Dar/Dodoma. Wakati tume zilizoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan zikibainisha sababu za kukwama kwa mpango wa kuwahamisha wakazi wa ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, Serikali imesema itaendelea na mpango huo lakini kwa mfumo mpya unaosisitiza hiari ya wananchi, ushirikishwaji mpana wa jamii na marekebisho ya kasoro zilizojitokeza awali.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Machi 12, 2026 katika Ikulu ya Chamwino wakati Rais Samia akipokea ripoti za tume mbili alizoziunda kuchunguza mzozo uliotokana na uhamaji wa wananchi kutoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro.
Tume ya kwanza iliyoongozwa na Dk Gerald Ndika ilichunguza matumizi ya ardhi katika Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, huku tume ya pili iliyoongozwa na Mussa Iyombe ikichunguza utekelezaji wa shughuli nzima ya uhamaji wa hiari wa wakazi kutoka ndani ya hifadhi hiyo.
Mgogoro wa Ngorongoro ulianza kushika kasi mwaka 2022 baada ya baadhi ya wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi hiyo kulalamikia uamuzi wa Serikali wa kuwaondoa katika maeneo ambayo wamekuwa wakiishi kwa miaka mingi.
RaisSamia Suluhu Hassan, apokea Taarifa za Tume ya Rais ya Kutathmini Mgogoro wa Ardhi katika Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na Tume ya Rais ya Kutathmini Zoezi la Uhamaji wa Hiari wa Wakazi wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma.
Malalamiko hayo yaliwavutia pia wanaharakati wa haki za binadamu waliojitokeza kuwatetea wakazi hao, wakidai baadhi yao waliondolewa kwa nguvu na nyumba zao kuchomwa moto, huku Serikali ikisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kulinda mazingira na mfumo wa ikolojia wa Ngorongoro.
Desemba 1, 2024 jijini Arusha, Rais Samia alikutana na kuzungumza na viongozi na wawakilishi wa jamii ya wakazi wa Ngorongoro na kuahidi kuunda tume hizo kuchunguza kwa kina masuala yaliyoibuliwa katika kikao hicho.
Baadaye Desemba 23, 2024, aliunda rasmi tume hizo, ambazo zilianza kazi Februari 20, 2025 kwa jukumu la kuchunguza na kutoa mapendekezo ya namna bora ya kushughulikia mgogoro huo, na leo zimewasilisha ripoti kwa Rais.
Akiwasilisha ripoti ya tume yake, Iyombe amebainisha mambo matano yaliyosababisha kukwama kwa mpango wa uhamaji wa hiari wa wananchi wanaoishi ndani ya Ngorongoro kwenda maeneo mengine yaliyoandaliwa na Serikali, hususan Msomera mkoani Tanga.
Ametaja sababu hizo kuwa ni kutoshirikishwa vya kutosha kwa wananchi, upungufu wa sheria na kanuni zinazoongoza mpango huo, ujenzi wa nyumba moja kwa familia zenye wake zaidi ya mmoja, kupungua kwa motisha kwa waliohama pamoja na mpango huo kuendeshwa zaidi kwa ushawishi badala ya utashi wa wananchi wenyewe.
“Mheshimiwa Rais, shughuli hii haikufanikiwa kama ilivyotarajiwa. Zimehama kaya 1,678 kati ya kaya 23,000 zinazoishi Ngorongoro, na sasa kuna zaidi ya Sh212.35 bilioni ambazo ziko tayari kujenga nyumba kwa watakaohama kwa hiari,” amesema Iyombe.
Mwenyekiti huyo amesema hadi sasa kuna nyumba 1,559 zilizojengwa Msomera ambazo hazijapata wakaaji, sababu ikielezwa kuwa wenye wake zaidi ya mmoja wanapata ugumu wa nyumba moja ataweza kumpa mke yupi.
Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kutathmini Zoezi la Uhamaji wa Hiari wa Wakazi wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro Katibu Mkuu Mstaafu, Mhandisi Musa Iyombe akizungumza katika hafla ya kuwasilisha Taarifa ya Tume yake, Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma Machi 12, 2026.
Tume hiyo iliyoundwa Desemba 2024, imekabidhi taarifa yake yenye kurasa zaidi ya 300, na imeomba pia Serikali kusitisha mara moja kuwajengea nyumba wakazi hao, badala yake iwape fedha ili wajenge nyumba kwa kufuata mila na tamaduni zao.
Pendekezo lingine lililotolewa na Tume hiyo ni kutaka kiundwe chombo maalumu cha kuratibu uhamaji wa hiyari badala ya mfumo unaotumika sasa.
Kuhusu sheria, amesema imekuwa na upungufu kwani inatambua kabila moja la Wamasai wakati kuna makabila mengine, hivyo kuna ubaguzi.
Vilevile, Tume imetaja malalamiko ya waliobaki ikiwemo kukosa huduma za msingi wakati waliohama kilio chao ni mazingira waliyoyakuta.
Malalamiko mengine ni ya wenyeji wa Msomera, ya kuporwa ardhi yao na kupewa wageni.
“Malalamiko ya wananchi kutoka pande zote ni ya msingi. Pamoja na kuwa Serikali inaendelea kuyashughulikia, bado zipo changamoto au malalamiko ambayo hayajafanyiwa kazi.
“Tume inapendekeza kuwa dosari zilizozorotesha mpango wa uhamaji wa hiari na kusababisha wananchi kulalamika zirekebishwe ili wananchi waendelee kuhama kwa hiari,” amesema mwenyekiti huyo.
Hata hivyo, ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika uhamaji huo ikiwemo wananchi kuwa na makazi bora na huduma za kijamii ambazo zimeboreshwa huku wananchi wakiendelea na shughuli za kilimo.
“Tume imebaini kukosekana kwa mpango mahsusi ulioandaliwa kutekeleza uhamaji wa hiari ulioandaliwa katika ngazi ya Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri. Tume inapendekeza kwamba Wizara ya Maliasili na Utalii iandae mpango mahsusi kuhusu uhamaji wa hiari uliojadiliwa na Baraza la Mawaziri,” amesema.
Kwa upande wa Tume ya Dk Ndika ya kutathmini matumizi ya ardhi katika hifadhi hiyo, imependekeza Sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro ifanyiwe marekebisho ili kuondoa utaratibu wa matumizi mseto ya ardhi ndani ya hifadhi hiyo.
Mabalozi kutoka Nchi mbalimbali wakiwa kwenye hafla ya kupokea Taarifa za Tume ya Rais ya Kutathmini Mgogoro wa Ardhi katika Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na Tume ya Rais ya Kutathmini Zoezi la Uhamaji wa Hiari wa Wakazi wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma, Machi 12, 2026.
Amesema Tume inatamani kuona jamii ya wenyeji inawekewa utaratibu wa kuwa na maisha bora kama ilivyo kwa Watanzania wote, hivyo katika maeneo yote matatu yaani Hifadhi ya Ngorongoro, Pori la Akiba la Pololeti na Pori Tengefu la Ziwa Natroni yaendelee kuwa na uhifadhi endelevu kutokana na umuhimu wake, hasa katika kulinda mfumo wa ikolojia wa Serengeti – Mara.
Pia, amesisitiza kwamba maeneo hayo yaendelee kuwa na uhifadhi endelevu wa kulinda na kuendeleza vivutio vya watalii, ili kulinda mapato ya utalii na uendelevu wa bioanuai kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Dk Ndika amesema baada ya tathmini ya kina na ili kushughulikia changamoto na malalamiko yaliyobainika kwa lengo la kuimarisha uhifadhi, shughuli za utalii na huduma za maendeleo ya jamii, wamependekeza mabadiliko ya sheria.
“Mfumo wa matumizi mseto wa ardhi ndani ya hifadhi ya ngorongoro siyo endelevu, hivyo tunapendekezwa kuwa: mosi, Sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro Sura ya 284, ifanyiwe mapitio na marekebisho kwa kuwashirikisha wadau wote muhimu ili iendane na wakati na mahitaji ya wakati wa sasa. Pili, shughuli zisizo za kiuhifadhi zitekelezwe nje ya hifadhi.
“Tatu, ili kuondoa uvamizi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, NCAA (Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro) iwatambue na kuwaorodhesha wakazi wote ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, makazi yao, mifugo na kuwapa cheti kulingana na matakwa Sheria ya Hifadhi ya Ngorongoro,” amesema.
Dk Ndika amesisitiza kuwa uhamaji katika Hifadhi ya Ngorongoro uwe endelevu na uwekewe msingi wa kisheria.
Baada ya kukabidhiwa ripoti, Rais Samia amesema Tume zimetoa mapendekezo ambayo wanakwenda kuyafanyia kazi ili kuboresha shughuli ya uhamaji wa hiari, ikiwemo kurekebisha makosa yaliyofanyika wakati wa utekelezaji wa shughuli ya uhamaji wa awali.
“Taarifa za Tume zimeonyesha umuhimu wa kulinda mifumo ya ikolojia inayounganisha na hifadhi ya Ngorongoro, Pori la Akiba Pololeti na maeneo ya Ziwa Natron. Haya maeneo ni maeneo muhimu sana kwa nchi yetu.
“Maeneo haya ni muhimu kwelikweli, kuna madini yanayotafutwa ulimwenguni, yapo katika maeneo haya. Kwa hiyo ni maeneo ya kuyalinda, ni maeneo muhimu kwa nchi yetu,” amesema kiongozi huyo.
Ameongeza kuwa: “Tumesikia kwamba Serikali tulifanya shughuli hii kwa nia njema lakini tulikosea baadhi ya maeneo na hayo ndiyo maeneo ya kukaa na kutafakari na kurekebisha. Kwa hiyo tutaendelea na shughuli hii baada ya kurekebisha.”
Wakati huohuo, Rais Samia amebainisha sababu za kuhifadhi Ngorongoro akisema ni urithi wa dunia, siyo tu wa Tanzania bali ulimwengu mzima.
Kwa hiyo, amesema ni lazima Watanzania ambao wameshushiwa Ngorongoro na Mwenyezi Mungu walinde urithi huo wa dunia.
“Ni eneo pekee ambalo lina kina cha mita 600 kwenda chini na ikazuka hiyo kreta kwa miujiza ya Mungu na leo mambo yale yako Tanzania lakini situ matokeo yale, bali na utajiri uliomo ndani yake.
“Ni eneo ambalo baiyoanuai yake ni nzuri na haina ushindani duniani, kuna wanyama wa aina zote, walao nyama na majani, ndege wazuri. Kuna vivutio vingi ambavyo sio rahisi kuvikuta kwingineko duniani kwenye bonde moja,” amesema.
Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kutathmini Masuala ya Ardhi katika Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufani Dk Gerald Ndika akizungumza katika hafla ya kuwasilisha Taarifa ya Tume yake, Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma, Machi 12, 2026.
Ameongeza kuna ushahidi wa uwepo wa binadamu wa zamani pale Olduvai, ni sehemu muhimu ya kuhifadhiwa. Ngorongoro ni eneo lenye misitu mingi, pia, kuna maeneo ya volcano.
“Kwa hiyo, ni eneo la kuhifadhiwa, ni eneo la kunyeyekewa, kwa faida ya taifa, lakini kwa faida pia ya ulimwengu au dunia yetu.
“Ni eneo la utalii wa aina nyingi, pale kuna utalii wa game reserve, kuna utalii wa driving, kuna utalii wa kupiga picha, kuna utalii wa aina tofauti tofauti ndani ya eneo moja,” amesema Rais Samia.
