Rais Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Simon Nyakoro Sirro, kufuatia vifo vilivyotokana na ajali mbili tofauti zilizotokea asubuhi ya Machi 13, 2026 katika Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu, ajali ya kwanza ilihusisha boti iliyokuwa imewabeba watumishi wa afya waliokuwa wakisafiri kutoka Kigoma kuelekea Kijiji cha Kagunga, mpakani mwa Tanzania na Burundi, kwa ajili ya kutoa huduma za afya katika vijiji vya mwambao wa ziwa hilo.
Boti hiyo ilipinduka na kuzama baada ya kukumbwa na upepo mkali, na kusababisha vifo vya watumishi saba wa afya, wakiwemo wanaume wanne na wanawake watatu.
Aidha, watu 14 walijeruhiwa na wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Maweni, huku juhudi za kuwatafuta watu wawili ambao bado hawajapatikana zikiendelea kufanywa na vikosi vya uokoaji.
Katika tukio la pili, wavuvi watatu waliokuwa wakivua katika Ziwa Tanganyika walipigwa na radi, na kusababisha kifo cha mvuvi mmoja huku wawili wakijeruhiwa.
Rais Dkt. Samia amesema amepokea kwa masikitiko taarifa za ajali hizo na kuziombea roho za marehemu zipumzike kwa amani.
Pia ametoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wa waliopoteza maisha, huku akiwatakia majeruhi wote uponyaji wa haraka.
Aidha, amewataka wananchi, hususan wanaotumia vyombo vya usafiri majini na wanaojihusisha na shughuli za uvuvi, kuzingatia tahadhari dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo upepo mkali na radi ili kuepuka ajali zinazoweza kuzuilika.
🔴 Tufuatilie kupitia YouTube ya Global TV, like, comment ili kuendelea kuhabarika kila siku kwa habari mbalimbali zenye ukweli na uhakika.
