Barker ataja sababu za kumuweka benchi Mpanzu

LICHA ya Elie Mpanzu kuonekana kupoteza nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza cha Simba kufuatia ujio wa Anicet Oura na Libasse Gueye, kocha wa timu hiyo, Steve Barker ameweka wazi kuwa bado ana imani kubwa na Mkongomani huyo, huku pia akitaja sababu ya kumuweka benchi.

Mpanzu ambaye kwa kipindi cha karibuni amekuwa akitokea zaidi benchi, ameendelea kuonyesha umuhimu wake ndani ya kikosi hicho, hasa baada ya kufunga bao lililoipa Simba ushindi wa 2-1 dhidi ya Singida Black Stars kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Machi 11, 2026.

Mara ya mwisho kwa Mpanzu kuanza kwenye kikosi cha kwanza cha Simba ilikuwa Februari 14, 2026 katika mchezo dhidi ya Stade Malien, kuhitimisha hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Katika mchezo huo, Mpanzu alicheza kwa dakika 70 kabla ya kufanyiwa mabadiliko.

Tangu wakati huo, Mpanzu amekuwa akianzia benchi huku akipewa nafasi chache za kucheza.

Alitokea benchi katika michezo dhidi ya Tanzania Prisons, Dodoma Jiji na Singida Black Stars, huku pia akibaki benchi Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba.

Kwa ujumla, katika michezo hiyo minne, Mpanzu ametumika kwa jumla ya dakika 63, kati ya dakika 360 za mechi hizo. Hata hivyo, muda huo mfupi haukumzuia kuonyesha mchango wake baada ya kufunga bao la ushindi dhidi ya Singida Black Stars.

Bao hilo lilimfanya kocha Barker kumzungumzia akieleza kuwa bado ni sehemu muhimu ya mipango ya timu licha ya ushindani mkubwa uliopo kwenye safu ya ushambuliaji.

Akizungumza na Mwanaspoti baada ya mchezo huo, Barker alisema kila mchezaji aliyepo ndani ya kikosi cha Simba ana umuhimu wake na uamuzi wa nani acheze au asicheze hutokana zaidi na mahitaji ya kiufundi ya kila mchezo.

“Ni sehemu ya kikosi chetu, hivyo mchezaji yeyote ambaye yupo Simba ni muhimu. Ndio maana Mpanzu bado yupo nasi. Kucheza au kutocheza ni maamuzi ya kiufundi, lakini ni mchezaji muhimu na nina mipango naye,” alisema Barker.

Kocha huyo aliongeza kuwa, ubora wa Mpanzu bado unahitajika ndani ya kikosi hicho, akisisitiza kuwa ushindani uliopo katika safu ya ushambuliaji ndio unaofanya baadhi ya wachezaji wasipate muda mwingi wa kucheza.

Bao alilofunga dhidi ya Singida Black Stars limekuwa la pili kwa Mpanzu katika msimu huu wa Ligi Kuu Bara na limeisaidia Simba kufikisha pointi 27 kwenye msimamo wa ligi ikiwa nafasi ya nne.

Simba kwa sasa ina pointi sawa na Azam FC iliyopo nafasi ya tatu, ingawa Azam ina uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa, huku pia ikiwa na mchezo mmoja mbele. Ushindani katika nafasi za juu za msimamo wa ligi unaendelea kuwa mkali kadri msimu unavyoendelea.

Baada ya ushindi huo dhidi ya Singida Black Stars, Simba sasa inaelekeza nguvu zake katika mchezo ujao wa ligi dhidi ya TRA United utakaochezwa Arusha, mwishoni mwa wiki hii.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, hasa ikizingatiwa kuwa TRA United nayo imetoka kupata ushindi dhidi ya Namungo FC ikiwa nyumbani.