Depu aendeleza moto Ligi Kuu, Nsajigwa hali bado tete

LAURINDO Aurelio ‘Depu’ amempatia kocha Pedro Goncalves kile alichohitaji baada ya kufunga bao pekee wakati Yanga ikiichapa Tanzania Prisons.

Depu ambaye alitokea benchi kipindi cha pili akiingia kuchukua nafasi ya Mohamed Damaro, dakika ya 78 alifunga bao hilo kufuatia kipa wa Tanzania Prisons, Mussa Mbissa kushindwa kuokoa mpira wa faulo uliopigwa na Allan Okello.

Mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa leo Machi 12, 2026 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, ilikuwa yenye matumizi makubwa ya nguvu kuanzia mwanzo hadi mwisho

Kipindi cha kwanza kilionekana kigumu zaidi baada ya timu zote kuamua kucheza mpira bila ya kujilinda sana ambapo mara kadhaa mshambuliaji wa Tanzania Prisons, George Mpole aliwapa wakati mgumu walinzi wa Yanga, Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Bacca.

Pia Prince Dube akiwa anaongoza mashambulizi ya Yanga, aliifanya safu ya ulinzi ya Tanzania Prisons muda wote kuwa makini kulinda lango lao lililokuwa na kipa, Mussa Mbissa.

Katika kipindi hicho cha kwanza, shambulizi lililojengwa na Yanga, mpira ulitoka kwa Dube na kumkuta Mwamnyeto akiwa sehemu nzuri ya kuuweka nyavuni, lakini alichelewa kidogo na walinzi wa Tanzania Prisons wakaondoa hatari hiyo.

Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves ambaye alianza na viungo wa kati watatu, Duke Abuya, Mohamed Damaro na Mudathir Yahya, alipoona anahitaji nguvu zaidi katika ushambuliaji, kipindi cha pili akamtoa Damaro na kuingia Depu.

Pigo la faulo lililopatikana nje kidogo ya boksi la Tanzania Prisons dakika ya 78 baada ya Okello kuangushwa, Mganda huyo akachukua jukumu la kupiga na kumshinda Mbissa, ndipo Depu akaukwamisha wavuni.

Hilo ni bao la sita kwa Depu akiwa ameanza vizuri tangu alipotua kikosini hapo dirisha dogo la usajili Januari 2026.

Yanga kwa ushindi huo, imeifanya kufikisha pointi 35 baada ya kucheza mechi 13, ikishinda 11 na sare tatu. Haijapoteza, ikifunga mabao 31 na kuruhusu mawili, ikiwa ndiyo timu iliyoruhusu mabao machache na kufunga mengi.

Kwa Tanzania Prisons, imeiachia maumivu timu hiyo ambayo tangu ianze kunolewa na Shadrack Nsajigwa, hii ni mechi ya tatu ya mashindano, akipoteza mbili, moja ligi kuu dhidi ya Yanga na nyingine Kombe la FA mbele ya TMA Stars, huku sare moja ya ligi dhidi ya Azam.

Tanzania Prisons imeendelea kukaa nafasi mbaya katika msimamo wa ligi ikishika ya 15 ikibaki na pointi 13 baada ya mechi 16, ikishinda tatu, sare nne na kupoteza tisa, huku timu hiyo ikifunga mabao manane na kuruhusu 17.