Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imeidhinisha uhalali wa Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, baada ya kutupilia mbali shauri lililokuwa likipinga uhalali wake.
Uamuzi huo umetolewa leo Ijumaa, Machi 13, 2026 na Jaji Awamu Mbagwa, aliyesikiliza shauri hilo lililokuwa limefunguliwa na wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu, Rosemary Mwakitwange na mawakili wawili Edward Heche na Deogratius Mahinyila.
Jaji Mbagwa katika uamuzi huo amekataa hoja za madai ya wadai akisema kuwa hayakuwa na msingi wa kisheria bali yalikuwa ni ya hisia na kwamba Rais aliunda tume hiyo na kuteua wajumbe wake kwa mujibu wa Sheria ya Tume za Uchunguzi.
“Hoja za madai ya wadai hazina msingi wa kisheria bali walitoa madai ya hisia. Kwa sababu hizo shauri hili linatupiliwa mbali,” amesema Jaji Mbagwa baada ya kurejea na kuchambua hoja za pande zote pamoja na masharti ya Sheria ya Tume za Uchunguzi.
Hata hivyo wakizungumza baada ya uamuzi huo, wadai, hao Mwakitwange, Heche na Mahinyila wamesema kuwa hawajaridhishwa na uamuzi huo kwa kuwa Mahakama haijajibu hoja zao zote, imejibu chache hivyo watasonga mbele kutafuta haki.
“Kwa hiyo tumezungumza na wateja wetu wameshaturuhusu kukata rufaa,” amesema Wakili Hekima Mwasipu, mmoja wa mawakili wa wadai.
Kwa upande wake wakili wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), ambacho pia kilikuwa mmoja wa wadaiwa katika kesi hiyo, Ferdnand Makore, ambacho pia kiliunga mkono madai ya wadai, amesema hata wao hawajaridhika na uamuzi huo akieleza kuna hoja mbalimbali walizoziibua hazikujibiwa kabisa.
“Kwa hiyo na sisi kama TLS tutakwenda kuzungumza na Baraza la Uongozi, kama litakubali tutaunga mkono rufaa ambayo wadai wataikata,” amesema wakili Makore.
Kwa upande wake, Mwakitwange amesema waliwasilisha hoja tano kupinga tume hiyo ambazo kupitia kwa mawakili wao waliona zinawakilisha uzito wa shauri hilo, lakini Mahakama haijazijibu zote badala yake imejibu mbili tu.
Heche kwa upande wake amesema kutokana na uzito wa shauri hilo na linahusu masilahi ya Watanzania na Mahakama haijajibu hoja zao kwa kina wameshakubaliana watakata rufaa.
Naye Mahinyila amesema pamoja na hatua nyingine wanazokusudia kuzichukua na kwa kuwa Mahakama imekataa hoja zao sasa wanasubiri hiyo tume ije iwaeleze Watanzania kuwa ni nani aliyefanya mauaji na kwa amri ya nani.
“Tunaamini tume hii kwa jinsi ilivyoundwa na kwa aina ya wajumbe wake haiwezi kuja kusema hayo. Lakini kama tume itafanya kazi ambazo tuliona kuwa haiwezi kuzifanya basi sisi tutakuwa waungwana tutaiomba radhi,” amesema Mahinyila na kusisitiza kuwa hawatarajii kabisa kupata uhalisia wa matukio hayo kutoka kwa tume hiyo.
Tume hiyo inayoongozwa Jaji Mkuu wa Tanzania mstaafu, Mohamed Chande iliundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Novemba 18, 2025 na akaizindua Novemba 20, 2025, kufuatia matukio ya siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025 na baada ya uchaguzi.
Matukio hayo ni vurugu zilizosababisha uharibifu wa miundombinu na mali za umma na watu binafsi pamoja na vifo na majeruhi, kufuatia maandamano ya kupinga uchaguzi huo katika majiji na miji mbalimbali nchini.
Mbali na Jaji Chade (mwenyekiti) wajumbe wa tume hiyo ni pamoja na Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue; Radhia Msuya, Balozi Paul Meela na Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu (IGP), Said Mwema.
Wengine ni Balozi David Kapya, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu mstaafu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Africa (SADC) na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa mstaafu, Stergomena Tax na Chama cha Sheria Tanganyika (TLS).
Hata hivyo, Mwakitwange, Heche na Mahinyila walifungua shauri hilo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wajumbe wa tume hiyo kwa majina yao, wakipinga uhalali wake.
Pia waliiunganisha TLS, kwa madai kuwa imeundwa kwa Sheria ya Bunge, pamoja na mambo mengine kukuza utawala wa sheria, kulinda na kusaidia umma kupata haki na huduma za kisheria katika masuala yote yanayohusu sheria.
Katika shauri hilo la maombi ya mapitio ya mahakama namba 32537/ 20267 waliiomba mahakama hiyo itoe amri za kufuta na zuio la uamuzi wa Rais wa uteuzi wa wajumbe wa tume hiyo.
Walikuwa wanadai kuwa tume hiyo haijakidhi vigezo vya kisheria kwa kuwa uundwaji na uteuzi wa wajumbe wake ulikiuka kanuni ya haki asili ya mtu kutokuwa hakimu wa kesi yake mwenyewe.
Walifafanua kuwa mamlaka ya uteuzi ni mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, chama tawala, ambacho kina masilahi katika uchaguzi huo na tume hiyo kwani kilichoshiriki na kushinda uchaguzi uliosababisha ghasia hizo.
Pia walidai kuwa mjumbe Tax ni mtuhumiwa kwani alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wakati ghasia za uchaguzi zilipotokea, alihusika kwa namna moja au nyingine chini ya wizara yake.
Vilevile walidai kuwa majaji wakuu wastaafu hawawezi kuchunguza kwa haki vurugu hizo kwani baadhi ya mali zilizoharibiwa ni za mahakama waliyoiongoza, na kwamba IGP mstaafu hawezi kumchunguza kwa haki, kwa kuwa, IGP aliyepo anaweza kuwa miongoni mwa watuhumiwa.
Walidai pia Amiri Jeshi Mkuu, mamlaka ya uteuzi wa tume hiyo (Rais) katika tarehe tofautitofauti alitoa maagizo kwa Polisi na Jeshi kujiandaa kwa ghasia za wakati na baada ya uchaguzi.
Katika hoja nyingine walidai kuwa uundaji wa tume hiyo umekiuka masharti ya Sheria ya Tume ya Uchunguzi, Sura 32 Marejeo 2023, kifungu cha 16, kwani hakuna ufafanuzi wa madhumuni yake yaliyo wazi bali yanategemea hisia tu, kinyume na misingi ya Katiba na utawala bora.
Pia walidai maneno yaliyotumika ‘Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani’ yanapunguza na kudharau vifo, watu waliopotea, miili iliyopotea, majeraha na athari kubwa kwa umma kwa jumla.
Hoja nyingine wanadai kuwa Tume hiyo si huru kwa kutokujumuisha wajumbe kutoka vyama huru vya kitaaluma kama asasi za kiraia na wadau wengine huru wasio na mgongano wa masilahi, kuepuka upendeleo kwa mamlaka ya uteuzi.
Walidai wajumbe wote ni watumishi wa umma waliostaafu, waliokuwa na nafasi za kuteuliwa na Rais, waliokula kiapo cha siri kwa Rais, ambacho hakijafutwa wakati wa kustaafu au hadi tarehe ya uteuzi kama wajumbe wa tume inayopingwa, hivyo hawawezi kuchunguza mamlaka ya uteuzi wao.
Hoja nyingine walidai kuwa tume hiyo haikutangazwa katika Gazeti la Serikali wala kula viapo kabla ya kuanza kazi kama sheria zinavyoelekeza.
