Zoezi la Pamoja Kati ya JWTZ na Jeshi la Marekani Lahitimishwa Msata

Bakari Mahundu
March 13, 2026
0 Comments

Picha ya Pamoja ya Kikosi Maalumu cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Kikosi cha Walinzi wa Taifa kutoka Jimbo la Nebraska, Marekani

Zoezi la pamoja la medani Justified Accord 2026 lililohusisha Kikosi Maalumu cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Kikosi cha Walinzi wa Taifa kutoka Jimbo la Nebraska, Marekani, limehitimishwa Machi 12, 2026 katika Kata ya Msata, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani. Zoezi hilo lililodumu kuanzia Februari 23 hadi Machi 13, 2026 lililenga kuimarisha ushirikiano wa kijeshi, kubadilishana uzoefu wa kiutendaji, pamoja na kujenga uwezo wa kukabiliana na majanga ya asili, uhalifu wa kimtandao na utoaji wa huduma za tiba.

Akifunga rasmi zoezi hilo, Mkuu wa Kamandi ya Vikosi chini ya Makao Makuu ya Jeshi, Meja Jenerali Said Nkambi, alisema majeshi hayo mawili yameendelea kujijengea uwezo na heshima kupitia mafunzo ya pamoja, huku akisisitiza kuwa ushirikiano huo umeongeza ufanisi katika mbinu za medani, huduma za tiba na shughuli za kijamii zinazolenga kujenga mtazamo chanya kwa wananchi. Aliongeza kuwa Marekani ni mshirika wa kimkakati wa Tanzania, na majeshi hayo yataendelea kubadilishana uzoefu katika nyanja za sayansi, teknolojia na operesheni za kijeshi.

Hafla ya kufunga zoezi hilo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kijeshi na kiraia, akiwemo Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andrew Lentz, pamoja na Mkuu wa Kamandi ya Marekani Ulaya Kusini anayeshughulikia shughuli maalumu barani Afrika, Meja Jenerali Craig Strong. Viongozi hao walipongeza mafanikio ya zoezi hilo na kueleza kuwa tathmini itafanyika ili kubaini mapungufu na kuboresha maandalizi ya mafunzo yajayo.

Katika kuendeleza ushirikiano huo, Jeshi la Marekani kupitia Kikosi cha Walinzi wa Taifa Nebraska, kinachosimamia pia Wakala wa Usimamizi wa Huduma za Dharura wa Jimbo la Nebraska (NEMA), limelikabidhi Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania magari tisa ya huduma za dharura kwa ajili ya kusaidia uokoaji wakati wa majanga. Aidha, ujumbe huo ulitembelea Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam kujionea utoaji wa huduma za tiba, ikiwa ni sehemu ya kubadilishana uzoefu katika sekta ya afya ya kijeshi.