Dar es Salaam. Aliyekuwa Gavana wa nne wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk Idrisa Rashid, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 78.
Dk Rashid aliyezaliwa mwaka 1948, wilayani Mbulu katika Mkoa wa Manyara, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Ijumaa ya Machi 13, 2026, baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Taarifa za kifo chake, zimethibitishwa na mwanawe, Mohamed Idrisa, alipozungumza na Mwananchi.
“Ni kweli amefariki. Baba alikuwa anaugua saratani na amefariki katika Hospitali ya Shifaa, alikokuwa anapatiwa matibabu,” amesema.
Mohamed, amesema mazishi ya Dk Rashid ambaye pia aliwahi kuwa mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), yatafanyika kesho Jumamosi Machi 14, 2026) mkoani Manyara.
“Hapa tunafanya utaratibu wa kwenda Msikiti wa Maamur kwa ajili ya taratibu, kisha tunasafiri kwenda Mbulu mkoani Manyara na huko ndiko tutakapomzika kesho,” amesema.
Dk Idris Rashid alizaliwa mwaka 1948, Mbulu mkoani Manyara. Ni mmoja wa wataalamu wa masuala ya fedha na uongozi wa mashirika aliyewahi kushika nafasi muhimu katika taasisi mbalimbali nchini Tanzania.
Alijulikana zaidi kwa mchango wake katika sekta ya benki, mawasiliano na nishati, ambako aliwahi kuongoza taasisi kubwa za umma na binafsi.
Dk Idris Rashid alipata elimu ya juu katika masuala ya uchumi na fedha, jambo lililomwezesha kujijengea taaluma thabiti katika sekta ya fedha.
Baada ya masomo yake, alianza kufanya kazi katika sekta ya benki alikojipatia uzoefu wa usimamizi wa fedha na uongozi wa taasisi za kifedha.
Katika safari yake ya kikazi, Dk Rashid aliwahi kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mwaka 1993 hadi 1998, hatua iliyomjengea heshima kama mtaalamu wa sera za fedha na usimamizi wa taasisi za kifedha, kabla ya kuwa mkurugenzi mtendaji wa Benki ya Akiba.
Baadaye alifanya kazi katika sekta ya mawasiliano akiwa katika uongozi wa kampuni ya simu ya mkononi ya Vodacom Tanzania, alikohusika katika maendeleo ya sekta ya mawasiliano iliyokuwa ikikua kwa kasi nchini.
Mwaka 2006 aliteuliwa kuwa mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Katika nafasi hiyo, alisimamia shughuli za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini kwa lengo la kuboresha huduma hiyo kwa wananchi na kukuza uchumi wa taifa.
Katika kipindi cha uongozi wake Tanesco, alihusishwa pia na mijadala mbalimbali ya sera na maamuzi ya kiutendaji katika sekta ya nishati, jambo lililomfanya kuwa mmoja wa viongozi waliokuwa wakifuatiliwa kwa karibu katika mijadala.
