Migogoro ya ardhi yatikisa ziara ya Kihongosi

Mwanza. Migogoro ya ardhi imekuwa fupa gumu kwenye Jiji la Mwanza huku wilaya za Ilemela na Nyamagana zikidaiwa Sh14 bilioni za fidia na wananchi.

Hayo yamebainika kwenye mkutano wa hadhara wa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi katika ziara yake ya kichama mkoani humo.

Katika mkutano huo uliofanyika jana Alhamisi, Machi 12, 2026 kwenye Uwanja wa Furahisha, Kihongosi alizungumza na mamia ya wananchi waliojitokeza licha ya mvua kunyesha maeneo mengi ya jiji hilo.

Kero za migogoro ya ardhi ndizo ziliteka mkutano huo baada ya karibu nusu ya wananchi waliopata nafasi ya kusikilizwa changamoto zao kutaja migogoro ya ardhi.

Si Mwanza pekee migogoro imekuwa kero kwani hata katika ziara mbalimbali ambazo Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amezifanya mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Rukwa sehemu kuwa ni migogoro ya ardhi.

Katibu wa NEC, Itikadi,  Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika viwanja vya Furahisha, Mwanza.

Ni kutokana na kadhia hiyo, Dk Mwigulu Machi 10, 2026, akiwa Sumbawanga mkoani Rukwa aliwataka viongozi na mawaziri wa kisekta kutafakari na kupendekeza mbinu itakayoleta suluhu ya kudumu.

Waliopewa jukumu hilo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Hamza Johari, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Leonard Akwilapo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe.

Kwa mujibu wa Dk Mwigulu, viongozi hao wanapaswa kukaa kwa dharura na kuja na mapendekezo yatakayomaliza migogoro ya ardhi iliyodumu kwa miaka mingi.

Amesema Serikali haiwezi kuendelea kuvumilia hali inayosababisha wananchi kulalamika na kukosa haki katika umiliki wa ardhi.

“Nimwelekeze Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Ardhi na Waziri wa Tamisemi kaeni kwa dharura na wataalamu wenu mfanye tathmini kama tatizo hili ni la kisera, kisheria au kimuundo. Lazima tupate jawabu na tufute machozi ya wananchi,” amesema.

Aliyokutana nayo Kihongosi

Katika mkutano wa Kihongosi, miongoni mwa waliolalamika ni Chacha Daniel aliyeambatana na baba yake aliyemtambulisha kwa jina la Mzee Erasto na kudai watumishi wa jiji wanajimilikisha viwanja vya watu, kikiwamo cha kwao cha mita za eneo 6,300 kilichopo Bugarika.

Alidai mwaka 2006 Halmashauri ya Jiji lilipima maeneo ya Bugarika katika mradi alioutaja kwa jina la Viwanja 3,500 na wenye maeneo yao kuthaminiwa.

“Wananchi tuliokuwa eneo hilo tuliondolewa. Hata hivyo, tulitakiwa kupewa viwanja vipya, lakini haikuwa hivyo mpaka sasa. Wanayenifanyia hivi ni wenyekiti wa CCM Kata ya Igombe, itakuwaje kwa mwananchi wa kawaida,” alihoji Daniel.

Mmoja wa wananchi wa Mwanza, akiwasilisha kero yake kwenye mkutano wa hadhara wa Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi, Kenani Kihongosi.

Kihongosi alimhoji mkuu wa Idara ya Ardhi Mwanza, Patrice Rwagasira kama analifahamu jambo hilo na kusema ndiyo na linawahusu wananchi 300 wa Bugarika ambao walifanyiwa uthamini.

“Lilipoletwa kwangu kwa kuwa mwaka 2006 sikuwepo ofisini nikajipa muda kulifahamu jambo hili na kubaini ni wananchi 300 wa Bugarika ambao walifanyiwa uthamini na kupewa fidia.

Alisema wale waliokuwa wamefanya uendelezaji kwenye maeneo yao, walipewa viwanja vingine na fidia na ambao hawakuwa wameendeleza walipewa fidia pekee.

“Huyu mzee (Daniel) naye alithamimiwa, lakini hakujitokeza kulipwa fidia hadi mwaka 2018 alipojitokeza na kutaka apewe kiwanja wakati haki yake ilikuwa ni fidia ambayo ipo hadi sasa, vilevile hivi sasa Bugarika ni eneo ambalo limeendelezwa kisasa,” amesema.

Changamoto kama hiyo ilitolewa na Pili Karume ambaye alidai waliondolewa kwenye maeneo yao ili kupitisha Barabara ya Kenyatta na hawajalipwa fidia.

Sawa na alichokisema Elias John ambaye alidai maeneo yao yalichukuliwa na kupewa mwekezaji lakini hawajalipwa fidia.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda alieleza changamoto kubwa kwenye mkoa huo ni migogoro ya ardhi Ilemela na Nyamagana.

Amesema Serikali inapaswa kutenga Sh14 ilioni ili kuwalipa fidia wananchi wa maeneo hao.

“Nyamagana wananchi wanadai fidia Sh8 bilioni na Ilemela Sh6 bilioni, tumekubaliana kwenye bajeti ijayo, halmashauri zote (Ilemela na Nyamagana) angalau ziweke asilimia 30 kulipa wananchi,” amesema.

Hata hivyo, aliwasilisha ombi kwa Kihongosi kwamba, wanaomba wizara fedha iwape mkopo wa pesa hizo ili walipe wananchi fidia na kumaliza changamoto ya migogoro ya ardhi, kisha Serikali kupitia wizara hiyo waendelee kuzidai halmashauri hizo.

Katika changamoto hizo, Kihongosi alitaka mamlaka husika kulisimamia na kulimaliza kwa kuhakikisha haki inatendeka kwa kila mmoja.

Alisema Chama cha Mapinduzi kitaendelea kusimamia misingi ya haki na ustawi wa wananchi, akiwasisitiza wananchi kuendelea kukiamini kwa kuwa ndicho kitakachowaletea maendeleo.

Kero nyingine katika mkutano huo ilikuwa ya ujenzi wa soko mtaa wa Malimbe, Kata ya Luchelele ambayo ilitolewa na Mahela Kalemela.

Alidai wananchi walijenga soko hilo kwa nguvu zao, lakini wamekatazwa kuliendeleza, ndipo Kihongosi alimtaka mkurugenzi wa halmashauri kulitolea ufafanuzi.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya, Amina Makilagi alitoa ufafanuzi huo akisema hilo si eneo la wananchi ni la masista ambao walipewa na aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa wa Mara, Mussa Kaisi (sasa ni marehemu) ambaye hakuwa na mtoto, hivyo alilitoa kama zawadi kwa masista.

Kero nyingine aliwasilishwa na Merciana Paulo ambaye alidai kudhulumiwa Sh78 milioni na moja ya chuo cha dini ambako alipewa tenda ya chakula.

Kihongosi aliagiza ofisi ya mkuu wa mkoa kulishughulikia suala hilo, pande zote mbili ziitwe na mwenye haki yake apatiwe kwa mujibu wa sheria.

Mkuu wa wa mkoa alisema atawasiliana na  polisi, mwanasheria mkuu wa serikali, mlalamikiwa na mlalamikaji ili kubaini nani mkweli katika hilo na haki itendeke.

Katika hatua nyingine, Kihongosi alimtaka mganga mkuu wa wilaya, kumsaidia kijana ambaye mzazi wake alisema amekosa pesa ya matibabu kutokana na kusumbuliwa uvimbe sehemu za siri.

Changamoto ya wazee kutozwa gharama wanapokwenda kupata matibabu iliibuka kwa mara nyingine, baada ya kuibuliwa pia wilayani Magu na Kahama mkoani Shinyanga katika ziara hiyo.

Kuhusu hilo Kihongosi aliwaagiza waganga wakuu wa maeneo hayo kufanya uchunguzi wa suala hilo na atakayebainika kwenda kinyume na sera ya afya achukuliwe hatua.

Mkutano huo ulikuwa faraja kwa Happiness Benedictor aliteeleza kusagika nyonga na kushindwa gharama ya matitabu ya kuwekewa bandia katika Hospitali ya Bugando.

Alipomuuliza gharama, alisema alipopimwa awali ilikuwa Sh14 milioni na Kihongosi akasema Chama kitalisimamia hilo.

Alimwambia mwenyekiti wa CCM mkoa kwamba hawawezi kushindwa kuokoa maisha ya huyo mama na kabla mkutano haujaisha, Kihongosi alimwambia mganga mkuu wa wilaya aangalie kwenye simu yake ametumiwa Sh15 milioni za matibabu ya mama huyo.