Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Usingizi leo Ijumaa, Machi 13, 2026, tafiti mbalimbali za afya zimebainisha umuhimu wa usingizi bora kwa afya ya mwili na akili.
Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali na dondoo za afya, usingizi ni sehemu muhimu ya maisha ya binadamu kama ilivyo lishe bora na mazoezi ya mwili.
Usingizi wa kutosha husaidia kupunguza msongo wa mawazo, kulinda afya ya moyo, ubungo na kuimarisha kumbukumbu na uwezo wa kufikiri.
Hata hivyo, baadhi ya watu duniani wanatajwa kuendelea kupuuza usingizi licha ya kuwa na mchango mkubwa katika ustawi wa afya na uwezo wa kufanya kazi.
Kwa mujibu wa Taasisi ya American Sleep Association, kati ya watu milioni 50 hadi 70 duniani, wanakabiliwa na aina fulani ya matatizo ya usingizi.
Miongoni mwa matatizo yanayoripotiwa zaidi ni kukosa usingizi (insomnia) pamoja na kukosa pumzi wakati wa usingizi (sleep apnea).
Inawezekana mtu akakosa usingizi kutokana na maumivu, maradhi, mazingira au kujinyima kutokana na matumizi ya simu hadi usiku au shughuli nyingine.
Tafiti zinaeleza kuwa, ukosefu wa usingizi wa kutosha unaweza kuathiri utendaji wa ubongo, kupunguza uwezo wa kufikiri na kuongeza hatari ya magonjwa mbalimbali ikiwamo shinikizo la damu, kisukari na matatizo ya moyo, kukosa ufanisi kazini na kupoteza kumbukumbu.
Aidha, kukosa usingizi kwa muda mrefu kunaweza kuongeza hatari ya kupata uzito kupita kiasi na kudhoofisha kinga ya mwili.
Kawaida binadamu anapaswa kulala saa saba hadi tisa ili mwili kufanya mchakato muhimu wa kurejesha nguvu, kurekebisha seli zilizochoka na kusaidia ubongo kupanga upya kumbukumbu na taarifa zilizokusanywa siku nzima.
Pia, wakati wa usingizi mzito ubongo huondoa taka za kimetaboli zinazoweza kuhusishwa na magonjwa ya mfumo wa fahamu kama vile ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu.
Kutokana na umuhimu huo, wataalamu wanashauri watu kuzingatia kanuni za afya ya usingizi ili kupata mapumziko bora usiku.
Miongoni mwa mambo yanayoshauriwa ni pamoja na kuwa na ratiba maalumu ya kulala na kuamka kila siku, kufanya mazoezi ya mwili wakati wa mchana, kupunguza matumizi ya vinywaji vyenye kafeini kabla ya kulala pamoja na kuweka mazingira mazuri ya chumba cha kulala.
Licha ya tafiti za kimataifa kama ule wa mwaka 2024 (PubMed/systematic review) kuonesha takribani asilimia 16.2 ya watu wazima duniani wana tatizo la kukosa usingizi sawa na watu zaidi ya milioni 852, kundi la vijana kupitia utafiti uliofanywa na Kampuni ya Marekani ya Amerisleep unaonyesha asilimia 70 ya vijana wa Gen Z wanatatizika kulala usiku kwa sababu ya kutokuwa na uhakika wa kifedha, kupanda kwa gharama za maisha pamoja na kutokuwa na uhakika wa kiuchumi.
Utafiti huo uliofanywa na unaonesha katika hilo vijana wengi huripoti kuhisi kulemewa na upangaji bajeti kama kuweka akiba.
Vijana wanasema daima wana wasiwasi kuhusu jinsi ya kusimamia bajeti yao, kulipa kodi ya nyumba na kuendelea na gharama za kila siku.
Badala ya kupumzika, wao hukaa kwenye simu zao au kwenye televisheni, wakijaribu kujizuia kutoka kwenye shinikizo, lakini wanashindwa hali inayowafanya kuwa hatarini.
Kituo cha Udhibiti Magonjwa cha (CDC), takribani theluthi moja ya watu wazima hawapati usingizi wa kutosha, jambo linalohusishwa na hatari ya magonjwa kama unene kupita kiasi, ugonjwa wa moyo, msongo wa mawazo, ajali na majeraha. kwa mujibu wa CDC Sleep Data and Statistics (2024).
Akizungumza na Mwananchi, Sebastian Manase kutoka Dodoma anasema changamoto aliyonayo ya uhusiano na kukosa fedha inamfanya usiku kukosa usingizi.
“Nina kama mwezi sasa hivi nalala saa nane au tisa usiku, nawaza mpenzi wangu ameniacha kisa sina kipato cha kueleweka napata maumivu,” anasema.
Amina Mbwambo kutoka Dar es Salaam anasema hutumia muda mwingi kuwa mtandaoni hasa TikTok kuperuzi na kutizama video siku ambazo haendi chuo, hivyo hujikuta akilala saa saba au nane usiku.
“Huwa naamka kichwa kikiwa kinauma, wakati mwingine ikiwa inanilazimu kuamka mapema napata shida kuamka,” anasema.
Utafiti uliochapishwa kwenye Jarida la Neurology ulionesha insomnia sugu inaweza kuongeza hatari ya matatizo ya kumbukumbu na kuzeesha ubongo kwa takribani miaka 3.5.
Utafiti uliochapishwa kwenye Jarida la Frontiers in Psychiatry uligundua kutumia simu au skrini kitandani huongeza hatari ya insomnia kwa asilimia 59 na hupunguza muda wa usingizi.
Dk Daudi Emmanuel akizungumza na Mwananchi amesema inawezekana umekosa usingizi kutokana na sababu kama maradhi, msongo wa mawazo wa masomo, fedha na kufiwa.
“Mtu mwenye msongo wa mawazo kusaidiwa kwake hakuwezi kuwa sawa na mtu anayeumwa au mwenye sababu nyingine ya kiafya, au anayechezea simu hadi usiku,’ amesema.
Amesema jambo la kufanya kwa mtu mwenye mawazo anaweza kujaribu kutengeneza mazingira mazuri ya kulala katika chumba kisafi chenye mwangaza unaoeleweka, wakati mwingine kusoma kabla ya kulala.
“Kwa wenye changamoto ya mawazo yanayosababisha kukosa usingizi wanapaswa kuonana na wataalamu wa saikolojia, watu wenye maumivu na maradhi wanatakiwa kupata msaada wa kidaktari,” amesema.
Amesema kila mtu akiweka ratiba na mazingira mazuri ya kulala, itapunguza changamoto ya athari zitokanazo na kukosa usingizi.
Daktari bingwa wa ubongo na uti wa mgongo, Mugisha Clement kutoka hospitali ya Aga Khan amesema kitaalamu muda ambao mtu anatakiwa alale ni kati ya saa saba hadi tisa.
Amesema sababu ya wengi kukosa usingizi inawezekana ni msongo wa mawazo unaosababishwa na mtindo wa maisha.
“Watu wanaotumia kahawa au chai kabla ya kulala wanaweza shindwa kupata usingizi, wanaochezea simu au kuangalia filamu wakati wa usiku wanaweza pia kushindwa kulala, mtu akilala anapumzisha ubongo akiamka anakuwa active hata kazini,” amesema.
Kwa mujibu wa World Sleep Society ilianzishwa mwaka 2008, maadhimisho hayo huandaliwa katika zaidi ya nchi 70 duniani kupitia mikutano, kampeni za uhamasishaji na shughuli za kielimu zinazolenga kuongeza uelewa kuhusu afya ya usingizi.
Siku hiyo pia huwapa wataalamu wa afya, watafiti na jamii kwa jumla fursa ya kujadili changamoto za usingizi na kutafuta suluhisho la matatizo yanayowakabili watu wengi duniani.
Kwa watu wanaokabiliwa na matatizo ya usingizi kwa muda mrefu, wataalamu wanashauri kutafuta ushauri wa kitabibu ili kufanyiwa uchunguzi na kupata matibabu sahihi.
Wataalamu wanasisitiza kuwa, usingizi wa kutosha ni nguzo muhimu ya afya njema, hivyo jamii inapaswa kuupa kipaumbele sawa na lishe bora na mazoezi ya mwili ili kuimarisha ustawi wa maisha ya kila siku.
Inashauriwa kuwa, watu wapunguze matumizi ya vifaa vya kielektroniki kama simu, televisheni na kompyuta angalau saa moja kabla ya kulala, kwa kuwa mwanga wa bluu kutoka kwenye vifaa hivyo unaweza kuvuruga mfumo wa usingizi wa mwili.
