New Stone na mtego wa kuepuka kushuka daraja ZPL

LICHA ya timu ya New Stone Town kuvuna alama tatu kwenye michezo 20 iliyocheza, bado ina matumaini ya kubaki salama katika Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), huku hesabu zao ni kushinda mechi 10 zilizobaki.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mussa Bajaka alisema endapo watashinda mechi hizo, watakuwa na alama 33 katika msimamo, ambao utawapandisha nafasi za juu kutoka mkiani walipo sasa, huku wakiwaombea mabaya wapinzani wao wapoteze ili wao wabaki salama.

Akizungumza na Mwanaspoti, Bajaka alisema kwamba mechi hizo zitatumika kama safari ya kubaki ligi kuu msimu huu, ambao ndio mara yao ya kwanza kushiriki. Alisema, matokeo yaliyopatikana katika mechi walizocheza hadi sasa, hasa mzunguko wa kwanza ambayo si mazuri, yamesababishwa na ugeni katika ligi hiyo, japokuwa kwa mzunguko wa pili wamerudi tofauti.

“Kila mechi ni ushindi kwetu, na hiyo ndiyo njia pekee tutakayoitumia katika mzunguko huu wa mwisho, na hiyo ndio itakayoinusuru timu isishuke daraja,” alisema.

Bajaka alisema tatizo lingine linaloitafuna Ligi ya Zanzibar ni kusimama mara kwa mara, jambo ambalo linadhoofisha wachezaji kwani muda mwingi wanaumia nje ya viwanja.

Alisema kwamba hilo linaiathiri timu nyingi kwani hazina uwezo wa kuwazuia wachezaji wasiondoke kwa kipindi chote ambacho ligi imesimama.

“Kwa hivyo, timu yetu itapata jibu rasmi tukikutana kwenye uwanja wa mazoezi,” alisema.

Wakati Bajaka akipiga hesabu hizo, lakini matumaini ya timu hiyo hayaakisi uhalisia wake, kwani katika mechi 20 ilizocheza, imeshinda moja na kupoteza 19, haijapata sare. Hivyo ina wastani mdogo zaidi wa kukusanya pointi unaowanyima kushinda mechi zote kumi zilizobaki.

Mbali na hilo, timu hiyo inaongoza kwa kuruhusu mabao mengi, ambayo ni 55, huku ikifunga machache zaidi 11.

Katika mechi 10 za mwisho, timu hiyo itavaana na Mlandege, ambao wanatetea ubingwa, huku wakiwa hawapo nafasi nzuri katika msimamo, wakishika nafasi ya saba na pointi 31, wakizidiwa saba na vinara Fufuni.

Mechi zingine ni Polisi vs New Stone Town, New Stone Town vs Chipukizi, New Stone Town vs Junguni, New Stone Town vs KVZ, New Stone Town vs New King, New Stone Town vs KMKM, New Stone Town vs JKU, New Stone Town vs Uhamiaji na New Stone Town vs Muembe Makumbi.