Dar es Salaam. Bei ya hisa za kampuni ya habari ya Nation Media Group (NMG) imeongezeka kwa asilimia 28.3 ndani ya siku mbili kufuatia tangazo la Jumanne kuwa mfanyabiashara Rostam Aziz ananunua hisa nyingi katika kampuni hiyo.
Jana, bei ya hisa hizo katika soko la hisa la Nairobi (NSE) iliongezeka kwa asilimia 7.6 na kufikia kiwango cha juu zaidi ndani ya miaka miwili cha Shilingi za Kenya 17 kwa hisa, huku thamani ya kampuni sokoni ikifikia Shilingi za Kenya 3.24 bilioni. Ongezeko hilo limeongezea faida ya asilimia 19.2 iliyorekodiwa Jumatano, wakati hisa hizo zilipouzwa bila kikomo cha kawaida cha udhibiti wa asilimia 10 kutokana na tangazo muhimu lililotolewa baada ya soko kufungwa Jumanne.
Kabla ya taarifa ya muamala huo kutangazwa, hisa za NMG zilikuwa zikiuzwa kwa Sh13.25 kwa hisa moja na ndani ya siku hizi mbili wawekezaji wameuza na kununua jumla ya hisa 298,887 za kampuni hiyo, zenye thamani ya Shilingi za Kenya 4.84 milioni. NMG ina jumla ya hisa milioni 190.295 zilizoko sokoni.
Kupitia kampuni yake Taarifa Ltd Rostam alinunua asilimia 54.08 NMG kutoka Aga Khan Fund for Economic Development (AKFED) katika muamala unaotarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu hadi minne ijayo, baada ya kupata idhini za mamlaka za udhibiti.
AKFED ilikuwa inashikilia hisa hizo kupitia kampuni ya uwekezaji inayojulikana kama NPRT Holdings Africa Limited, ambayo sasa itahamishiwa kwa Taarifa Ltd.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Jumatano, Machi 11,2026 Rostam aliahidi kuingiza uwekezaji mpya katika moja ya kampuni kubwa ya vyombo vya habari barani Afrika, wakati ambapo kampuni hiyo inaongeza uwekezaji katika majukwaa ya kidijitali ili kuwafikia wasomaji na watazamaji wengi zaidi kulingana na mwenendo wa kimataifa wa matumizi ya vyombo vya habari.
Pia aliahidi kuendelea kulinda viwango vya uhariri vilivyotambulisha kampuni hiyo tangu ilipoanzishwa miaka 66 iliyopita na Aga Khan IV.
“Dhamira yetu ni kuongeza uwekezaji ili tuweze kuwa na faida zaidi. Ajira zaidi zitaanzishwa kadri tunavyoendelea mbele kwa sababu tunahitaji kubadilika na kuwahudumia Wakenya wote ili ushirikiano huu uwe na mafanikio,” alisema Rostam.
Aidha, alithibitisha kuwa anaingia katika kampuni hiyo kama mshirika wa kimkakati wa muda mrefu, jambo linalowapa wawekezaji katika soko la hisa uhakika wa kuendelea kuwepo kwa mbia mkuu mwenye uthabiti katika moja ya kampuni kongwe zilizoorodheshwa NSE.
NMG iliorodheshwa NSE mwaka 1973, miaka 15 baada ya kuanzishwa na Aga Khan IV kwa lengo la kuipatia Kenya vyombo vya habari huru na vinavyojitegemea ili kusaidia kukuza utawala wa kidemokrasia wakati wa uhuru. Kampuni hiyo ilianza na gazeti la Kiswahili Taifa Leo, kabla ya kupanua shughuli zake hadi kufikia zaidi ya chapa 30 za vyombo vya habari ndani ya Afrika Mashariki.
Hisa za NMG pia zimeorodheshwa katika soko la hisa la Uganda, Dar es Salaam na Rwanda.
Kampuni ya Taarifa imeahidi kuendelea kuiorodhesha NMG katika NSE pamoja na masoko mengine ambako hisa zake zimeorodheshwa pindi itakapokamilisha ununuzi huo. Kampuni hiyo haitatoa ofa ya kununua hisa zilizobaki zinazomilikiwa na wawekezaji wadogo.
Kupanda kwa bei ya hisa za NMG wiki hii pia kunaonyesha kuwa wawekezaji wana mtazamo chanya kuhusu ujio wa mbia mkuu mwenye uzoefu wa kuendesha kampuni ya vyombo vya habari.
Ikumbukwe kuwa Rostam alikuwa miongoni mwa waanzilishi na wanahisa wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (NMG) kati ya mwaka 2000 na 2006, ambayo inazalisha magazeti ya The Citizen, Mwananchi, na Mwanaspoti yaliyokuja kununuliwa na NMG mwaka 2006.
Baadaye alinunua kampuni ya New Habari (2006) Limited na alikuwa mwekezaji mkuu katika kampuni ya Africa Media Group kati ya mwaka 2005 na 2019, ambapo alikuwa ndiye mmiliki wa vituo vya televisheni na redio kama Channel Ten, DTV, CTN, Classic FM, na Magic FM.
Aidha, alikuwa miongoni mwa wanahisa waanzilishi wa Vodacom Tanzania mwaka 1999 kabla ya kuuza hisa zake mwaka 2019. Baadaye alishiriki katika muungano wa wawekezaji ulionunua kampuni ya tatu kwa ukubwa ya simu nchini Tanzania, Tigo Tanzania, ambayo sasa inajulikana kama Yas.
