Dar es Salaam. Uhaba wa madawati waibuliwa Temeke, wanafunzi zaidi ya 2,500 wakosa sehemu ya kukaa.
Diwani wa Kata ya Makangarawe, Temeke jijini Dar es Salaam, Fadhil Mboga, amefanya ziara katika Shule za Msingi Jitihada na Yombo Dovya kujionea hali ya miundombinu na maendeleo ya kitaaluma katika shule hizo.
Ziara hiyo iliyofanyika leo Ijumaa Machi 13, 2026 imelenga kutathmini changamoto zinazoikabili sekta ya elimu katika kata hiyo, ikiwemo uhaba wa madawati, uchakavu wa majengo na upungufu wa miundombinu muhimu kwa wanafunzi na walimu.
Katika ziara hiyo, Mwananchi ilishuhudia baadhi ya wanafunzi wakikaa chini darasani kutokana na uhaba wa madawati. Kwa mujibu wa takwimu za shule hizo mbili zenye zaidi ya wanafunzi 4,000 kwa pamoja, upungufu wa madawati umefikia 836.
Kwa wastani wa wanafunzi watatu kwa dawati, hali hiyo inaacha zaidi ya wanafunzi 2,500 bila sehemu ya kukaa madarasani.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Jitihada, Jubilate Kapesa, amesema shule hiyo inahitaji madawati 939 lakini yaliyopo ni 380 pekee, hivyo kuwa na upungufu wa madawati 559.
Mbali na hilo, amesema shule pia inakabiliwa na uchakavu wa miundombinu ya vyoo kutokana na kutumika kwa muda mrefu.
Kwa upande wa Shule ya Msingi Yombo Dovya, Mwalimu Mkuu Salum Gawaza amesema shule hiyo yenye wanafunzi 1,911 na walimu 38 imekuwa na changamoto ya uhaba wa madarasa, madawati na miundombinu ya vyoo.
Amesema shule hiyo inahitaji madarasa 43 lakini yaliyopo ni 24 pekee, hali inayosababisha darasa moja kuwa na wanafunzi kati ya 80 hadi 100.
Kwa upande wa vyoo, amesema shule inahitaji matundu 86 lakini yaliyopo ni 38 tu, huku kwa walimu kukiwa na matundu sita pekee.
“Kwa madawati tunahitaji 637 lakini yaliyopo ni 360, hivyo kuna upungufu wa 277 ndiyo maana baadhi ya wanafunzi wanakaa chini,” amesema.
Ameongeza kuwa walimu wanahitaji meza na viti 46 lakini vilivyopo ni 20 pekee. Pia shule inahitaji projesta mbili na kompyuta angalau 40 ili kurahisisha ufundishaji, hususan wa masomo ya sayansi.
Hata hivyo amesema licha ya changamoto hizo, shule imeendelea kufanya vizuri kitaaluma, ikifaulisha asilimia 98 mwaka 2022, asilimia 95 mwaka 2023, asilimia 97 mwaka 2024 na asilimia 98 mwaka 2025.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mboga amesema ipo haja ya wadau kushirikiana kutafuta suluhisho la haraka la tatizo la madawati.
Amesema Mbunge wa Temeke, Mariam Kisangi, ameahidi kutoa madawati 50 ambapo 25 yatapelekwa Shule ya Msingi Jitihada na 25 Shule ya Msingi Yombo Dovya.
Mboga pia amesema halmashauri ina mkakati wa muda mrefu wa kuboresha miundombinu ya elimu ikiwemo kujenga shule za ghorofa na kutengeneza samani za shule.
Aidha, ameitisha kikao cha dharura kesho Jumamosi Machi 14, 2026 kitakachowakutanisha wazazi, walimu na viongozi wa serikali za mitaa kujadili namna ya kutatua changamoto hizo haraka.
Wananchi walalamikia ukosefu wa shule ya sekondari
Mbali na changamoto za shule za msingi, wakazi wa Makangarawe pia wamelalamikia kukosekana kwa shule ya sekondari katika kata hiyo.
Katibu wa CCM kata ya Makangarawe, Julius Mkada, amesema wanafunzi wengi hulazimika kusoma shule za mbali, hali inayoongeza gharama kwa wazazi.
Mzazi na mkazi wa eneo hilo, Safia Mohammed, amesema kukosekana kwa shule ya sekondari karibu kumekuwa kukisababisha wazazi kutumia gharama kubwa za usafiri wa daladala kwa watoto wao.
Hata hivyo, wakazi hao wameeleza matumaini yao kutokana na ujenzi wa shule ya sekondari ya ghorofa unaoendelea katika kata hiyo, unaotarajiwa kukamilika mwaka 2028.
