Ramadhani ni mwezi wa toba, kuokolewa na moto

Mwezi wa Ramadhani ni mwezi ambao milango ya pepo hufunguliwa na milango ya moto hufungwa.

Katika mwezi huu, Allah Mtukufu huwapa neema waja wake wanaofunga kwa kuwaokoa na moto wa jahannam. Moto ambao joto lake ni kali sana, kina chake ni kirefu, na adhabu yake ni nzito. Mtume wa Allah (rehema na amani ziwe juu yake) alisema kila siku usiku wa Ramadhani, Allah huwa na watu anaowaokoa na moto, na kila mmoja wao huwa na dua inayokubaliwa.

Pia, katika kila wakati wa kufuturu kuna watu wanaoachiwa huru na moto. Katika baadhi ya riwaya imeelezwa kuwa kila usiku wa Ramadhani watu 60,000 huokolewa na moto.

Lengo kuu la mja hapa duniani ni kuondoka akiwa amepata radhi za Allah, ameandikiwa pepo, na ameokolewa na moto. Huo ndio ushindi wa kweli.

Allah Anasema: “Basi atakayeepushwa mbali na moto na akaingizwa peponi, huyo amefaulu. Na maisha ya dunia si chochote ila ni starehe ya udanganyifu.

Hii ni hamasa kwa wafungaji kuzidisha dua, hasa wakati wa kufuturu, wamuombe Allah awajibu maombi yao, awaondolee shida zao, na awatimizie matarajio yao.

Hizi hapa baadhi ya sababu za kuokolewa na moto.

Mosi: Kuwa na ikhlasi (unyenyekevu wa moyo kwa Allah pekee) katika matendo, maneno na hali zako zote kwa siri na kwa dhahiri Ikhlasi ni kufanya kila jambo kwa ajili ya Allah tu, bila kutafuta sifa za watu, umaarufu, matamanio, wala masilahi ya dunia.

Na miongoni mwa alama ya ikhlasi, kuwa na bidii katika ibada, kupenda matendo yako yajulikane na Allah pekee. Na kutokuwa na tamaa ya kusifiwa na watu. Anayetaka daraja hii, ajitahidi kwa dhati.

Pili: Kuifunga vizuri swaumu kwa kuepuka ria (kujionyesha) kujiepusha na maasi na kutekeleza wajibu wote ipasavyo, hususan kusimamisha swala tano za faradhi. Mtume wa Allah amesema:

“Saumu ni ngao; mja hujikinga nayo dhidi ya moto.” Saumu ni kama ngao ya kivita, huwa inamlinda mfungaji dhidi ya matamanio duniani na adhabu ya akhera.

 Tatu: Swaumu ni sawa na kuacha huru mtumwa, ikiwa kuacha huru mtumwa ni sababu ya kuokolewa na moto na saumu nayo ni sababu ya kuokolewa na moto.

 Lakini saumu hiyo iwe ya kuacha maasi, kuepuka makosa madogo, Saumu ya viungo (macho, masikio, ulimi), na zaidi ya yote, saumu ya moyo (kuacha kila kinachomshughulisha na Allah).

Ramadhani si mwezi wa kupuuza anasa za dunia, bali ni fursa ya pepo na kuokoka na moto.

“Anapofunga mmoja wenu, asiseme maneno machafu wala asifanye fujo; akitukanwa aseme: Mimi nimefunga.” Kadhalika amesema “Asiyeacha kusema uongo na kuutenda, Allah hana haja ya yeye kuacha chakula na kinywaji.”

Nne: Miongoni mwa sababu za kuokolewa na moto ni kuwalisha wahitaji, hasa katika Ramadhani.

Allah Ameweka kulisha masikini kuwa mbadala wa kuacha mtumwa huru katika baadhi ya kafara.

Hii inaonyesha cheo kikubwa cha kitendo hiki. Mtume wa Allah amesema: “Atakayemfuturisha mfungaji, atapata ujira sawa na wake bila kupungua chochote.”.

Tano: Kulia kwa hofu ya Allah Mtume wa Allah amesema:

“Hataingia motoni mtu aliyelia kwa hofu ya Allah.”

Ramadhani ni mwezi wa kulainika kwa nyoyo.

Katika swala za tarawehe na tahajjud (swala ya usiku wa manane), macho hutokwa na machozi, nyoyo hutetemeka. Hata chozi moja la kweli kwa hofu ya Allah linaweza kuwa sababu ya kuokoka kwako.

 Na miongoni mwa watu saba watakaokuwa katika kivuli cha Arshi siku ya Kiyama ni: Mtu aliyemkumbuka Allah akiwa peke yake, macho yake yakatokwa na machozi.

Tunamuomba Allah Atupe macho yanayolia kwa hofu yake, nyoyo zenye unyenyekevu, na atuandike miongoni mwa waliokombolewa na moto katika mwezi huu mtukufu.

Sita: Kung’ang’ania dua ya kuomba kuokolewa na moto. Mtume wa Allah amesema: “Hakuna Mwislamu anayemuomba Allah pepo mara tatu isipokuwa pepo husema: ‘Ewe Allah mwingize peponi.’

Wala hakuna anayejikinga na moto mara tatu isipokuwa moto husema: ‘Ewe Allah muokoe na mimi.’” (Ahmad).

Hivyo zidisha dua ya kuomba uachiliwe huru na moto.

Omba kwa unyenyekevu, ukiwa na udhu, ukielekea Qibla, ukimsifu Allah na kumtaja kwa majina yake mazuri.

Tafuta nyakati za kujibiwa dua, kama vile wakati wa theluthi ya mwisho ya usiku, wakati wa adhana, kati ya adhana na iqama, baada ya swala za faradhi, Ijumaa pindi hatibu anapopanda katika mimbari hadi swala imalizike, na saa ya mwisho baada ya Alasiri siku ya Ijumaa.

Kisha sisitiza dua yako, na ni vyema kuifuatisha dua hiyo kwa kutoa sadaka ili ikubaliwe haraka.