Mradi wa umeme jua Shinyanga waingizwa gridi ya taifa

Shinyanga. Awamu ya kwanza ya mradi wa umeme jua katika Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imekamilika kwa asilimia 95.5 ikiwa sehemu ya mpango wa kupunguza changamoto ya umeme katika mkoa huo na mingine ya Kanda ya Kiwa.

Hayo yameelezwa na leo Machi 13, 2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la umeme Tanzania (Tanesco) Lazaro Twange wakati wa ziara ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, ilimshirikisha pia Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi.

Amesema kuwa mradi huo utasaidia katika shughuli za uchimbaji wa madini, viwanda vya pamba pamoja na reli ya kisasa (SGR).

Shamba la panel 82,000 za umeme jua lilopo wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga. Picha na Hellen Mdinda.

“Awamu ya kwanza ya mradi huu unazalisha megawati 50 ambayo imekamilika kwa asilimia 95.5 na wiki mbili zilizopita umeme wake uliingizwa katika Gridi ya Taifa.

“Uzalishaji huu utasaidia katika uendeshaji wa shughuli za kiuchumi kama za viwandani hasa katika zao la pamba, uchimbaji wa madini pamoja na usafiri wa SGR katika mikoa ya Kanda ya Miwa,” amesema Twange.

Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo, Subira Mgalu kwa niaba ya wajumbe ameeleza kufurahishwa na utekelezaji wa mradi huo ambapo amesema thamani ya fedha zilzotolewa ni sawa na utekelezaji ulifanyika katika mradi huo

“Hongereni sana kwa mkandarasi utekelezaji wa mradi huu mkubwa, tumeona thamani ya fedha zilizotolewa, Sh118 bilioni kwa awamu ya kwanza, zinaendana na utekelezaji uliofanyika hapa hadi kufikia hatua ya kuingizwa katika Gridi ya Taifa” amesema Mgalu.

Mitambo ya umeme jua uliopo wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga. Picha na Hellen Mdinda.

Kwa upande wake Meneja mradi wa umeme jua, Emmanuel Anderson ameeleza kuwa katika mradi huo kuna paneli zaidi ya 80,000 ambazo katika uzalishaji wake wa megawati 50 zinaweza kudumu si chini ya miaka 25 kuanzia pale mradi utakapo anza kutumika.

“Awamu ya pili ya mradi ya uzalishaji wa megawati 100 imekaribia kuanza, ili kukamilisha mradi mzima wa umeme jua,” amesema Anderson.

Mradi mzima unatarajia kugharimu shilingi bilioni 323 kwa awamu zote mbili.

Mradi huo ulioanza rasmi Desemba 2023 na ulitarajiwa kukamilika mapema mwaka huu.