Kwa niaba ya Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira (TRAMEPRO), napenda kuungana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na jumuiya ya kimataifa katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Figo. Siku hii ni muhimu katika kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda na kutunza afya ya figo.Takwimu za kimataifa zinaonesha kuwa zaidi ya watu milioni 850 duniani wanaishi na aina fulani ya ugonjwa wa figo, huku takribani asilimia 10 ya watu wazima duniani wakiwa na dalili za ugonjwa huo. Aidha, mamilioni ya watu hulazimika kutegemea matibabu ya gharama kubwa kama dialysis au upandikizaji wa figo (kidney transplant) ili kuendelea kuishi.
Barani Afrika, tafiti zinaonesha kuwa kati ya asilimia 13 hadi 15 ya watu wazima wanaweza kuwa na dalili za ugonjwa wa figo. Nchini Tanzania, tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa takribani asilimia 10 hadi 12 ya watu wazima wanaweza kuwa katika hatari au tayari wana dalili za ugonjwa wa figo, huku wengi wakigundulika katika hatua za mwisho za ugonjwa.
Gharama za matibabu ya magonjwa ya figo ni kubwa sana. Mgonjwa anayehitaji dialysis hulazimika kufanya matibabu hayo mara mbili hadi tatu kwa wiki, ambapo gharama ya kikao kimoja inaweza kufikia wastani wa dola za Marekani 80 hadi 200. Hii ina maana kuwa kwa mwaka mmoja, gharama za matibabu zinaweza kufikia dola 10,000 hadi 25,000 au zaidi kwa mgonjwa mmoja.
Aidha, matibabu ya upandikizaji wa figo (kidney transplant) yanaweza kugharimu kati ya dola 15,000 hadi 30,000, bila kujumuisha gharama za dawa za kudhibiti kinga ya mwili ambazo mgonjwa hulazimika kutumia maisha yote.
Kutokana na hali hii, ni wazi kuwa kinga ni bora zaidi kuliko tiba, na jamii inapaswa kuhamasishwa kuchukua hatua za kulinda afya ya figo mapema.
Katika muktadha huu, tiba asilia ina nafasi muhimu katika kusaidia kuimarisha kinga ya mwili na afya kwa ujumla. Hata hivyo, bado kuna changamoto ya uhaba wa ushahidi wa kisayansi unaothibitisha kwa kina baadhi ya dawa na mbinu za tiba asilia. Kwa sababu hiyo, TRAMEPRO inaendelea kusisitiza umuhimu wa tafiti za kisayansi, uthibitishaji wa dawa za asili, na ushirikiano kati ya wataalamu wa afya na taasisi za utafiti.
Kwa sasa, nikiwa katika ziara ya kitaaluma mjini New Delhi, India, ninapata uzoefu na kujifunza kuhusu matibabu mtambuka (Integrative Medicine) katika taasisi mbalimbali ikiwemo Max Super Speciality Hospital pamoja na taasisi za tiba asilia chini ya mfumo wa AYUSH. Uzoefu huu unalenga kuimarisha uelewa na ushirikiano katika kuunganisha tiba asilia na tiba za kisasa kwa manufaa ya afya ya jamii.
TRAMEPRO itaendelea kushirikiana na taasisi za utafiti, hospitali, na wataalamu wa magonjwa ya figo ili kuendeleza tafiti, kutoa elimu kwa jamii, na kuhakikisha matumizi salama na yenye tija ya tiba asilia.
Katika maadhimisho haya, ninatoa wito kwa:
Watabibu wa tiba asilia kuzingatia viwango vya usalama, maadili ya kitaaluma na uthibitisho wa kisayansi katika huduma wanazotoa.
Wananchi kuchukua hatua za kinga dhidi ya magonjwa ya figo ikiwa ni pamoja na kudhibiti shinikizo la damu na kisukari, kunywa maji ya kutosha, kutumia dawa kwa usahihi, na kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara.
Serikali na taasisi za utafiti kuendelea kuwekeza katika tafiti za dawa za asili na kuimarisha mfumo wa huduma za afya jumuishi.
Kwa pamoja tunaweza kujenga mfumo wa afya unaounganisha hekima ya tiba asilia na sayansi ya tiba ya kisasa kwa manufaa ya binadamu na mazingira yetu.
Mungu aibariki Tanzania na awajalie wananchi wake afya njema.
Boniventura Mwalongo Katibu Mkuu – TRAMEPRONew Delhi, India 12 Machi 2026