Masilingi awataka watendaji kuongeza uwazi kwenye miradi ya CSR

Geita. Mwenyekiti wa Tume ya Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini na Gesi, Balozi Wilson Masilingi, amewataka watendaji wa halmashauri nchini kuhakikisha kunakuwepo uwazi na ushirikishwaji wa wananchi katika uteuzi wa miradi inayotekelezwa kupitia fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR), kutoka kampuni za uchimbaji madini.

Masilingi amesema kukosekana kwa uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi hiyo kunaweza kusababisha malalamiko na hata migogoro katika jamii, hasa pale wananchi wanapohisi hawajanufaika ipasavyo na rasilimali za madini zinazopatikana katika maeneo yao.

“Huwezi kupeleka zahanati katika kijiji ambacho tayari kina zahanati. Kama wananchi wanahitaji ajira au uwezeshaji wa kiuchumi kwa vijana wao, ni muhimu kusikiliza mahitaji yao badala ya kuamua miradi bila kuwashirikisha,” amesema Masilingi.

Masilingi ametoa wito huo leo Machi 12, 2026, mkoani Geita katika ziara yake ya kwanza tangu ateuliwe kushika wadhifa huo na Rais Samia Suluhu Hassan.

Masilingi amesisitiza kuwa baadhi ya nchi za Afrika zimejikuta zikiingia katika machafuko kutokana na kukosekana kwa uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali zao, hali inayotoa mianya kwa migogoro na propaganda za kiuchumi kutoka nje ya bara hilo.

“Chuki na migawanyiko inayojitokeza katika baadhi ya nchi zinazoendelea mara nyingi hutokana na ukosefu wa uwazi na uwajibikaji. Hali hiyo huwafanya wananchi kuwa na mashaka kuhusu namna rasilimali zao zinavyosimamiwa,” amesema.

Katika ziara hiyo, Masilingi alitembelea mgodi wa dhahabu wa Geita Gold Mining Limited (GGML) na kupongeza uongozi wa mgodi huo kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia mpango wa CSR.

Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu unaojengwa kwa ufadhili wa mgodi huo chini ya usimamizi wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita.

Kwa mujibu wa taarifa za mgodi huo, GGML hutenga zaidi ya Sh9 bilioni kila mwaka kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya jamii katika halmashauri za mkoa huo.

Mbali na miradi ya CSR, katika mwaka wa fedha 2025/2026 mgodi huo unatarajia kulipa takribani Sh70 bilioni kama fidia kwa wananchi watakaopisha maeneo yao kupisha shughuli za uchimbaji.

Malipo hayo yanatarajiwa kumaliza kilio cha zaidi ya miaka 25 cha wakazi wa mitaa ya Nyakabale na Nyamalembo katika Manispaa ya Geita waliokuwa wakidai fidia.

Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Ofisa Mahusiano Mwandamizi wa GGML, Gilbert Mworia, amesema makadirio ya fidia hiyo yametokana na tathmini iliyochukua takribani miezi sita tangu ilipoanza rasmi Agosti 21, 2025.

“Kuanzia mwezi huu wa Machi 2026 wananchi wataanza kulipwa fidia. Kama kuna changamoto ndogo ndogo zinajitokeza, ni muhimu kuelewa kuwa hatua hii ni kubwa na linafanyika kwa kuzingatia sheria za nchi pamoja na taratibu za kampuni,” amesema Mworia.