Komba, hatua ya Tanzania kuuza mahindi Congo, itamuhakikishia mkulima soko la uhakika na kumuongeza tija katika kilimo cha zao hilo.

“Hili soko la Congo linakwenda kuongeza tija kwa wakulima wetu, tunajisikia faraja kwa hili. Ni wakati sasa kwa wakulima kuzalisha kwa wingi,” amesema Dk Komba.

Dk Komba amebainisha kuwa NFRA ina utoshelevu wa kutosha wa chakula na kinachofanyika hivi sasa ni kutafuta masoko ili kuuza ziada.

“Msingi mkubwa wa NFRA ni kuhifadhi chakula kwa ajili ya utoshelezi wa mahitaji ya ndani ya nchi panakuwa na shida. Sasa kiwango cha tani 150,000 za chakula zipo za kuhakikisha usalama wa ndani.”

“Tunachokiuza kile kilichoongezeka, ujumbe huu wa wageni umeangalia upatikanaji na ubora wa mahindi, lakini pia wameangalia namna ya kusafirisha kutoka Tanzania hadi Congo,” ameeleza Dk Komba.

Viongozi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) wakiwa ujumbe wa Rais wa Jamhuri ya Kongo waliokuja nchini kwa ajili ya kuangalia namna ya mahindi yanayohifadhiwa kabla ya kuanza taratibu za kuyanunua

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya NFRA, Balozi John Ulanga amesema Congo wana mahitaji makubwa ya nafaka hasa mahindi na katika ziara walioifanya nchini humo, waliahidi kuja Tanzania kuangalia hifadhi iliyopo na teknolojia inayotumiwa.

“Tuna furaha ziara yetu Congo imezaa matunda, tuna uhakika wa kuuza mahindi Congo. Hatua hii itatusaidia NRFA kuongeza uwezo wa kuhifadhi na kununua nafaka kutoka kwa wakulima na kuongeza uchumi wao,” amesema Balozi Ulanga.

Kwa mujibu wa Balozi Ulanga, Congo ni watumiaji wakubwa wa ugali na wana upungufu wa tani milioni tatu za unga kwa mwaka, sawa na tani milioni tano za mahindi.

Balozi Ulanga amesema Congo pia wanaongea na mataifa mengine kuhusu uhitaji wa mahindi, lakini wameanzia Tanzania.

Amefafanua kuwa, baada ya ujumbe huo kuonana na watendaji Wizara ya Kilimo, Serikali itatangaza kiwango cha mahindi kitakachouzwa katika mataifa hayo baada ya majadiliano.

Mmoja wa viongozi wa msafara huo, Tony Munongoll amesema “tuna furaha kuja Tanzania na wajumbe wenzangu, tupo hapa kwa mwaliko maalumu wa Serikali ya Tanzania, tumevutiwa namna ambavyo walivyopiga hatua katika uzalishaji na usambazaji wa mkubwa wa mahindi.”

“Tumeona namna walivyohifadhi mahindi yapo vizuri, kwa sasa tunaangalia mbele zaidi ili kuimarisha uhusiano kati yetu na Tanzania,” amesema Munongoll.