Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amegeuka mbogo baada ya mkazi wa Mpanda mkoani Katavi, Jonathan Kayanda kumweleza hajalipwa fidia licha ya tathimini kufanyika miaka mitatu iliyopita.
Tukio hilo limetokea leo Ijumaa Machi 13, 2026, muda mfupi baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara Kwagira-Karema yenye urefu wa Kilomita 112 mkoani Katavi.
Kayanda anayeishi Kijiji cha Milala, mkoani anadai Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), ilifanya tathimini katika shamba lake ili kupitisha gridi ya Taifa ya umeme kutoka Tabora kwenda Kigoma.
“Imepita miaka mitatu tuliahidiwa, wengine tumepigwa picha lakini hatujajibiwa chochote mheshimiwa utatusaidiaje,” amehoji.
Baada ya maelezo hayo, Dk Mwigulu alimwita meneja wa Tanesco ili kupata taarifa za kina kuhusu kero iliyowasilishwa na Kayanda.
Dk Mwigulu: Meneja tuambie mnalipa lini?
Meneja Tanesco: Mheshimiwa Waziri Mkuu, uthamini na uhakiki ulishafanyika tunasubiri taarifa ya mwisho kwa ajili ya malipo.
Dk Mwigulu: Mnasubiri kutoka wapi?
Meneja Tanesco: Kutoka halmashauri.
Dk Mwigulu: Halmashauri gani?
Meneja Tanesco: Ya Manispaa ya Mpanda.
Dk Mwigulu: Ipo mkoa gani?
Meneja Tanesco: Ipo Mkoa wa Katavi.
Dk Mwigulu: Nyinyi mpo mkoa gani?
Dk Mwigulu: Mnaisubirije hiyo si mnatembea tu kwa miguu…
Meneja Tanesco: Nitaifuatilia Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Baada ya maelezo, Dk Mwigulu alihoji wamechukuliwa mashamba yao na kuzuiwa kuyaendeleza, tathimini imeshafanyika lakini mnasubiriana na mpo mkoa mmoja.
“Nyie si mpo hapa hapa,ndio maana nilizuia mambo ya kuandikiana barua, watu ofisi zinatazamana mnaandikiana barua, mambo ya kishamba,” ameeleza Dk Mwigulu.
Kisha Dk Mwigulu akamwita mkurugenzi wa halmashauri mara mbili, akiwataka kutojificha kwa sababu yupo ziarani katika eneo lao, hata hivyo, hakuwepo katika eneo hilo.
Alimuuliza Ras (Katibu Tawala) watu wapo wapi, akajibiwa kuwa kuna baadhi ya wataalamu wametangulia eneo la mkutano wa hadhara utakaohutubiwa na Dk Mwigulu.
Hata hivyo, Dk Mwigulu aliuhoji uongozi wa mkoa huo, kuwa tathimini hiyo inakamilika lini ili Kayanda apatiwe haki yake. Akajibiwa kuwa suala hilo limechukuliwa na kwenda kufanyiwa kazi.
“Kabla ya sijamaliza ziara mniambie mnalipa lini, nyinyi kwa sababu mpo ofisini hata msipofanya kazi mnalipwa, mnakaa na haki za watu waliotoa mali zao,”
“Mzee alishatoa mali zake na mradi umeshatekelezwa, haki zake hamjampa na tathimini mmeshafanya. Mnaona umri wake unaenda au mnasubiri afariki dunia, kabla ya sijatoka Katavi mniambie mnawalipa lini,” amesema.
Dk Mwigulu ameeleza kuchukizwa na tabia za watendaji wa Serikali kusema changamoto za wananchi zinafanyiwa kazi, lakini hakuna mwanga na kila siku wapo kazini.
Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu amesema watendaji wa halmashauri ya Mpanda wana bahati ya hawakuwepo wakati anasikiliza kero za wananchi kwani angewachangisha ili kumlipa mkazi wa eneo hilo anayewadai.
Nyaraka za Mzee huyo zilikaguliwa na wasaidizi wa Dk Mwigulu na kubaini kuwa ana madai halali ya Sh2 milioni kwa halmashauri ya Wilaya ya Mpanda.
“Wilaya inadaiwa Sh2 milioni, mkurugenzi na mkuu wa wilaya wako wapi? Wametangulia kwenye mkutano… hawa wana bahati wametanguliwa ningewaambia wamlipe hapahapa.
“Mkuu wa Mkoa (Mwanamvua Mrindoko) waambie watu ninapokuja kwenye mkutano wawe wameshaipata hiyo Sh2 milioni. Waambie tukifika kwenye mkutano wawe wameshaipata Sh2 milioni,” amesema.
Awali mkazi huyo (mzee) ambaye hakujitambulisha jina aliyekuwa ameshika nyaraka zinazoonyesha kiwango cha fedha anachodai, alimwambia Dk Mwigulu kuwa anazungushwa kuhusu malipo yake.
