WAWAKILISHI wa mshambuliaji wa Namungo FC, Mkongomani, Fabrice Ngoy wamepokea mkataba mpya kutoka kwa uongozi wa kikosi hicho cha Wauaji wa Kusini ambao wanataka wakamilishe dili hilo mapema, kabla ya msimu huu wa 2025-2026, haujaisha.
Mshambuliaji huyo aliyeitumikia Namungo kwa misimu mitatu, mkataba wake wa sasa unafikia ukomo mwishoni mwa msimu huu wa 2025-2026, ambapo uongozi wa kikosi hicho cha ‘Wauaji wa Kusini’, unafanya haraka kukamilisha dili hilo mapema zaidi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Namungo, Ally Suleiman, alisema kabla ya kukukutana na wawakilishi wa nyota huyo, ila walianza mazungumzo ya awali na mchezaji mwenyewe, ambapo tayari walimwekea mkataba wa miaka miwili zaidi kikosini.
“Kuna miezi mitatu mbeleni imebaki kabla ya mkataba wake kuisha, tunahitaji kufanikisha dili hilo mapema, ili kuondokana na presha mwishoni mwa msimu huu, Ngoy ni mchezaji tunayependa kuendelea naye tena katika timu yetu,” alisema Suleiman.
Kwa upande wa Ngoy, alisema suala hilo amewaachia wasimamizi wake kwa ajili ya mazungumzo hayo, ingawa kwa sasa malengo yake makubwa ni kuendelea kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali, kisha mwisho wa msimu ndipo atajua hatima yake.
Nyota huyo ameaminiwa na kocha, Juma Mgunda, licha ya uwepo wa washambuliaji wengine wakiongozwa na mkongomani mwenzake, Heritier Makambo aliyetoka TRA United zamani Tabora United na Abdulaziz Shahame ‘Haaland’, aliyetokea kikosi cha TMA FC.
Ngoy alijiunga na Namungo msimu wa 2023-2024, akitoka Kitayosce iliyobadilishwa jina na kuitwa Tabora United na sasa TRA United, baada ya kuifungia mabao 15 ikiwa Ligi ya Championship, nyuma ya kinara, Edward Songo wa JKT Tanzania aliyefunga 18.
Mshambuliaji huyo alitua hapa nchini kwa mara ya kwanza msimu wa 2022-2023, akitokea Real Nakonde FC ya Zambia na msimu wa 2023-2024, alifunga bao moja tu, huku 2024-2025, akifunga mawili na sasa msimu wa 2025-2026, tayari amefunga manane.