Urasimu, tozo za kero kwenye taasisi za umma, mashirika kumulikwa

Dodoma. Serikali imetangaza mchakato wa kupitia upya mashirika na taasisi za umma zinazohusika na udhibiti na usimamizi wa shughuli za kibiashara.

Lengo la Serikali ni kupunguza urasimu unaosababishwa na kanuni na tozo zisizo za lazima, zinazokwamisha ukuaji wa biashara nchini.

Mpango huu pia unalenga kuondoa urasimu unaochangia kuchelewesha uwekezaji na kupunguza tija katika sekta ya biashara.

Aidha, Serikali inapanga kupunguza idadi ya taasisi za udhibiti na kubaki na mashirika machache yenye ufanisi, yatakayorahisisha ufanyaji wa biashara na kuvutia wawekezaji zaidi, huku ikihakikisha udhibiti muhimu unadumishwa.

Hatua hiyo ilielezwa na Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, Machi 11, 2026 jijini Dodoma wakati wa mkutano wa uhakiki wa rasimu ya Mpango wa Pili wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji.

Profesa Mkumbo alisema mapitio hayo yatarahisisha mazingira ya biashara, kuongeza uwekezaji na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Amesema hivi sasa baadhi ya biashara zinakutana na vikwazo vya urasimu kutokana na idadi kubwa ya taasisi za udhibiti pamoja na tozo nyingi wanazotozwa wafanyabiashara.

Kwa mujibu wa Waziri Kitila, mtu akitaka kuanzisha biashara ndogo mfano wa kizimba cha samaki anakutana na taasisi zaidi ya 27.

“Nilikuwa nazungumza na mheshimiwa Kadogosa, (Masanja, mbunge wa Bariadi Vijijini), akaniambia yeye alianzisha biashara hiyo alitumia zaidi ya Sh20 milioni kulipia tozo mbalimbali, na si mtaji wa biashara, kwa namna hii hatuwezi kukuza biashara,” amesema Profesa Mkumbo.

Amesema Wizara ya Mipango, kwa kushirikiana na Tamisemi, inaandaa mfumo wa kupima na kushindanisha mikoa pamoja na mamlaka za Serikali za mitaa, ili kubaini jinsi zinavyorahisisha biashara na kuvutia uwekezaji.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesema kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kunahitaji ushirikiano thabiti kati ya Serikali na sekta binafsi.

Amesema kila mwaka, vijana kati ya milioni 1.5 hadi milioni 2 uhitimu katika ngazi mbalimbali za elimu na kuingia kwenye soko la ajira, hali inayofanya sekta binafsi kuwa muhimu katika kuunda nafasi nyingi za ajira na kukuza uchumi.

 “Sasa tukiiacha sekta binafsi ikasinzia hatuwezi kufikia malengo yetu, lazima tuijenge, tuheshimu na kuikuza kwa sababu Serikali pekee haiwezi kutengeneza ajira kwa vijana wote wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka,” amesema Dk Mwigulu.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, ili kufikia uchumi wa kipato cha juu kama inavyolenga Dira ya 2050, kunategemewa uzalishaji wenye ushindani wa kimataifa, hususan katika sekta za viwanda, kilimo chenye tija, uchumi wa bluu na mageuzi ya kidijitali.

Waziri Mkuu aliwataka wakuu wa mikoa na wakurugenzi wa halmashauri kuwa na mtazamo chanya kwa sekta binafsi na kusaidia kukuza biashara badala ya kuwakandamiza wafanyabiashara.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Bahati Geuze aliyewasilisha maoni kwa niaba ya makatibu tawala wa mikoa, aliishauri Serikali kuendelea kulea na kukuza sekta binafsi kwa kuzipa kipaumbele kampuni na taasisi binafsi katika maendeleo ya uchumi.

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Dk Oscar Kikoyo aliishauri Serikali kuhakikisha sheria zinazotungwa zinaendana na malengo ya mpango wa kuboresha mazingira ya biashara pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.