******
Wakala wa Nishati Vijijini (REA), umeendelea kutekeleza miradi ya kupeleka huduma ya umeme katika maeneo ya vitongoji ili kuwawezesha wananchi waliopo maeneo hayo kupata huduma bora ya nishati ya umeme kwa ajili ya Maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Hayo yamebainishwa na Msimamizi wa Miradi ya REA, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mha. Danstan Kalugira wakati akizungumza na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kuhusu miradi inayotekelezwa na REA katika wilaya ya Ludewa mkoani Njombe.
Mha. Kalugira amesema kuwa, kiasi cha fedha takribani shilingi bilioni 3.1 tayari zimetolewa na Serikali kupitia REA ili kutekeleza mradi huo wa kupeleka umeme kwenye vitongoji takribani 6 vya wilaya ya Ludewa ili wananchi wanufaike na huduma ya umeme.
“Katika mradi huu hapa wilayani Ludewa, mkandarasi kampuni ya SUMA JKT ndiye anayetekeleza mradi huu mkubwa ambao unatarajiwa kuunganishia wateja wapatao 160 wa awali mara baada ya mradi kuwa umekamilika, ” Amesema Mha. Kalugira
Ameongeza kuwa, japokuwa kipindi hichi ni cha masika mvua nyingi zinanyesha ila mkandarasi huyo anaendelea kutekeleza mradi kwa kasi, weledi na ni matarajio kuwa atakwenda kumaliza mradi huo kwa wakati katika muda uliopangwa ili wananchi watakaounganishwa na nishati ya umeme waweze kunufaika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Bw. Deodatus Balile ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha ya utekelezaji wa miradi hiyo inayoendelea katika mkoa wa Njombe na maeneo mengine nchini.
“Tumejionea kwa macho yetu namna fedha hizi zinazotolewa na Serikali na jinsi zinavyotekeleza miradi ya kupeleka huduma ya umeme katika wilaya hii ya Ludewa ili wananchi wapate nishati bora ya uhakika, ” Amesisitiza Bw. Balile.
Ziara ya TEF imelenga kutembelea miradi ya kimkakati inayotekelezwa na REA katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo miradi ya Awamu ya Pili B (HEP 2B) ya kupeleka umeme kwenye vitongoji vipatavyo 9,009.
Mwisho








