Tanzania yalipa CAF zaidi ya Sh80 Bilioni uwenyeji AFCON 2027

Serikali ya Tanzania imelipa Dola Milioni 32 (zaidi ya Sh80 Bilioni) kwa Confederation of African Football (CAF) kama sehemu ya masharti ya kuwa mwenyeji wa mashindano ya Africa Cup of Nations 2027 (AFCON 2027).

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, alisema malipo hayo ni ada ya lazima inayotakiwa kulipwa na nchi zilizochaguliwa kuandaa mashindano hayo makubwa ya soka barani Afrika.

“Kwa kawaida, kila nchi inayokuwa mwenyeji wa AFCON inalazimika kulipa kiasi fulani cha fedha kwa CAF kama sehemu ya maandalizi ya mashindano hayo,” alisema Makonda.

Aliongeza kuwa Serikali ya Tanzania tayari imetekeleza kikamilifu malipo yote yanayotakiwa na CAF ili kuruhusiwa rasmi kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.

“Tayari tumelipa fedha zote zinazohitajika kwa CAF ili Tanzania iweze kuwa mwenyeji rasmi wa AFCON. Tunazungumzia takribani dola milioni 32 za Marekani,” alifafanua.

Makonda alitoa kauli hiyo Machi 12, 2026 alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo wakati walipokagua maendeleo ya ujenzi wa Arusha International Football Stadium jijini Arusha.

Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji mwenza wa mashindano ya AFCON 2027 pamoja na Kenya na Uganda kupitia zabuni ya pamoja inayojulikana kama Pamoja Bid.