📍Yasifu uwekezaji wa shilingi bilioni 429
NA MASHAKA MHANDO, Tanga
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeiashauri Serikali kuongeza kasi ya utatuzi wa changamoto za miundombinu wezeshi katika Bandari ya Tanga, ili kuendana na kasi ya ongezeko la shehena na meli kubwa zinazoingia bandarini hapo kufuatia maboresho makubwa yaliyofanyika.
Ushauri huo umetolewa Leo Machi 13 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Profesa Joyce Ndalichako, wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua utendaji na ufanisi wa bandari hiyo, ambayo hivi sasa imekuwa mbadala muhimu katika kupunguza msongamano wa mizigo kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kukagua gati jipya, Profesa Ndalichako alipongeza uwekezaji wa Shilingi Bilioni 429 uliowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita, akisisitiza kuwa ni lazima kasi ya ujenzi wa barabara za kuingia na kutoka bandarini iongezwe ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo kwenda kwa walaji.
“Kamati inampongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake ya kuifungua Tanga. Tunaunga mkono mpango wa kuunganisha bandari hii na reli ya kisasa ya SGR kutoka Tanga hadi Musoma, hatua itakayochochea tija na ajira kwa wingi,” alisema Profesa Ndalichako.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, alibainisha kuwa Serikali inaendelea na mpango wa kuunganisha bandari hiyo na mtandao wa reli wa kilomita 248 (Tanga–Mruazi–Ruvu) na hatimaye kufika Arusha. Alieleza kuwa reli ya SGR kupitia Minjingu na Engaruka hadi Musoma itakuwa kiunganishi muhimu cha kiuchumi.
Meneja wa Bandari ya Tanga, Salehe Mbega, alieleza kuwa maboresho hayo yameongeza kina cha maji kufikia mita 12, hali inayoruhusu meli kubwa zenye urefu wa hadi mita 200 kutia nanga, tofauti na hapo awali.
“Ufanisi umeongezeka kiasi kwamba meli sasa zinahudumiwa ndani ya siku tatu hadi tano. Hata hivyo, kutokana na ubora wa huduma zetu, mahitaji yameongezeka na wakati mwingine hadi meli 14 husubiri nje ya bandari. Ili kutatua hili, tuna mpango wa kujenga magati matatu mapya na kituo cha kisasa cha abiria (Terminal) katika awamu ya tatu ya mradi,” alisema Mbega.
Maboresho hayo yanatajwa kuwa kichocheo kikubwa cha uchumi wa mkoa wa Tanga, yakigusa sekta za usafirishaji, biashara ndogondogo, na kuimarisha nafasi ya mkoa huo kama kitovu cha uwekezaji nchini.
.jpeg)

.jpeg)

