Dar es Salaam. Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa niaba ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza jumla ya nafasi 105 za ajira katika kada mbalimbali, ikiwakaribisha Watanzania wenye sifa kuomba nafasi hizo kabla ya Machi 24, 2026.
Tangazo hilo lililotolewa Machi 10, 2026 linaeleza kuwa nafasi hizo zinalenga kuongeza nguvu kazi yenye weledi na kuimarisha utendaji wa taasisi hiyo.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, waombaji watakaofanikiwa watapangiwa vituo vya kazi.
Vituo hivyo ni katika ofisi mbalimbali za benki hiyo ikiwemo makao makuu Dodoma, ofisi ndogo za Dar es Salaam na Zanzibar na matawi ya Arusha, Mbeya, Mtwara na Mwanza au katika Chuo cha BoT kilichopo Mwanza.
Nafasi zilizotangazwa zinahusisha kada za kitaalamu, kiutawala na kiufundi. Baadhi ya nafasi hizo ni Ofisa wa Benki Daraja la III (nafasi 16), Mhasibu III (nafasi 11), Bank Examiner III (nafasi 7), Mtaalamu wa Tehama III (nafasi 8) na Computer Analyst/Programmer III (nafasi 6).
Pia zipo nafasi za Mkaguzi wa Ndani (Systems Auditor) III (nafasi 4), Mtaalamu wa Sheria III (nafasi 2), Ofisa Usalama III (nafasi 2), Mtaalamu wa Manunuzi III (nafasi 2), Ofisa Mipango III (nafasi 1), Mtaalamu wa Fedha III (nafasi 1) na Mtaalamu wa Biashara III (nafasi 1).Kwa upande wa kada za uhandisi na ufundi, BoT imetangaza nafasi za Mhandisi Mitambo III (nafasi 1), Mhandisi wa Umeme III (nafasi 1), Fundi Umeme III (nafasi 1) na Electronics Technician III (nafasi 1).
Aidha, zipo nafasi za Muhudumu wa Mapokezi III (nafasi saba), muhudumu wa jikoni III (nafasi tano), Porter III (nafasi mbili), Katibu Muhtasi III (nafasi tatu) pamoja na Walinzi (Security Guard III) nafasi 19.
Kwa mujibu wa Sekretarieti ya Ajira, waombaji wa nafasi mbalimbali wanapaswa kuwa na sifa za kitaaluma kulingana na aina ya kazi husika, ikiwemo stashahada, shahada au vyeti vya ufundi kutoka taasisi zinazotambuliwa na Serikali.
Waombaji wa nafasi za Ofisa wa Benki, Mhasibu, Bank Examiner na Mtaalamu wa Fedha wanatakiwa kuwa na shahada katika fani za uhasibu, fedha, biashara au uchumi, huku baadhi ya nafasi zikihitaji usajili katika bodi au taasisi za kitaaluma.
Vyeti vya kitaaluma kama CPA, ACCA, CIMA, CFA au vyeti vya kitaalamu vya benki vitachukuliwa kuwa faida ya ziada kwa baadhi ya waombaji kulingana na mahitaji ya kazi husika.
Kwa upande wa nafasi za teknolojia ya habari kama Computer Analyst/Programmer na Mtaalamu wa Tehama, waombaji wanatakiwa kuwa na elimu ya shahada au stashahada katika sayansi ya kompyuta, teknolojia ya habari au fani zinazofanana.
Aidha, waombaji wote wanatakiwa kuwa raia wa Tanzania wenye umri usiozidi miaka 45 isipokuwa wale waliopo katika utumishi wa umma au wanaotuma maombi katika taasisi zenye masharti maalumu ya ajira.
Waombaji wanapaswa kuwasilisha nakala za vyeti vya elimu, vyeti vya kitaaluma, cheti cha kuzaliwa, wasifu binafsi (CV), picha ya pasipoti pamoja na majina ya wadhamini watatu wanaoweza kuthibitisha uadilifu na uwezo wao wa kufanya kazi.
Sekretarieti ya Ajira imeonya kuwa maombi yatakayowasilishwa nje ya mfumo rasmi wa Ajira Portal hayatapokelewa, na waombaji watakaowasilisha vyeti bandia au kutoa taarifa za uongo watachukuliwa hatua za kisheria.
Maombi yote yanapaswa kuwasilishwa kupitia mfumo wa Ajira wa Serikali mtandaoni (Ajira Portal) kabla ya Machi 24, 2026, huku waombaji watakaokidhi vigezo pekee wataitwa kwenye usaili.
