REA HAINA BAYA NA MTU SIKU HIZI KIJIJINI KAMA MJINI TU…WANANCHI WANAINJOI SANA

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

LEO naomba unipe nafasi kidogo tuzungumze kuhusu Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambayo ni taasisi ya serikali ya Tanzania iliyoanzishwa chini ya Wizara ya Nishati.

Jukumu namba moja la REA ni kusimamia na kurahisisha upatikanaji wa nishati bora na ya uhakika (hasa umeme) katika maeneo ya vijijini ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Nimeanza na kuilezea REA kwa kifupi ili unaposoma nilichoandika basi uelewe nazungumza kuhusu nini. Ndio maana najua wapo ambao hawajui REA ni nini na inafanya kazi gani nchini kwetu Tanzania.

Ngoja nikueleze kwa lugha rahisi zaidi iko hivi ukiona kijijini umeme unawaka katika nyumba ya bibi au babu,baba mkubwa au baba mdogo ,Shangazi au Mjomba kule kijijini basi ujue waliofikisha na kusamabaza umeme huo ni REA.

REA kila wanapolala na kuamka wao wanafikiria ni kwa namna gani umeme utafika katika vijiji vyetu,iwe kijiji cha kule Mpitimbi,iwe kijiii cha Madunda kule Ludewa au kule kwa Mpiga Miti wilayani Liwale.

Yaani ukiona umeme kijijini kwenu ujue hao ndio REA sasa .Hata ukiwa kule Oldonyosambo na umeme ukawa unawaka hao ni REA .Nadhani tumeelewa.Usiichukulie poa kabisa.Nakwambia ukweli.Wee cheka tu kama hamnazo.

Ikumbuwe nchini Tanzania tunavyo vijiji 12,364 na Vitongoji 64539na kote huko REA wapo kazini kwa ajili ya kufikisha nishati bora ya umeme na kwa kazi nzuri ambayo wameendelea kuifanya vijiji vyote vina umeme na kazi sasa inaendelea katika vitongoji.

Hata hivyo naomba iweleke katika hivyo vitongoji ambavyo nimevitaja hapo juu tayari vingine vina umeme, lengo ni kuwezesha wananchi waliko huko wanapata nishati ya umeme kama walioko mijini. Ukweli REA wameendelea kubadilisha maisha ya wananchi wa vijijini. Huo ndio ukweli maana kijiji chochote unachotaka kwenda umeme upo.

Zile mechi zetu za Simba na Yanga,Mtibwa na Kagera Sugar au Singida BS na Azam unaziona hata ukiwa kule Kijiji Kilumbi au Mwamalugu kule wilayani Sikongone mkoani Tabora utaziona mechi vizuri ukiwa katika Kibanda umiza kwa kuwa REA wapo kazini .

Unaposikia vijiji vyote vina umeme basi kichwani kwako ujue kuna mabilioni ya fedha yametumika. Serikali inatumia fedha nyingi kuhakikisha wananchi wanapata umeme. Nitoe mfano halisi kujenga kilometa moja ya umeme wa Msongo wa kati(33kv) inagharimu zaidi ya Sh.milioni 25.

Ukiona laini ya umeme yenye urefu wa kilometa 100 ujue gharama iliyotumika hapo si chini ya Sh.bilioni 2.5. Na kiasi hicho cha fedha ni katika maeneo ambayo yanafika kwa urahisi katika kufikisha miundombinu ya umeme wa REA.Maeneo mengine gharama ni zaidi ya hiyo.

Kwa mfano hivi karibu nimepata nafasi ya kutembelea miradi ya REA katika Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe.Ziara hiyo ilihusisha Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)ambalo Mwenyekiti wake ni Deodatus Balile.

Tukiwa katika ziara hiyo tumeona ugumu ambao REA wanaupata kufikisha nguzo katika vijiji na vitongoji vya Wilaya hiyo.Pale Madunda kuna milima mirefu sana na mabonde lakini REA bila kujali ugumu wa Mazingira hayo wamefikisha nguzo katika vitongoji sıta vya Kitewele,Kimata , Kigulu,Chanjale Lumbira na Nkanda.

Msimamizi wa miradi ya REA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mhandisi Danstan Kalugira anaeleza namna ambavyo REA imelazimika kuwatumia SUMA JK kusimika nguzo kwa umbali kilometa 36.69 za msongo wa kati na za msongo wa chini ni kilometa 15.06.

Katika mradi huo zitatumika mashine umba sita. Nimesema mashine unauliza mashine ndio nini?Acha mambo yako mashine umba kwa lugha tuliyozoea huku mtaani tunaita Transifoma.

Na idadi ya wateja watakaonufaika wa mwanzo ni 160, hivyo mradi ukikamilika wananchi changamkieni umeme wa REA.Nikwambie ukweli acha kulaza damu, kwani wee hutaki kuangalia vipindi vya Azam TV hasa Chanel ya Sinema? Kwani hupendi kuangalia taarifa ya habari ya Alasiri,Aridhio au habari ya saa mbili usiku?Changamka wewe 🤣🤣

Wakati wa ziara hiyo pia tumeona namna ambavyo REA imewakaribisha wawekezaji na mashirika binafsi kuwekeza katika kuzalisha umeme vijijini kupitia vyanzo vya maji. Kwa Wilaya ya Makete tumeona mradi wa kuzalisha umeme wa Ijangala uliopo wilayani Makete mkoani Njombe.

Mradi huo unazalisha megawati 360 na utaunganishwa katika gridi ya Taifa.Mradi huo unasimamiwa na Kanisa la Kiinjili la Kulutheri Tanzania(KKKT)Kusini Kati. REA imetoa fedha ya ruzuku Sh.bilioni 1.63 kuufanikisha mradi huo.

Lakini kupitia mpango wa upanuzi wa umeme vijijini Tanzania (TREEP) mradi huo umepata Mkopo nafuu wa Sh. Milioni 922 kusaidia shughuli mbalimbali za utekelezaji wake.

Kwa Wilaya ya Njombe Kudewa Jukwaa la Wahariri pia limeona mradi wa kuzalisha umeme wa Lupali wenye uwezo wa kuzalisha megawati 317 ambapo REA imetoa fedha ya ruzuku Sh.bilioni 5.3 .Ni mradi unatekelezwa na Shirika la Benedictine Sisters of St.Gertrude Convint Imilawaha .

Ukifika katika mradi huo utaona REA ilivyokuwa siriazi katika kusambaza nishati ya umeme vijijini na kwenye vitongoji .Lakufurahisha zaidi wenye dhamira ya kweli wakala huo upo tayari kushirikiana nao kwa kila hatua.REA bwana wala hawana baya mtu.

Kaimu Meneja Usaidizi wa kifundi kwa waendelezaji kutoka REA Mhandisi Emmmanuel Yassaya anatumia nafasi hiyo kulieza Jukwaa la Wahariri kwamba imefungua milango kwa sekta binafsi kuwekeza katika kuzalisha nishati hiyo.

Hata hivyo kutokana na kazi kubwa na nzuri ambayo imefanywa na REA, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania Deodatus Balile anatoa pongezi kwa REA kwa jinsi ilivyodhamiria kupeleka umeme vijijini.

Balile anasema hapo miaka ya nyuma kidogo ukiwa unasafiri moja ya alama ya kujua umefika mjini ni uwepo wa taa lakini sasa ni tofauti kwani vijiii vyote vina umeme .Ukienda kwa staili ya zamani utapotea.Usicheke mtu wangu.

Na hapo sijazungumzia ule mradi wa kusambaza gesi asilia majumbani ili wananchi wapike kwa nishati safi.Ni mradi ambao umetekelezwa katika mikoa ya Lindi na Pwani na tayari watu 1000 wanatumia nishati safi ya kupikia.

Nenda Kisevule Centre pale wilayani Mkurunga kisha muulizie dada Mariam Rashid atakwambia anavyoinjoi kupika kwa gesi aliyofungiwa bure na Serikali kupitia REA.Ni mradi uliogharimu Sh.bilioni sita.

Pamoja na hayo yooooote niliyoeleza jambo la msingi la kuzingatia kwa wananchi ni vema wakaheshimu na kutunza miundombinu ya REA kwani fedha nyingi zimetumika.

Kumekuwa na tabia kuharibu miundombinu aidha kwa kuiba waya au kuchoma nguzo .Wapo wengine wanaiba transfoma ili kwenda kuuza kama Skrepa.Tuache tabia hiyo.

Kuwa mzalendo kwa kulinda miundombinu ya REA na kila mmoja wetu akawa mlinzi kwa mwenzake.Hata hivyo wakati wa Mjini unasema REA wa nini walioko katika vitongoji wanasema REA itakuja lini.?

Nikutakie mfungo mwema wa Ramadhani, mfungo mwema wa Kwaresma.Halafu nimeshanunua Abaya la wifi yenu kwa ajili ya Sikukuu ya Eid wakati naivutia kasi Pasaka. Alamsiki swahiba.

Ni mimi 0713833822/0762451570.