Dar es Salaam. Upande wa Jamhuri katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili washtakiwa tisa wanaodaiwa kuongoza genge la uhalifu na kujipatia zaidi ya Sh5.7 bilioni kwa udanganyifu mali ya Equity Bank Tanzania Limited, umedai bado unaendelea na majadiliano ya kumaliza kesi hiyo.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 20 yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu, wizi na utakatishaji fedha.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Jasmine Elphas, aliyekuwa ofisa wa benki hiyo makao makuu, mfanyabiashara, Fredrick Ogenga, pamoja na Lilian Koka, aliyekuwa ofisa wa benki hiyo.
Wengine ni Halifa Maina, Kaizilege Mohamed, Daudi Fata, Mrisho Mrisho, Neema Paul na Jefferson Ogenga, wote ni wafanyabiashara.
Leo Ijumaa Machi 13, 2026 Wakili wa Serikali Titus Aron alitoa taarifa hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.
“Shauri limeitwa kwa ajili ya kutajwa na bado upande wa Jamhuri unaendelea na majadiliano na washtakiwa kwa ajili ya kumaliza kesi, hivyo tunaomba mahakama ipange tarehe nyingine tuone majadiliano yamefikia hatua gani,” alidai Wakili Aron.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mhini aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 18, 2026 kwa ajili ya kutajwa tena. Washtakiwa waliendelea kubaki rumande kutokana na shtaka la utakatishaji fedha kutokuwa na dhamana.
Katika kesi ya msingi ya uhujumu uchumi namba 18447 ya mwaka 2025, washtakiwa wanadaiwa kuwa kati ya Agosti 30, 2024 na Juni 28, 2025 katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam waliendesha genge la uhalifu na kujipatia zaidi ya Sh5.7 bilioni mali ya benki hiyo.
Inadaiwa kuwa katika kipindi hicho Jasmine na Ogenga, wakiwa katika makao makuu ya benki ya Equity Ilala, waliiba Sh3.6 bilioni kutoka akaunti ya clearing and settlement iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Pia Caroline anadaiwa kuiba Sh728 milioni, huku Lilian akidaiwa kuiba Sh26 milioni katika makao makuu ya benki hiyo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Maina anadaiwa kuiba Sh101 milioni, Mohamed Sh57 milioni, Fata, Sh758 milioni, Mrisho, Sh211 milioni na Neema, Sh32 milioni katika vipindi tofauti kati ya mwaka 2024 na 2025.
Aidha, washtakiwa hao wanakabiliwa pia na mashtaka 10 ya utakatishaji fedha zinazodaiwa kupatikana kutokana na wizi huo.
