Dk Mwigulu: Tutachukua hatua kali makandarasi wasiolipa wafanyakazi

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, ameagiza Wizara ya Maji kuwaandikia barua makandarasi wote wanaotekeleza miradi ya maji kuwalipa kwa wakati mafundi, vibarua na wafanyakazi wengine mara tu wanapopokea fedha kutoka Serikalini.

Agizo hilo limetolewa leo Ijumaa Machi 13, 2026 baada ya mfanyakazi wa mradi wa maji wa miji 28 katika eneo la Shanwe, Mpanda mkoani Katavi, Abubakari Chacha, kulalamikia kucheleweshwa kwa mishahara na upungufu wa vitendea kazi.

“Mafundi tunacheleweshewa mishahara yetu na pia vitendea kazi vinakuwa vichache, vikimalizika vinachelewa kuletwa,” amesema Chacha.

Akijibu malalamiko hayo, Dk Mwigulu amesema si sahihi kwa makandarasi kuchelewesha malipo wakati Serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya miradi.

“Hili halikubaliki. Kila fedha inayolipwa kwenye mradi, mafundi, vibarua na wote wanaofanya kazi walipwe,” amesema.

Ameonya kuwa mkandarasi anayemaliza mradi huku akiwa anadaiwa na wafanyakazi wakati tayari amelipwa na Serikali, anakuwa anawaibia wananchi.

Kuhusu ucheleweshaji wa vitendea kazi, Waziri Mkuu ameagiza suala hilo kushughulikiwa ili malighafi zifike kwa wakati kwenye mradi huo ambao umefikia asilimia 55.2 ya utekelezaji.

Awali, Naibu Waziri wa Maji, Kundo Mathew, alikiri kuwepo kwa changamoto ya ucheleweshaji wa mishahara na kusema tayari walielekeza wafanyakazi walipwe kulingana na kima cha chini cha Serikali.

Kuhusu ucheleweshaji wa malighafi, amesema unatokana na uzalishaji mdogo ukilinganishwa na mahitaji makubwa katika maeneo mbalimbali, akitolea mfano saruji inayohitajika kwa wakati mmoja katika maeneo kama Mugumu, Chato na Kiomboi.

Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Katavi kuchunguza mwenendo wa upokeaji na usambazaji wa dawa katika hospitali za mkoa huo.

Ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Majalila, wilayani Tanganyika.

Amesema Serikali imekuwa ikipeleka fedha nyingi kwa ajili ya dawa huku takwimu zikionyesha utoshelevu wa zaidi ya asilimia 90, lakini wagonjwa wanapofika hospitali wanaambiwa wakazinunue kwenye maduka binafsi.

“Hii michezo haikubaliki. Serikali inaleta zaidi ya Sh1 bilioni na tunaambiwa dawa zinatosha kwa zaidi ya asilimia 90, lakini mgonjwa anaambiwa akanunue nje,” amesema.

Kwa mujibu wa Dk Mwigulu, Mkoa wa Katavi umepokea Sh1.062 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vitendanishi katika mwaka wa fedha, ambapo zaidi ya Sh300 milioni zimepelekwa hospitali ya wilaya, Sh294 milioni vituo vya afya na zaidi ya Sh462 milioni zahanati.

Amesema uchunguzi unatakiwa kuangalia mtiririko wa fedha, dawa zinazonunuliwa na matumizi yake ili kubaini kama kuna watu wanapeleka dawa katika maduka binafsi kwa masilahi yao.

“Haiwezekani kuwe na takwimu za utoshelevu wa dawa lakini wagonjwa wanaambiwa wakazinunue nje,” amesema.

Dk Mwigulu pia ameagiza Takukuru kuchunguza matumizi ya fedha katika miradi ya maendeleo ili kuhakikisha kuna thamani ya fedha na kuzuia ubadhirifu.

“Hatutavumilia tabia za kugawana fedha za miradi. Nataka uchunguzi wa kila fedha iliyopokelewa na matumizi yake,” amesema.

Katika mkutano huo, mkazi wa Mpanda, Elias Mayala alilalamikia barabara ya Katuma–Sigwesa kukatika kwa miezi miwili na kusababisha adha kwa wananchi.

Uongozi wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura ) Mkoa wa Katavi ulisema barabara hiyo ipo kwenye bajeti na wanasubiri kibali cha kuanza matengenezo.

Akijibu hilo, Dk Mwigulu amesema tayari ameshatoa kibali na kuagiza matengenezo yaanze mara moja.