Mambo ya kuzingatia unapokula matunda

Dar es Salaam. Matunda ni chakula cha asili chenye virutubisho vingi muhimu kwa afya ya binadamu. Matunda yanaweza kuwa matamu, machungu au kuwa na ladha ya wastani, na mengi huliwa mabichi hali inayosaidia kuhifadhi virutubisho vyake kwa kiwango kikubwa.

Ofisa lishe mtafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Fatma Juma, anataja mambo  muhimu ya kuzingatia katika ulaji wa matunda katika maisha ya binadamu. 

Mambo hayo ni pamoja na kufahamu maana ya matunda, aina zake, sifa na upatikanaji, umuhimu wake kiafya, namna bora ya kuyaandaa, mambo ya kuepuka wakati wa maandalizi, kiasi kinachotakiwa kuliwa kwa siku pamoja na namna ya kuyaendeleza katika jamii.

Anasema kuwa mtu anayezingatia masuala hayo hujiweka katika nafasi nzuri ya kuwa na afya bora na kuimarisha kinga ya mwili

 Anafafanua kuwa matunda ni chakula cha asili chenye vitamini na madini muhimu kwa mwili wa binadamu na yanaweza kuliwa mabichi huku yakibaki na virutubisho vingi vinavyohitajika.

Anasema matunda hupatikana katika aina mbalimbali kulingana na msimu na maeneo yanapopatikana. Kuna matunda ya msimu kama embe, nanasi   ambayo hupatikana kwa wingi wakati wa msimu wake na bei yake huwa nafuu. 

Pia yapo matunda yanayopatikana mwaka mzima kama ndizi na mapera, ingawa bei zake hubadilika kidogo kulingana na kipindi.

Aidha, kuna matunda ya asili yanayojiotea porini kama ukwaju, ubuyu, mabungo, masungwi na mengineyo, pamoja na matunda yanayolimwa kama mapapai, maembe, machungwa, mananasi, matikiti maji na mafenesi. Uwepo wa matunda haya humuwezesha mtu kuwa na chaguo pana la chakula cha asili chenye virutubisho muhimu kwa afya.

Kwa upande wa umuhimu wake, Fatma anasema matunda yana vitamini, madini na nyuzinyuzi zinazosaidia shughuli mbalimbali za mwili ikiwemo utengenezaji wa damu, mmeng’enyo wa chakula na uzalishaji wa nishati. Pia husaidia kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali.

Anabainisha kuwa nyuzinyuzi zilizopo kwenye matunda husaidia mmeng’enyo wa chakula kwa kuongeza ujazo wa kinyesi na kurahisisha usafirishaji wake kwenye utumbo, hali inayosaidia kuzuia tatizo la kufunga choo. 

Ulaji wa nyuzinyuzi pia hupunguza hatari ya kupata matatizo ya mfumo wa chakula kama bawasiri na saratani ya utumbo mpana.

Matunda pia yana mchango mkubwa katika afya ya ngozi kwa kusaidia kuifanya iwe laini, yenye unyevunyevu, kuzuia makunyanzi na kukarabati seli zilizoharibika. 

Anasema matunda yenye rangi ya machungwa kama mapapai na matikiti maji, husaidia kuboresha uwezo wa kuona, kuzuia upofu wa usiku na kupunguza hatari ya magonjwa sugu kama kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.

Ili kupata faida kamili ya matunda, jamii inashauriwa kuchagua matunda safi na salama. Fatma anasema unaponunua sokoni ni vyema kuchagua matunda ya msimu kwani hupatikana kwa urahisi, huwa mapya na bei yake ni nafuu. Kwa wale wanaovuna kutoka kwenye miti yao, wanashauriwa kuchagua matunda yaliyoiva vizuri na ambayo hayajaharibiwa na wadudu au wanyama.

Anasisitiza umuhimu wa kuosha matunda kwa maji safi yanayotiririka ili kuondoa vumbi, uchafu na mabaki ya dawa. 

Pia anashauri kutumia vifaa safi wakati wa kukata au kuandaa matunda, akionya kuwa kutumia kisu au ubao uliotumika kukata nyama mbichi bila kuoshwa kunaweza kusababisha maambukizi ya vijidudu.

Kwa matunda ambayo maganda yake yanaweza kuliwa kama mapera, maembe, zabibu na peasi, anashauri yasimenywe kwani maganda yana virutubisho muhimu. 

Vilevile, anaonya kuepuka kuhifadhi matunda karibu na taka au maeneo yenye wadudu kama nzi kwa kuwa hali hiyo huongeza hatari ya uchafuzi.

Kuhusu kiasi, anasema mtu mzima anashauriwa kula angalau matunda mawili kwa siku, ambapo kipimo kimoja kinaweza kuwa chungwa moja, ndizi moja, nusu parachichi au nusu embe kubwa. Watoto nao wanahitaji kula matunda mara kwa mara ili kusaidia ukuaji wao na kuimarisha afya.

Matunda yanashauriwa kuliwa katika hali yake halisi baada ya kuoshwa vizuri. Kwa watoto wadogo, matunda yanaweza kukamuliwa au kupondwa na kutolewa kwa kijiko. 

Hata hivyo, Fatma anasisitiza kuwa kula tunda zima ni bora zaidi kuliko kunywa juisi kwani mara nyingi juisi huongezewa maji na sukari hivyo kupunguza faida zake kiafya.

Kwa upande wa kuendeleza upatikanaji wa matunda, jamii inahimizwa kupanda miti ya matunda majumbani, shuleni na katika maeneo ya umma. Anasema badala ya kupanda maua pekee, watu wanaweza kupanda matunda yanayoota chini kama strawberry au kupanda miti kama miembe ambayo hutoa kivuli na matunda wakati wa msimu.

 Pia anasisitiza umuhimu wa kutoa elimu kupitia vyombo vya habari na kuboresha mazingira ya masoko ili kurahisisha upatikanaji wa matunda kwa jamii.