Global Publishers
March 13, 2026
0 Comments
WAZIRI wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth ameeleza sababu ya kwa nini jeshi la Marekani bado halijaanza kusindikiza meli zinazopita katika Strait of Hormuz, licha ya mvutano mkubwa wa kijeshi katika eneo hilo.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo Machi 13, 2026 Pentagon, Hegseth alikabiliwa na swali kutoka kwa mwandishi aliyedai kuwa Marekani ina ubora wa kijeshi wa anga na baharini dhidi ya Iran, lakini bado haijachukua hatua ya kusindikiza meli katika njia hiyo muhimu ya biashara ya mafuta duniani.
Akijibu swali hilo, Hegseth alisema Marekani ilikuwa tayari imepanga na kutambua hatari hiyo, lakini hatua za kijeshi lazima zichukuliwe kwa mpangilio unaofaa.
“Tulipanga hilo, tunalitambua, Lakini tunataka kufanya mambo kwa hatua na kwa njia ambayo inaleta mantiki zaidi, huku tukihakikisha tunatuma ujumbe sahihi kwa dunia,” alisema.

Mlango wa Hormuz ni mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa mafuta duniani, ambapo takribani asilimia 20 ya mafuta ya dunia hupitia katika njia hiyo kila siku. Katika wiki za hivi karibuni, meli kadhaa zimeripotiwa kushambuliwa katika eneo hilo huku mvutano kati ya Iran na mataifa ya Magharibi ukiendelea kuongezeka.
Zaidi ya meli 3,000 hupita katika mlango huo kila mwezi, zikiwemo meli kubwa za kubeba mafuta kutoka nchi za Mashariki ya Kati kwenda Ulaya, Asia na maeneo mengine ya dunia.
Mlango wa Hormuz hutumiwa sana na wazalishaji wakubwa wa mafuta katika eneo la Mashariki ya Kati kama Saudi Arabia, Iraq, Kuwait, Qatar na United Arab Emirates kusafirisha mafuta na gesi kwenda masoko ya kimataifa.