Wiki saba zijazo nchi yetu itajiunga na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi (Mei mosi), tunayoaminishwa kuwa, ni kwa ajili ya wafanyakazi na sio wastaafu, ambao labda watakuja tengewa siku yao, japo kitaifa tu!
Maana tunaaminishwa pia, ukisha achia ngazi mchuma uondoke, wewe ni mstaafu na Siku ya Wafanyakazi haikuhusu tena, japo ulikuwa ni mfanyakazi, sasa unabaki ili kuhakikiwa tu kama bado uko hai au umeishakua mkazi wa Kinondoni.
Unategemewa sasa uchape lapa na uishie Kimbiji, usubiri kama mwenye huruma mmoja atakuja kuwapa siku ya wastaafu.
Mstaafu hawezi kuthibitisha chochote kama huko duniani siku hii ya wafanyakazi inakuwa na umuhimu wowote kwa wastaafu waliokuwa wafanyakazi au yanakuwa yale yale ya wafanyakazi kuambiwa na wahusika kuwa tuna jambo letu!
Mstaafu amekuwa akijiuliza sana kwamba, inakuwaje wahusika hawafanyi hesabu zinazohusika mwaka mzima ili siku ya Mei mosi, mgeni wa heshima anafika pale na hesabu kamili na anatoa kilichopo na sio ahadi za ‘tuna jambo letu.”
Mbona wakati tunaijenga nchi yetu hii ilikuwa ikiwezekana?
Mgeni wa heshima alikuwa kila Siku ya Wafanyakazi akitangaza nyongeza ya mishahara ya wafanyakazi, hata ikiwa 250 (msikiege, tukisema tunatoka mbali!) na tutarudi nyumbani tukifurahi kwa kuongezwa mshahara shilingi nyingi sana mbili unusu!
Enzi hizi za vikokotozi si ndio ingekuwa rahisi zaidi na sio ahadi za ‘tuna jambo letu’ na likachukua miezi hadi kutimizwa!
Mstaafu anawasliana na wastaafu wenzake wa kweli sio wale wa kuvaa suti wanaosemekana kuwawakilisha wastaafu kwenye nini sijui, wakati pensheni ya mwezi ya shilingi laki moja na elfu tano imedumu kwa miaka ishirini na wao wapo tu wakiwakilisha, lakini dhahiri sio kwenye kuwapambania wapate nyongeza ya pensheni!
Mstaafu anafikiria kuwasiliana na wastaafu wenzake ili wapange mikakati ya amani ya kwenda kushiriki maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi na wastaafu ya mwaka huu bila kuwa na haja ya kualikwa rasmi kutokana siku hii kuaminishwa kwamba, ni ya wafanyakazi tu walio kazini, na sio wastaafu, japo kwa miaka 40 iliyopita walikuwa ni ‘never miss’ wa siku hiyo!
Ndio, tutashauriana twende kwa amani, rudia hapo kwa amani, kama Gen O, Old is God’s Gold’ ama tutakwenda kama chama cha sawa sauti ya wastaafu kwa nauli yetu na sio mpaka tubembeleze mtu!
Mstaafu wetu angependa kusisitiza hapo ‘kwa amani’ maana kuna watu wakisikia tu kuna wazee wanakwenda kuadhimisha Mei mosi bila kualikwa, vichwa vyao hupata moto na virungu na mabomu ya machozi huhamia kwenye ubongo kisha kwenye mikono!
Hatutakuwa na mengi. Kwanza nyongeza ya pensheni ya wa kima cha chini ifike shilingi laki tano kwa mwezi. Inawezekana. Ni utashi tu. Kama nchi inaweza kulipa watu milioni 24 kwa mwezi, basi inaweza kabisa kuwalipa shilingi laki tano kwa mwezi kwa wastaafu waliojenga nchi hii na kuifikisha ilipo. Rudia, ni utashi tu.
Mbili, wakati umefika sasa wa hivi vibubu vya akiba ya wafanyakazi kuanzisha benki ambayo wastaafu wanaweza kupata mikopo midogo kirahisi maana hela yao ipo humo na itakuwa kama dhamana yao, badala ya kuwaacha wakibamizwa na hizi benki za kidotcom ambazo tozo za mikopo kwa mfanyabiashara na mstaafu ni moja! Vibubu vianzishe benki.
Tatu, na hili ndio kubwa zaidi. Siri-kali na vibubu viangalie kumlipa mstaafu shilingi milioni tano na laki tano akiwa hai, rudia, akiwa hai na kumpa akiwa tayari mkazi wa Kinondoni! Mpeni mwenyewe afaidi mwishoni mwishoni jasho lake mwenyewe maana watoto wake tayari wana ajira zao pamoja na kikokotoo kuwahusu wataweza kumzika mdingi wao.
Mpeni mstaafu milioni tano na laki tano zake mlizoahidi akiwa hai na sio akiwa Kinondoni!
Nimemaliza. Tungoje Mei mosi tu, ‘gate crash’ maadhimisho yatapofanyika tuyasisitize hayo matatu muhimu sana.
0754 340606 / 0784 340606
